Friday, June 22, 2012

CHADEMA WANGECHUKUA NCHI HIVI LEO,BARAZA LA MAWAZIRI LINGEKUWA HIVI


Spika acha kupendeelea - Mbowe

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoundwa na wabunge wa Chadema, Freeman Mbowe amedai kuwa ugomvi ndani ya Bunge unatokana na meza ya Spika pamoja na wasaidizi wake kuwaonea wabunge wa upinzani na kuwapendelea wabunge wa CCM.

Mbowe, ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema, alitoa hoja hiyo jana ndani ya Bunge wakati akichangia hotuba ya Bajeti ya Serikali na pia alisisitiza suala hilo wakati alipofanya mkutano na waandishi wa habari.

Wakati anatoa hoja hiyo bungeni, Spika wa Bunge Anne Makinda alimjibu kuwa yeye pamoja na wasaidizi wake ambao ni Naibu Spika na wenyeviti watatu wa Bunge hilo wanatimiza majukumu yao kwa kuzingatia kanuni namba nane ya Bunge.

“Kuna mkakati wa makusudi wa kuwalinda wabunge wa CCM hata pale wanapovunja kanuni za Bunge na wanapowadhalilisha wabunge wa Chadema, na sisi tunapojibu kwa nguvu ile ile, meza ya Spika wanakuwa wakali kuchukua hatua,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema hatua hiyo inawafanya wabunge wa upinzani wawe na hasira kwani hata pale wanapoomba mwongozo inamchukua muda mrefu kwa Spika au wasaidizi wake kuwaruhusu kufanya hivyo.

“Meza yako Spika ikiyumba pamoja na wasaidizi wako na ikikubali kuubeba upande mmoja na kuchukua hatua kali upande mwingine, ni wazi kuwa hapo hakuwezi kuwepo amani,” alisema Mbowe.

Alitoa mfano Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba (CCM) akidai alitoa dhihaka juu ya maoni ya Kambi ya Upinzani ya Bajeti hadi akaitupa lakini hakuna hatua zilizochukuliwa na kiti cha Spika.

TIMU 20 KUCHEZA LIGI DARAJA LA KWANZA


Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeridhia mapendekezo ya Kamati ya Mashindano ya kutaka Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuwa na timu 20 badala ya 18 za sasa.
Lengo la mabadiliko hayo ni Ligi ya Taifa (NL) kuchezwa kwa kanda, hivyo

msimu huu timu mbili zaidi (ukiondoa tatu ambazo zimeshapanda kutoka NL) zitaongezwa ili kufikisha idadi ya timu 20 katika FDL.
Timu ambazo zimepanda kutoka NL iliyochezwa katika vituo vitatu ni; Kanembwa JKT ya Kigoma iliyoongoza Kituo cha Kigoma, Ndanda SC ya Mtwara iliyoibuka kinara Kituo cha Mtwara na Polisi Mara iliyokamata usukani katika Kituo cha Musoma.

Kamati ya Utendaji pia imepitisha mapendekezo ya kuchezwa play off ili kupata timu mbili zaidi za kucheza FDL msimu huu. Timu zitakazocheza play off katika utaratibu utakaotangazwa baadaye na Kamati ya Mashindano ni tatu zilizoshuka kutoka FDL na tatu nyingine zilizoshika nafasi za pili katika NL kutoka vituo vya Kigoma, Mtwara na Musoma.

Timu tatu zilizoshuka FDL ni AFC ya Arusha, Samaria ya Singida na Temeke United ya Dar es Salaam wakati zilizoshika nafasi za pili katika NL na vituo vyao kwenye mabano ni Kurugenzi ya Iringa (Mtwara), Mwadui ya Shinyanga (Kigoma) na Tessema ya Dar es Salaam (Musoma).
Hata hivyo, timu zitakazoshuka kutoka Ligi Kuu bado zitaendelea kuwa tatu kama ilivyo kwa zitakazopandwa.

AWAMU YA KWANZA USAJILI MWISHO AGOSTI 10
Kipindi cha kwanza cha usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu wa 2012/2013 kitamalizika Agosti 10 mwaka huu kulingana na kalenda ya Matukio ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ya 2012/2013.
Uhamisho wa wachezaji unafanyika kuanzia Juni 15 hadi Julai 30 mwaka huu wakati kipindi cha kuacha wachezaji (sio wa Ligi Kuu. Wachezaji wa Ligi Kuu wanacheza kwa mikataba) ni kuanzia Juni 15- 30 mwaka huu.

Kwa klabu za Ligi Kuu kutangaza wachezaji watakaositishiwa mikataba yao ni kuanzia Juni 15-30 mwaka huu na usajili wa wachezaji unafanyika kuanzia Juni 15 hadi Agosti 10 mwaka huu.
Tunasisitiza kipindi cha usajili kiheshimiwe na mikoa yote kwa sababu usajili huo huo ndiyo utakaotumika katika michuano ya Kombe la FA. Kwa maana nyingine hakutakuwa na kipindi kingine cha usajili wa wachezaji kwa klabu zote nchini hadi hapo litakapofunguliwa dirisha dogo.

Mechi ya kufungua msimu ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kati ya mabingwa wa Ligi Kuu, timu ya Simba na makamu bingwa Azam itachezwa Agosti 25 mwaka huu wakati Ligi Kuu itaanza Septemba Mosi mwaka huu, na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) yenyewe itaanza Septemba 15 mwaka huu.
Ratiba ya Ligi Kuu itatolewa Julai 23 mwaka huu.

MISRI YAOMBA KUIKABILI NGORONGORO HEROES
Chama cha Mpira wa Miguu Misri (EFA) kimeomba mechi mbili za kirafiki kwa timu yao ya vijana na timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Tanzania (Ngorongoro Heroes).


EFA imeomba mechi hizo zichezwe Julai 3 na Julai 5 mwaka huu kwa masharti maalumu. Ikiwa zitachezwa Misri, mwenyeji (EFA) atagharamia Ngorongoro Heroes kwa malazi, chakula, usafiri wa ndani na sehemu ya kufanyia mazoezi.

Ikiwa mechi hizo zitachezwa Dar es Salaam, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litaigharamia timu ya Misri kwa malazi, chakula, usafiri wa ndani na sehemu ya mazoezi. Hivyo kila timu itajigharamia kwa usafiri wa ndege na posho kwa timu yake.
Sekretarieti ya TFF inafanya uchambuzi wa gharama ili kujua ipi ni nafuu kabla ya kufanya uamuzi wa wapi mechi hizo zichezwe.

Ngorongoro Heroes imeingia raundi ya pili ya michuano ya Afrika ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Algeria baada ya kuitoa Sudan katika raundi ya kwanza.
Itacheza mechi ya kwanza ya raundi ya pili Julai 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati ya marudiano itakuwa Agosti 11 mwaka huu nchini Nigeria.

HAIJALISHI TOFAUTI YA UMRI.. HUYU NDIO ROBERT EVANCE ANAYEMNYIMA TYRA BANKS USINGIZI

WAKIWA WAMETOFAUTIANA UMRI KWA MIAKA 14 LAKINI TYRA BANKS AMEONESHA KUTO KUJALI HILO NA KUENDELEA KIJIRUSHA NA KISINGLE BUTTON CHAKE HIKI AMBACHO KWA SASA AMEKIFANYA JUDGE WA ILE CIRCLE YA 19 YA AMERICAN NEXT TOP MODEL.
ROBERT EVANCE AMBAYE NI MODEL MWENYE UMRI WA MIAKA 24 KWA SASA AMEONEGANA KUNOGEWA NA PENZI LA MAMA HUYU MWENYE MAFANIKIO ZAIDI KUPITIA MITINDO.. KATIKA SIKU ZA HIVI KARIBUNI.. WADAU WENGI WA MITINDO MAREKANI WAMEKUWA WAKIJIULIZA... TYRA AMEKUWA NEW JENNIFER LOPEZ? MAANA JENNIFER LOPEZ HAONI AIBU KUJIINGIZA KATIKA MAPENZI NA VIJANA WADOGO.

MCHEZA SINEMA WA MAREKANI, DEIDRE LORENZ ATUA MJINI MOSHI NA SHAUKU KUBWA YA KUONA KAMA KWELI MLIMA KILIMANJARO UKO TANZANIA

                              Deidre Lorenz na Rais wa IBF-USBA bala la Africa,

 Mcheza sinema toka Marekani Deidre Lorenz amewasili mjini Moshi tayari kushiriki kwenye mbio za Mt. Kilimanjaro Marathon zitakazofanyika juni 24. Lorenz amwasili jana na ndege ya Ethiopian Airlines ambao ndio wafadhali wa mbio za Mt. Kilimanjaro Marathon zinazofanyika jumapili ya mwisho ya mwezi wa sita kila mwaka.

Ujio wa Lorenz ambaye amecheza sinema nyingi zikiwamo Santorini Bule, Perfect Strangers, The Big Fight umeleta msisimko mkubwa katika mji huu mkuu wa Kilimanjaro. Ujio wake umefuatia matayarisho ya muda mrefu ambayo yanaendana na hadhi yake.

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika kumshuhudia mcheza sinema huyu, Lorenz alisema kuwa ameisikia kuwa mlima wa Kilimanjaro uko Kenya kwa kwa muda mrefu na ana furaha kubwa sana ya kufika ili kushughudia kuwa mlima huu maarufu duniani uko Tanzania. “Nimekuwa nautangaza sana ujio wangu kwenye blog na tovuti yangu, wapenzi wangu pamoja na watu wengi wanangojea kurudi kwangu nikawaambie niliyoyashughudia” alisema Deidre Lorenz ambaye ameshawahi kuteuliwa zaidi ya mara tatu kwa tuzo za Oscar. Lorenz alisema kuwa kwa miaka mingi alifikiri kuwa mlima Kiliamnjaro uko Kenya kwa jinsi nchi hiyo jiraniminavyoutangaza nchini Marekani.

“Sasa nimeona mwenyewe kwa macho yangu kuwa kweli mlima (Kilimanjaro) huu maarufu duniani uko Tanzania na sio Kenya” alisema Deidre Lorenz ambaye anaishi kwenye jiji la New York City linalofahamika kama jiji la pesa (International Financial Capital) la kimataifa. Lorenz ameshukia katika hoteli ya Bristol Cottages iliyopo karibu na benki ya Standard Chattered mkabala na bustani ya Manispaa ya Uhuru Park.

Mji wa Moshi na viunga vyake vinarindima kwa ujio wa watalii wengi kutoka Marekani ambao wamekuja kushiriki kwenye mbio hizi zilizojijengea umaarufu mkubwa kwa kuitangaza Tanzania nchini Marekani. Mbio za Mt. Kilimanjaro Marathon zilianzishwa na Marie Frances mwaka 1991 baada ya kuombwa na balozi wa zamania wa Tanzania nchini Misri.

Mbio hizi zimejijengea umaarufu mkubwa na zimeshawahi kupata tuzo nyingi baadhi zikiwa zimetolewa na Wonders of the World Magazine lenye wasomaji zaidi ya milioni 5 likiwa limezipa nafasi ya 2 kama mbio zenye hadhi ya kukimbiwa duniani wakati jarida la Forbes la Marekani lenye wasomaji wengi duniani limeipa nafasi ya kwanza. Ndio maana Manispaa ya Moshi itampa barabara na kuiita “Marie Frances Boulevard”mwaka 2009.

Mbio hizi hukimbiwa na watalii wa Warekani wanaokuja Tanzania kupanda mlima Kilimanjaro na kutembelea mbuga za wanyama. Mt. Kilimanjaro Marathon zinajulikana kama 7 continental races zikiwa zinakimbiwa katika mabara 7 ya dunia.

Ratiba ya Deidre Lorenz inaonyesha kuwa leo ijumaa atakitemnbelea kituo cha watoto yatima cha Upendo kinachoendeshwa na watawa wa Precious Blood. Lorenz atakaa na watoto hao na kuwasomea hadithi mbalimbali za watoto zilizoandikwa na Waltz Disney mwandishi maarufu wa karne ya ishirini wa Marekani.

