Tuesday, June 19, 2012

HOTUBA YA MWENYEKITI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA

HOTUBA YA MWENYEKITI WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
MHE. JOSEPH WARIOBA KATIKA MKUTANO WA WAANDISHI WA
HABARI TAREHE 19 JUNI, 2012 KATIKA UKUMBI WA
KARIMJEE, DAR ES SALAAM


Ndugu Wanahabari,

Nianze kwa kuwashukuru kwa kuitikia mwaliko wetu. Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilianza kazi mwanzoni mwa Mwezi Mei, 2012 na kipindi hiki tumekitumia kwa maandalizi na sasa tuko tayari kuanza awamu ya kwanza ya kazi yetu, yaani kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi. Baada ya hapo itafuata awamu ya pili ya kuandaa taarifa, mapendekezo na Rasimu ya Katiba Mpya. Baadaye Tume itakutana na Mabaraza ya Katiba na mwisho Rasimu ya Katiba itafikishwa kwenye Bunge Maalum.

Kabla ya kuanza mchakato wa kushauriana na wananchi, ikiwa ni pamoja na safari za mikoani, tumeona ni muhimu na busara kukutana na nyinyi kwanza. Vyombo vya habari ni wadau wakubwa katika mchakato huu. Tume inaamini kwamba vyombo vya habari vina nafasi kubwa sana katika kufanikisha mchakato mzima hasa katika kutangaza maoni ya wananchi ili, licha ya kukusanya maoni tu, mchakato uwasaidie wananchi kubadilishana mawazo kuhusu aina ya Taifa wanalolitaka na aina ya Katiba wanayoitaka.

Ndugu Wanahabari,
Pamoja nami leo Wajumbe wote wa Tume, ikiwa ni pamoja na Makamu Mwenyekiti - Jaji Augustino Ramadhani, Katibu na Naibu Katibu.

Jukumu tulilokabidhiwa ni kubwa na muhimu kwa Watanzania, hivyo basi matayarisho tuliyokuwa tunayafanya yalikuwa na lengo la kuhakikisha mchakato mzima unakwenda kama ilivyokusudiwa.

Katika maandalizi yetu, tulitambua umuhimu wa elimu kwa umma kuhusu mambo yatakayozingatiwa katika Katiba. Ni wazi kuwa wananchi hawawezi kutoa maoni yao kwa ukamilifu bila ya kuwa na elimu ya kutosha. Kwa hiyo, kwa kuzingatia umuhimu huo, Tume imetumia muda mwingi kupata na kuandaa nyaraka muhimu kwa ajili ya kuwapatia wananchi elimu ya kutosha.

Tume imepata nakala elfu mia tano za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977, nakala elfu kumi za Katiba ya Zanzibar ya 1984 na nakala elfu mia tano za Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83. Kwa kutambua kwamba nyaraka hizi hazitoshi, na hata kama zikipatikana kwa wingi ni vigumu kwa wananchi kuzisoma na kuzielewa kwa urahisi, Tume imeandaa nyaraka ambazo ni rahisi kuzisoma na kuzielewa.

Nyaraka hizo ni Katiba ya Jamhuri ya 1977, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, kwa lugha nyepesi, Hadidu za Rejea, Program ya Elimu kwa Umma na Utekelezaji wa Kazi za Tume. Nyaraka hizi tumeanza kuzisambaza na leo, tunawakabidhi nyinyi nyaraka zote ili msaidie kuzitangaza na kuelemisha wananchi. Aidha, Tume imeandaa vipeperushi kuhusu kazi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara.

Ndugu Wanahabari,
Hivi karibuni Tume itaanza safari za mikoani. Tume imejigawa katika makundi saba na kila kundi litafanya safari nne mikoani kati ya sasa na mwisho wa mwaka. Kila kundi litafanya kazi katika mkoa kwa wastani wa mwezi mmoja isipokuwa kwenye mikoa iliyo midogo kwa eneo, ambapo Tume itatumia muda mfupi. Tutaanza na mikoa minane ambayo ni Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga.

Tunaomba wananchi wajitokeze kwa wingi na kutoa maoni yao kwa uhuru, uwazi, bila ya hofu yoyote na kwa utulivu. Tunaomba wananchi wawe wavumilivu na watoe maoni bila jazba au kubeza. Tunaomba wananchi wawe wavumilivu sana kusikiliza mawazo ya wengine hata kama hawakubaliani na mawazo hayo.

Lengo letu kama Tume, ni kuhakikisha kuwa Watanzania kwa jumla wanatoa maoni yao. Tungependa sana kama ingeliwezekana, kila Mtanzania apate fursa ya kutoa maoni yake. Lakini, ukizingatia ukubwa wa nchi yetu na mazingira halisi, ni wazi haitawezekana kuonana na kila mtu. Pamoja na hivyo, ni kusudio letu kufanya kila linalowezekana kupata mawazo ambayo yataonyesha matakwa, mategemeo na mahitaji ya Watanzania wote. Katika upeo huo, basi tutafanya kila jitihada kwa njia mbali mbali kujaribu kuhakikisha kwamba maoni ya Watanzania kwa ujumla yanawasilishwa na kufanyiwa kazi vilivyo.

Pamoja na mikutano mbali mbali itakayofanyika katika mikoa yote, tutakuwa na mfumo wa kupokea maoni ya Watanzania wa kutoka pande zote za ndani ya nchi na nje ya nchi kupitia simu, barua pepe, mitandao ya kijamii kama facebook, twitter na blogu na tovuti na pia kwa njia ya posta. Tunaomba wananchi wajitahidi kutoa hoja badala ya malalamiko peke yake. Mapendekezo ya mambo ya kuingia kwenye Katiba yatasaidia sana badala ya malalamiko tu.

