Tuesday, August 7, 2012

" Haaa Eti Wabunge Wetu Nao Wanalewa Kazini, Wanavuta Sigara Kali"

WAKATI kashfa ya baadhi ya wabunge kuhongwa na kampuni za mafuta ili yatetee mikataba yao haijapoa, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai ameibua tuhuma nyingine nzito kwamba baadhi ya wawakilishi hao wamekuwa wakiingia kwenye vikao wakiwa wamelewa pombe na sigara zisizo za kawaida.

Katika siku karibuni, baadhi ya wabunge wamekuwa wakinaswa na kamera wakiwa wamelala bungeni wakati vikao vinaendelea, kwa maelezo ya uchovu, kauli ambayo huenda sasa ikaongeza mjadala miongoni kama kinachosababisha walale wakati vikao vinaendelea iwapo ni uchovu wa kazi au ulevi.

“Kuna wabunge ninavyohisi wanaingia bungeni wakiwa wamevuta sigara fulani kubwa, kulamba vitu fulani au hata kupata bia mbili tatu,” alisema Ndugai akihojiwa jana asubuhi katika kipindi cha medani za siasa na uchumi cha Star tv.Ndugai alisema amekuwa akiona hali hiyo hasa Bunge la kuanzia mchana, bila kueleza ni hatua ambazo zimekuwa zikifanyika kupambana na wawakilishi hao wa wananchi wanapobainika wamelewa.

“Wabunge ni watu kama watu wengine, wana tabia kama walivyo wanadamu wengine, wapo ambao kwa namna ninavyohisi wanaingia bungeni hasa vikao vya kuanzia mchana wakiwa wamepiga bia,” alisisitiza
Ndugai ambaye ni Mbunge wa Kongwa, mkoani Dodoma.

Ingawa hakufafanua, inavyofahamika sigara yenye kulevya ni bangi,kulamba vitu fulani vyenye kulewesha maana yake inaweza kuwa kuna baadhi ya wabunge wanatumia dawa za kulevya, pia ulevi mwingine wa kutumia bia. Bila kueleza hatua ambazo Bunge linachukua kwa wabunge walevi, Ndugai aliwataka wabunge kuweka maslahi ya taifa mbele na kujenga tabia ya kuongea mambo wakiwa na ushahidi.

“Ni kwamba kuna wabunge wamekuwa wakizungumza mambo bila ushahidi, hili jambo halikubali, wabunge wanapaswa kuzingatia sheria kama walivyo Watanzania wengine, unapomtuhumu mtu lazima uwe na
ushahidi, lakini inasikitisha sana unakuta mbunge anasema jambo, anamtaja mtu kwamba anahusika na hili na lile wakati hana hata chembe ya ushahidi,” alisema.

Pia, aliwataka wanasiasa wote kujenga tabia za kuthamini yale ambayo yanafanywa na wanasiasa wengine.

“Nimekuwa nikifuatilia mambo yanavyokwenda nchini, kuna wanasiasa wanakosea, unakuta mpinzani amekuwa akisema mabaya tu kwa chama tawala, unakuta tunaitwa mafisadi, siyo sahihi, kwa mfano Star tv kukawa na mtu mgoni, ni tatizo la huyo haina maana kwamba wafanyakazi wote ni wagoni. CCM ni taasisi kubwa, mambo haya yanaweza kutokea.

Lakini pia siyo kweli kwamba wanachama na viongozi wote wa upinzani ni wasafi,” alisema Ndugai na kuongeza: “Kuna wanasiasa wamekuwa na tabia ya kuona kila kinachofanywa na CCM ni ushetani, hiyo siyo sawa! Kwa mfano mimi jimboni nimefanya maendeleo mengi. Wakati naingia Bungeni mwaka 2000 kulikuwa na shule chache mno za sekondari, lakini sasa ziko zaidi ya 30, hata zahanati zilikuwa chache sasa ni zaidi ya 40, ni kutokana na jitihada zangu na chama changu, mtu anapokuja kusema hatujafanya kitu tunashindwa kumuelewa.” 

Naibu Spika huyo alikwenda mbali zaidi na kuwashauri viongozi wa Serikali akiwamo Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa na utaratibu wa kupitia kauli zinazotolewa na wanasiasa, kwa maelezo kuwa baadhi yao
wamekuwa wakitoa kauli nzito, au kukashifiana bila kuchukuliwa hatua.

“Unaweza kukuta mwanasiasa anaibua kashfa nzito, lakini hachukuliwi hatua wala kuulizwa, hiyo siyo sahihi. Wanasiasa tunapaswa kubishana kwa hoja, siyo vinginevyo,” alisema Ndugai.

Ndugai alipoulizwa kuwa wabunge hao hatua watakazochukuliwa kutokana na tabia zao, alisema suala hilo haina haja ya kulizungumzia zaidi ila libaki kama alivyosema.

“Hilo siwezi kulizungumzia zaidi libaki kama nilivyozungumza na walioniomba nizungumze nao,” alisema. CHANZO: MWANANCHI.

Madaktari Kujadili Hali Ya Dr Ulimboka

WAKATI kukiwa na taarifa za kurejea nchini kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka viongozi wa Jumuiya hiyo na Umoja wa Madaktari Tanzania (MAT), wanatarajia kukutana leo kujadili mkanda mzima wa sakata lililomkumba kiongozi huyo.  Baada ya kikao hicho, madaktari hao watakutana na familia yake na kisha kumuuliza Dk Ulimboka kama angependa kilichomtokea kiwekwe wazi kwa jamii.

 Dk Ulimboka ambaye alikuwa anaratibu mgomo wa madaktari uliokuwa ukiendelea nchi nzima, alitekwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Jumatato ya Juni 27 mwaka huu na kupelekwa katika msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji a Dar es Salaam, ambako aliteswa na kujeruhiwa vibaya.

Katika tukio hilo daktari huyo aling’olewa meno mawili na kucha za mkono mmoja na baadaye kulazwa katika Kitengo cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalum (ICU) katika Taasisi ya Mifupa (MOI).  Baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya Juni 30 mwaka huu, alisafirishwa kwenda Afrika a Kusini kwa ajili ya vipimo na matibabu.

 Kusafirishwa kwake kulifuatia taarifa ya jopo la madaktari lililokuwa linamhudumia kutoa taarifa kwa madaktari bingwa kuhusu abadiliko ya afya.

 Taarifa za kurejea kwa Dk Ulimboka zimezagaa katika mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam, huku baadhi ya watu wakizijadili katika mitandao ya kijamii.  Akizungumza na gazeti hili Katibu wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Edwin Chitage, alisema kuwa hali ya Dk Ulimboka inazidi kuimarika lakini alisita kueleza wazi ni lini kiongozi huyo wa madaktari atarudi nchini.

 “Tukiwa tayari tutatoa taarifa katika vyombo vya habari juu ya suala zima la afya ya Dk Ulimboka,” alisema Dk Chitage.  Alisema leo au kesho viongozi mbalimbali wa MAT na Jumuiya ya Madaktari, watakutana kujadili suala la kiongozi huyo.

 “Ndani ya siku mbili hizi (leo na kesho) viongozi tutakutana na kujadili ripoti ya matibabu ya Dk Ulimboka na tutajadili kama tuvieleze vyombo vya habari ama laa,” alisema Dk Chitange.  Hata hivyo Dk Chitange alisema hatua hiyo itategemea na kauli ya familia ya Dk Ulimboka na  yeye mwenyewe (Dk ULimboka) kwa kuwa na wao pia watashirikishwa.

 “Dk Ulimboka na familia yake tutawashirikisha katika mambo ambayo tutayajadili,” alisema Dk Chitage. 

    Alipoulizwa kama kiongozi huyo wa madaktari sasa anaweza kufanya shughuli zake kama awali, alisema hana uhakika kwa kuwa hana taarifa za ndani zaidi . CHANZO: MWANANCHI

RAIS JAKAYA KIKWETE AELEKEA KAMPALA LEO

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Rubani Bomani na wanaanga wenzie  wa Ndege za Serikali  kabla ya kuanza safari ya kwenda Kampala, Uganda, kuhudhuria mkutano wa nchi za Maziwa Makuu asubuhi leo Agosti 7, 2012
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisindikizwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Mhe Saidi Mecky Sadik  kabla ya kuanza safari ya kwenda Kampala, Uganda, kuhudhuria mkutano wa nchi za Maziwa Makuu asubuhi leo Agosti 7, 2012
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi la Tanzania,  Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo  kabla ya kuanza safari ya kwenda Kampala, Uganda, kuhudhuria mkutano wa nchi za Maziwa Makuu asubuhi leo Agosti 7, 2012. Katikati yao ni Inspekta Jenerali wa Polisi, Saidi Mwema.

(PICHA NA IKULU)

MADHARA YA UNENE, YANASHINDA YA UVUTAJI SIGARA!

TAARIFA hii inaweza kuwashangaza baadhi ya watu, lakini takwimu zilizotolewa hivi karibuni zilizowahusisha zaidi ya watu 60,000 nchini Kanada, zinaonesha kwamba unene una madhara zaidi kuliko uvutaji sigara.

Taarifa kwamba unene ni hatari kwa afya, unaweza kuwashangaza watu wengi hasa ukizingatia kwamba hivi sasa watu kuwa wanene na wenye matumbo makubwa, limekuwa ni jambo la kifahari na la kawaida.

Utafiti huo unaonesha pia kuwa kama kusingekuwepo na tatizo la unene wa kupindukia (obesity) kwa watu wengi duniani, basi safari za kwenda hospitali kwa matatizo mbalimbali ya kiafya, nayo yangepungua kwa zaidi ya asilimia 10.

UNENE WA KUPINDUKIA, CHANZO CHA MARADHI
Ni muhimu watu kuondokana na imani potofu kuwa unene ni dalili ya afya njema, badala yake waelewe kwamba unene wa kupindukia ni chanzo cha maradhi ukiwemo ugonjwa wa kisukari (diabetes type 2).

Licha ya vyakula vya mafuta mengi kuchangia unene, vyakula vingine vya kawaida vinavyoliwa na watu wengi, vimetajwa kuwa hatari zaidi kwa kuongeza unene.
Baadhi ya vyakula hivyo ni pamoja na keki, chips, vitumbua, maandazi, soda, nyama za kukaanga, unywaji wa soda, vinywaji vya kutia mwili nguvu (energy drinks) na vyakula vingine vitamu vitamu na vyenye sukari nyingi.

Ni ukweli ulio dhahiri kwamba, unene wa kupindukia una uhusiano mkubwa na magonjwa sugu na una athari pia katika umri wa kuishi binadamu na kwamba soda inachangia sana kuongeza uzito mwilini.

Kujua namna ya kuishi kwa kula vyakula kwa kuchagua kwa kigezo cha kula chenye faida tu mwilini, ndiyo dawa pekee na ya uhakika ya kujikinga na kupambana na maradhi hatari.

Pendelea kula vyakula asilia na jiepushe kula vyakula vilivyotayarishwa na kuhifadhiwa (vyakula vya makopo na vya kwenye maboksi) na badala yake pendelea kula vyakula asilia na vilivyo ‘fresh’. Kama ni nafaka, kula vyakul

Jiepushe na ulaji wa kiasi kingi cha sukari (kwa kupitia njia mbalimbali, kama soda, juisi, n.k), kwani sukari inachangia kwa kiasi kikubwa kudhoofisha kinga ya mwili na kuchochea chembechembe za saratani mwilini.

Hakikisha pia unafanya mazoezi mara kwa mara. Hata kama unakula chakula bora kuliko watu wote duniani, kama hufanyi mazoezi lazima utapatwa na matatizo ya kiafya. Mazoezi na shuruba za mara kwa mara, huongeza uzalishaji wa homoni za ukuaji wa mwili (Human growth hormone).

Hakikisha unakunywa maji safi na salama kwa wingi kila siku ili kuuweka utumbo wako safi. Kama inavyoelezwa, kifo huanzia tumboni, huna budi kuhakikisha tumbo lako linakuwa safi kila siku kwa kunywa maji ya kutosha yatayokuwezesha kupata choo kila siku na kwa kufanya hivyo utauweka utumbo wako safi.

Mwisho, hakikisha unapata muda wa kupumzika na kulala usingizi wa kutosha kila siku, kwani ukosefu wa usingizi na kuacha kupumzika vina athari sana kwenye uzalishaji wa homoni muhimu mwilini.

GODBLESS LEMA ATUA UINGEREZA KUONGEZA CHOPA

Mheshimiwa Godbless Lema wa Chadema akikagua Helikopter ikiwa ni moja ya vitendea kazi vya kampeni za 'M4C'. Mheshimiwa Lema, pamoja na kufanya maandalizi hayo ya vitendea kazi, kesho Jumanne Agosti 7 anatarajiwa kufungua tawi la Chadema jijini London saa mbili usiku, Thatched House Barking kwa ushirikiano mkubwa na Makamanda wa Serengeti Freight Forwarders.

Yanga Yapeleka Kombe La Kagame Bungeni

 Wachezaji wa Yanga wakiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri Mkuu , Fatuma Karume ,wabunge na Kocha wao wakiwa na Kombe lao la Kagame Bungeni mjini Dodoma.
 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mama Fatuma Karume wakishikilia Kombe la Kagame lililotwaliwa na  Yanga hivi karibuni lililoletwa na wachezaji wa Yanga na Viongozi wao akiwemo Kocha wao mpya Tom Saintfiet Bungeni mjini Dodoma.
 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na Mke wa Rais, Marehemu Abeid Amani Karume Mama Fatuma Karume kwenye Viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Mke wa Rais, marehemu Abeid Amani Karume Mama Fatuma Karume ambae ni Mfadhiri wa Yanga kwa pamoja wakiingia Bungeni pamoja na Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji kupeleka kombe la Kagame Bungeni.

Chanzo: Anna Nkinda, Maelezo

Magazeti ya Leo Jumanne 7th August 2012