Siku kesho jumamosi atatembelea hospitali ya KCMC ambapo atakutana na manesi ili kuwapa shavu kwa kazi yao nzuri wanayoifanyia jamii. Jioni ya jumamosi atahudhuria Pasta Party ambapo atapata nafasi ya kukutana na wakimbiaji wengine na kuchagua namba ya kukimbia kesho yake siku ya jumapili tarehe 24 juni.

RAMADHANI SHAULI AONESHWA MKANDA WA UBINGWA WA IBF AFRICA ATAKAOGOMBANIA IDDI PILI


                       Ramadhani Shauli akiwa na mkanda wa ubingwa wa IBF Africa
Bondia  Ramadhani Shauli akiwa ameushika Mkanda wa I.B.F Africa wakati ulipokuwa ukioneshwa mbele ya waandishi wa habari baada ya kuwasili Dar es salaam jana ukitokea USA mkanda huo utakaogombaniwa na Shauli na bondia Sande Kizito kutoka Uganda utafanyika siku ya Iddi pili katika ukumbi wa Diamond Jubilee kushoto ni Makamu wa Rais wa Kamisheni ya Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) Madaraka Nyerere na Promota wa mpambano huoMkurugenzi wa Kitwe General Traders, Lucas Rutainirwa

 Bondia Nassibu Ramadhani kushoto na Ramadhani Shauli wakifungu mkanda wa ubingwa wa IBF Africa utakaogombaniwa na Ramadhani Shauli kushoto na bondia Sande Kizito kutoka Uganda

Mtoto Mchanga akutwa ametupwa akiwa amefariki karibu na Msikiti wa Soweto jijini Mbeya Asubuhi hii


 Katika hali ya kutatanisha wananchi wa Soweto jijini Mbeya wamekutana na Kifurushi ambacho ndani yake kulikuwa na mtoto mchanga amewekwa na kutupwa akiwa amefariki, ikiwa ni tukio la pili kutokea eneo hilo baada ya tukio kama hilo kutokea wiki mbili zilizopita.

 Hata hivyo akiongea na baadhi ya wananchi ambao hawakupenda kutaja majina yao wamedai kwamba kuna dispensary jirani hapo ambayo hawakutaka sema ni hospital ipi ambapo wana wasi wasi kwamba hutoa Mimba mabinti na kuwatupa eneo hilo. Jamani Binadamu tumekuwa wanyama huu ndio mwisho wa dunia, wanawake tunataka nini Jamani??
 Kwa picha na habari zaidi tembelea Mbeya yetu Blog

LULU AKAANGWA NA MAWAKILI WA SERIKALI JUU YA UMRI WAKE


MAWAKILI wa Serikali jana waliwasilisha vielelezo Mahakama kuu kuthibitisha kwamba umri wa msanii wa filamu Elizabert Michael ni zaidi ya miaka 18.Habari zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na mawakili wawili; mmoja wa Lulu na mwingine wa Serikali ambao hawakutaka kutajwa, zimeeleza kuwa vielelezo hivyo vimewasilishwa jana mahakamani hapo.
Habari zimeeleza kuwa moja ya vielelezo hivyo vya Jamhuri ni Mkanda wa video aina ya CD, yenye mahohjiano kati ya mshtakiwa huyo na mtangazaji mmoja nchini.

"Vingine ni maelezo ya mshtakiwa huyo aliyoyatoa polisi wakati alipohojiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili, maombi ya hati ya kusafiria (Passport) na maombi ya leseni ya udereva, alisema mmoja wa mawakili hao.

 Awali vielelezo hivyo walitakiwa kuviwasilishwa juzi, lakini ilishindikana na badala yake vikawasilishwa jana.

 Baada ya vielelezo kesi hiyo itasikilizwa Juni 25 mwaka huu. Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akituhumiwa kumuua msanii mwenzake, Marehemu Steven Kanumba aliyefariki dunia nyumbani kwake Sinza, April 7, 2012.

 Hata hivyo umri wake umezua utata baada ya mawakili wake wanaomtetea kudai kuwa bado ni mtoto kwa kuwa ana umri wa miaka 17 na si 18 kama hati ya mashtaka inavyoonyesha.

 Hivyo mawakili hao walilazimika kuwasilisha maombi mahakamani kuiomba mahakama iruhusu ufanyike uchunguzi wa umri sahihi wa mshtakiwa huyo na ikiridhika kuwa ni mtoto basi kesi yake iendeshwe kwa misingi ya kesi za watoto wanaokinzana na sheria ili kulinda maslahi yake.

 Juni 11, 2012 Mahakama Kuu ilikubali yenyewe kufanya uchunguzi huo kwa lengo la kubaini usahihi wa umri wa mshtakiwa huyo na ikaziagiza na kuzipangia tarehe pande zote katika kesi hiyo kuwasilisha mahakamani hapo vielelezo watakavyovitumia katika hoja zao.

 Jopo la mawakili wanaomtetea Lulu likiongozwa na Kennedy Fungamtama Juni 13 waliwasilisha mahakamani hati za viapo vya wazazi wake na vielelezo vingine kikiwemo cheti cha kuzaliwa na cha ubatizo vinavyoonesha kuwa bado ni mtoto.

 Lakini taarifa zilizopatikana mahakamani hapo zinaeleza kuwa vielelezo vilivyowasilishwa na Jamhuri vinaonesha kuwa mshtakiwa huyo ni mtu mzima kwa kuwa kwa mujibu wa vielezo hivyo ana umri zaidi ya miaka 18.

 Viapo vya wazazi wa mshtakiwa huyo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Peter Kibatala ambaye ni mmoja wa mawakili wanaomtetea Lulu vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo ana umri wa miaka 17.

 Viapo hivyo ambavyo Gazeti hili limefanikiwa kuviona ni kiapo cha mama yake Lulu Lucresia Augustin Kalugila, mkazi wa Dar eS Salaam na kiapo cha baba mzazi Michael Kimemeta, mkazi wa Moshi.

 Viapo vyote vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo alizaliwa April 16, 1995 katika kituo cha Afya Muhimbili na kupewa cheti cha kuzaliwa namba B.0318479 cha Julai 23, 2004.

 Pia viapo hivyo vinaeleza kuwa baada ya kuzaliwa mshtakiwa, mama yake alimpa jina la Diana Michael Kimemeta, lakini alimpeleka mtoto huyo Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ndugu zake, walimpa jina la Elizabeth, jina la bibi yake Elizabeth Shikana

Okwi asaini Orlando Pirates kwa Sh 190m

                                                          Emmanuel Okwi.

 KLABU ya Orlando Pirates ipo kwenye hatua za mwisho kumsajili kiungo mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, raia wa Uganda.
 Okwi anatarajiwa kwenda nchini Afrika Kusini wiki ijayo ili kukamilisha mchakato wa usajili wake ambao utaigharimu Orlando Pirates kiasi cha randi milioni 7 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 190.
 Mganda huyo ambaye alichangia kuipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita, aliwahi kufanya majaribio klabuni hapo msimu uliopita na alikuwa ameitwa tena kwa ajili ya kukamilisha zoezi hilo kwa mara ya pili.
 Gazeti moja la michezo la Afrika Kusini limemnukuu Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga: “Kila kitu kimekamilika lakini kuna vitu vichache ambavyo tunatakiwa kukamilisha kabla hatujamruhusu rasmi Okwi.
 “Okwi alikuwa msaada mkubwa kwenye klabu yetu kutwaa ubingwa wa ligi kuu (Bara) msimu uliopita, ulikuwa ni uamuzi mgumu kumruhusu aondoke, lakini tuna furaha na tunamtakia neema huko aendako.”

UNAIJUA NGOZI YAKO NI AINA GANI NA UITUNZAJE?!!

Ni vizuri sana kwako kuweza kujua aina ya ngozi yako maana itasidia wewe uweze kuitunza ngozi yako vizuri.Vile vile itakusaidi katika kujua ni vipozi vya aina gani utumie kutokana na ngozi yako. Hakuna ngozi mbili ambazo zinafanana exactly ila zinatofautiana ambapo inawezekana ngozi yako ikawa ni Ngozi Kavu, Ngozi ya Kawaida, Ngozi ya mafuta na ngozi mchanganyiko yaani combine skin.
ZAIDI INGIA BONGO UREMBO UKAREMBEKE

Mrisho Ngassa atua Jangwani


                                                 Mrisho Ngassa.
KIUNGO wa Azam FC, Mrisho Ngassa, jana Alhamisi alitua makao makuu ya klabu ya Yanga yaliyopo Jangwani jijini Dar es Salaam na kupokewa kwa shangwe kubwa.
Ngassa ana uwezekano mkubwa wa kuwemo kwenye kikosi cha Yanga kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza Julai 14, mwaka huu.
Ngassa aliwasili Jangwani saa 5:07 asubuhi akiwa ndani ya gari lake aina ya Toyota Corona lenye namba za usajili T 508 AUB, ikiwa ni muda mfupi baada ya mazoezi ya timu hiyo kumalizika kwenye Uwanja wa Kaunda, kisha kwenda kuegesha gari lake sehemu maalum inayotumiwa na viongozi na wachezaji wa Yanga pindi wanapowasili klabuni hapo.
Wakati umati wa mashabiki uliokuwa ukishuhudia mazoezi ukijiandaa kuondoka, ghafla ulimuona Ngassa na ndipo ukalizunguka gari lake na kuanza kumshangilia. Kuona hivyo Ngassa alisita kwa muda kutoka kisha kufungua mlango wa gari na kutoka.
Mashabiki hao walimvamia na kumbeba juujuu kwa furaha huku wakiimba kwa kulitaja jina lake ‘Ngassa! Ngassa! Ngassa! Ngassa!’ Lakini baadaye aliwataka wamshushe, mashabiki hao walitii amri hiyo.
Baada ya hapo, alianza kuelekea ndani ya jengo huku akisalimiana na wachezaji wa Yanga waliokuwepo eneo hilo, muda mfupi baadaye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Seif Ahmeid ‘Seif Magari’ alitokea ndani ya jengo hilo na kuingia naye kwenye chumba namba saba.
Baadaye, Ngassa alipandisha ghorofani na kuingia kwenye chumba namba saba ambapo alikuwemo mshambuliaji wa timu hiyo, Jerry Tegete. Mpaka gazeti hili lilipoondoka klabuni hapo 5:45 asubuhi, Ngassa alikuwa hajatoka chumbani humo.
Alipoulizwa kuhusiana na ujio wake Jangwani, Ngassa alisema: “Nimekuja kuonana na Jerry, tulipanga tukutane hapa kwa ajili ya kufanya mazungumzo yetu binafsi, siyo ya mpira.”
Aidha, habari za ndani kutoka kwa mmoja wa viongozi wa klabu hiyo, zimethibitisha kuwa kweli Jangwani wamefanya mazungumzo na Azam, kilichobakia ni makubaliano ya mwisho kabla ya kumtambulisha rasmi Ngassa kuwa mchezaji wa Yanga.
Mpigapicha wa gazeti hili, Richard Bukos, alimpiga picha mchezaji huyo wakati akiwasili klabuni hapo lakini Ngassa na baadhi ya mashabiki walimuomba kufuta picha hizo sababu mambo hayajakamilika na kudai zinaweza kumsababishia matatizo ya uhamisho wake.

Ureno yatua nusu fainali Euro 2012

CRISTIANO Ronaldo jana aliendelea kung’aa baada ya kufanikiwa kuiongoza nchi yake kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano ya Euro 2012 kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Czech.
Ronaldo alifunga bao pekee kwenye mchezo huo baada ya kuiwahi krosi safi iliyopigwa na winga wa Manchester United, Luis Nani katika dakika ya 79.
Katika mchezo huo Czech walionekana kuzidiwa katika dakika zote na walifanikiwa kufika langoni mwa Ureno mara moja tu kipindi cha kwanza.
Ronaldo sasa amefikisha mabao matatu kwenye michuano hiyo baada ya kufanikiwa kufunga mawili kwenye mchezo wa makundi dhidi ya Uholanzi.
Katika historia ya Ureno haijawahi kutwaa ubingwa huu zaidi ya kufika hatua ya nusu fainali mara mbili mwaka 1984 na 2000.
Kutokana na ushindi huo, Ureno inasubiri kukutana na mshindi wa mechi kati ya Ufaransa dhidi ya Hispania katika nusu fainali ya kwanza mnamo Juni 27, 2012.