Tume, kwa kiwango fulani imeanza kuratibu maoni ya wananchi yanayotolewa kwa njia mbali mbali. Mwelekeo wa kubaini maeneo ya kufanyia kazi unaanza kuonekana, hasa kuhusu taasisi za dola kama vile Serikali na vyombo vyake vyote na madaraka ya viongozi na taasisi mbali mbali. Tume inaomba maeneo mengine muhimu nayo yapewe uzito, hasa maeneo yaliyo katika Sura ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Sehemu hiyo ndiyo moyo wa Katiba. Yapo maeneo manne muhimu ambayo Tume ingependa kupata maoni ya wananchi.

Eneo la Kwanza, linahusu misingi ya Taifa. Misingi ndiyo nguzo ya utamaduni wa nchi na wananchi wake; misingi ndiyo nguzo ya nidhamu ya nchi na wananchi wake; misingi ndiyo nguzo ya maadili ya nchi na wananchi wake. Katiba yetu imetaja misingi mikuu kuwa ni uhuru, haki, udugu, amani, demokrasia na Serikali kutofungamana na dini yoyote ingawa wananchi wana uhuru wa kuabudu. Misingi hii ndiyo nguzo ya mshikamano na utulivu wa wananchi. Baadhi ya watu wanasema ama misingi hii haitoshi au imetelekezwa. Wengine wanasema inatosha. Tume ingependa kupata maoni ya wananchi kuhusu eneo hili.

Eneo la Pili, ni kuhusu mamlaka ya wananchi. Katiba ya sasa inaeleza kwamba wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na msukumo mkubwa wa mchakato huu wa kupata Katiba Mpya ni matakwa ya kuwawezesha wananchi kutunga Katiba yao. Lakini kuna watu wanasema mamlaka ya wananchi hayakufafanuliwa, wanasema mamlaka ya taasisi za dola kama vile Serikali, Bunge, Mahakama, Tume mbali mbali za kikatiba, na hata Vyama vya Siasa, yamefafanuliwa. Lakini mamlaka ya wananchi hayakufafanuliwa na wala hakuna utaratibu wa kuyatumia madaraka hayo. Wanasema wananchi wanatumiwa tu kisiasa wakati mamlaka yao yote yameporwa. Wengine wanasema mamlaka hayo yapo isipokuwa wananchi wameyakasimu kwa taasisi mbali mbali. Tume ingependa kupata maoni ya wananchi kuhusu eneo hili.

Eneo la Tatu, ni malengo muhimu na misingi ya mwelekeo wa shughuli za Serikali. Malengo hayo yameelezwa vizuri sana katika Ibara ya 9 ya Katiba. Baadhi yake ni:-


  • Kwamba utu na haki nyinginezo zote za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa;



  • Kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine;



  • Kwamba mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi;



  • Kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini.



  • Kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada za kuondosha umaskini, ujinga na maradhi;



  • Kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache binafsi.


Malengo haya ndiyo ndoto (vision) ya wananchi. Malengo haya ndiyo yanajumuisha matumaini ya Watanzania kuhusu aina ya Tanzania wanayoitaka. Mgawanyo wa madaraka kwa mamlaka mbali mbali za dola unakusudiwa kuhakikisha kwamba malengo haya yanafikiwa.

Baadhi ya watu wanasema kuwa malengo haya yanatosha ila hayatekelezwi kwa ukamilifu. Wengine wanasema kuwa hayatoshi katika zama hizi. Tume ingependa kupata maoni ya wananchi kuhusu malengo muhimu ya Taifa. Tume itapenda kufahamu ndoto za wananchi kuhusu rasilimali za Taifa na jinsi ya kuzilinda, kuziendeleza na kuzitumia kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Tume ingependa kusikia ndoto za wakulima, wafanyakazi, wafugaji, wavuvi, wafanya biashara wakubwa na wadogo, wanaume, wanawake, wazee, vijana, walemavu na kadhalika.

Eneo la Nne, ni haki za binadamu na wajibu kwa jamii. Sehemu ya Tatu ya Sura ya Kwanza ya Katiba ina orodha ndefu ya haki na wajibu muhimu kwa raia. Baadhi ya watu wanasema haki hizi hazitoshi. Wengine wanasema haki za mtu binafsi zinadhulumu haki za jamii na wengine wanasema haki za binadamu zinaminywa au hazitekelezwi kwa ukamilifu au zinavunjwa. Tume inapenda kupata maoni ya wananchi.

Ndugu Wanahabari,
Awamu ya Pili ya uratibu na ukusanyaji wa maoni ya wananchi itafanyika kupitia Mabaraza ya Katiba. Wakati huo, Tume itawaomba wananchi watoe maoni yao kuhusu Rasimu ya Katiba. Kupitia kwenu, naomba wananchi kufika kwa wingi katika mikutano ya ukusanyaji wa maoni katika awamu zote mbili. Nawaomba wananchi kutoa mawazo yao kwa uwazi na bila ya hofu yoyote. Tume itafanya kazi zake kwa uhuru, uwazi na tunawahakikishia kwamba maoni yote yatakayotolewa na wananchi, taasisi, asasi za kiraia na makundi mengine yote yataheshimiwa na kufanyiwa kazi ipasavyo.

Ndugu Wanahabari,
Nimalizie kwa kurudia tena kwamba jukumu la vyombo vya habari ni kubwa katika kufanikisha kupatikana kwa Katiba Mpya. Pamoja na mambo mengine, wananchi wa sehemu moja ya nchi watafahamu maoni ya wenzao katika sehemu nyingine ya nchi. Naomba mlikubali jukumu hili ili kusaidia nchi ipate Katiba Mpya iliyo nzuri.

Nawashukuru.

TOA MAONI, TUPATE KATIBA MPYA

No comments: