Friday, November 9, 2012

Dk Mwinyi Atembelea Vituo Vya Uchunguzi Na Matibabu Vinavyojengwa Mkoani Dodoma

 Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi akiwasili katika eneo la Ujenzi wa kituo cha kisasa cha Matibabu mkoani Dodoma.
 Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi (kulia) akizungumza kabla ya kukagua ujenzi wa Kituo cha Kisasa cha uchunguzi na Matibabu katika Chuo Kikuu cha Dodoma kinachonjengwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
 Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi (kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Dk. Emmanuel Humba baada ya kukagua ujenzi wa Kituo cha Mfano cha Uchunguzi na Matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kinachojengwa na Mfuko huo.

TAARIFA KWA UMMAUzinduzi Wa Shindano La Kusaka Mabingwa Wa Kero Kwa Wateja

                             Uzinduzi wa Shindano la Kusaka Mabingwa wa Kero kwa Wateja

Jumuiya ya watumiaji wa huduma mbalimbali nchini kupitia mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter imezindua rasmi shindano la kusaka kampuni zinazotoa huduma na bidhaa mbovu kwa wateja nchini Tanzania.

Jumuiya hiyo inawajumuisha watu wa kada mbalimbali wakiwemo wanasheria, wanaharakati, waandishi wa habari, viongozi wa kisiasa, wafanyabiashara na wateja wa huduma na bidhaa mbalimbali nchini Tanzania.

Lengo la jumuiya hiyo ni kushinikiza wafanyabiashara nchini kutoa huduma na bidhaa bora kwa wateja na kuwakumbusha umuhimu wa wateja. Kauli mbiu ya wanajumuiya hao ni Mteja ni Mfalme.

Katika wiki ya kwanza tangu jumuiya hiyo kuzinduliwa jumla ya makampuni 21 yameingizwa katika shindano hilo kwa wateja wao kuwasilisha malalamiko yao. Kwa taarifa zaidi kuhusu ni fuatilia akaunti ya Twitter @hudumambayatz au kundi la Facebook linalojulikana kama HUDUMA BONGO.

Ili kuweza kupiga kura yako unahitajika kuwa na akaunti hai (yenye mawasiliano mara kwa mara) katika mtandao wa Twitter au Facebook na kujiunga na jumuiya hiyo. Mara tu utakapowasilisha kero yako utaifanya kampuni unayoilalamikia kuingia katika mchuano mkali wa kumsaka bingwa wa huduma mbovu kwa wateja nchini.

Huduma Bongo inatoa wito kwa makampuni yote kuboresha huduma na bidhaa zao ili kuweza kuwapatia wateja kilicho bora zaidi katika soko hili la ushindani.

Imetolewa na Mshauri wa Habari wa Huduma Bongo - hudumabongo@gmail.com
Novemba 9, 2012

Akamatwa Na Sehemu Za Siri Za Mpwa Wake A. Kusini

Mwanamume mmoja nchini Afrika Kusini amekamatwa baada ya kupatikana akiwa na sehemu za siri kwenye pochi lake ambazo zinaaminika kuwa za mpwa wake ambaye hajulikani aliko.

 Msemaji wa polisi, aliambia BBC kuwa babada ya kukamatwa kwake , mwanaume huyo aliwapeleka maafisa wa polisi kwenye msitu katika mkoa wa Eastern Cape, ambako mwili uliokatwakatwa ulipatikana.

 Kichwa cha msichana huyo pamoja na miguu yake ilikuwa imekatwa na zilipatikana karibu na kiwiliwili chake. Mtu huyo mwenye umri wa miaka 42, anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa kosa la mauaji.

 Mmwanaume huyo alishtakiwa baada ya kushukiwa kuhusika na kutoweka kwa msichana huyo mwenye umri wa miaka 18, aliyepotoea katika mji wa Ngcobo siku ya Jumapili.

 Msemaji wa polisi, Mzukisi Fatyela alisema kuwa sehemu hizo za siri, zilipatikana ndani ya pochi lake. Alisema sababu ya kuuawa kwa msichana huyo haijulikani na kwamba uchunguzi unafanyika.

 Alipoulizwa ikiwa mauaji hayo yanahusishwa na waganga ambapo sehemu za mwili wa watu hutumiwa kwenye madawa yao, bwana Fatyela alisema kuwa hawezi kubaini hilo kwa sasa. Kumekuwa na visa vingi vya kuuza sehemu za siri za watu katika sehemu nyingi za Afrika kwa sababu sawa na hizo.

 Afrika Mashariki imeshuhudia visa vingi vya kuuawa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi au maalbino, huku sehemu za miili yao zikikatwa kwa sababu za kishirikina. Mwanaume huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.

 BBC-SWAHILI

Uongozi Wa Sauti Za Busara Wakana Kumdhulumu Bi Kidude

Mkurugenzi wa Sauti za Busara ZanzibarYussuf Mahmoud amesema kutokana na malalamiko yanayotolewa na familia ya Bi Fatma Baraka Khamisi (Bi Kidude) wameamua kuzikabidhi fedha za msanii huyo mkongwe alizokuwa akizihifadhi ili kuepusha migogoro zaidi.

Ameyasema hayo  katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo huko  Kikwajuni wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kufuatia malamiko ya baadhi ya wanafamilia wa Bi Kidude  wanaodai kwamba mzazi wao anaibiwa fedha zake na viongozi wa Sauti za Busara.

Mkurugenzi huyo amesema lengo la Sauti za Busara ni kuwasaidia wasanii wa Zanzibar na Afrika kwa jumla katika kuwatangaza na kuwatafutia maslahi ndani na nje ya nchi na sio kuwadhulumu kipato chao.

Amesema baada ya juhudi kubwa walizofanya kuanzia mwaka 2005 walipoanza kumsaidia Bi Kidude ikiwa ni pamoja na kumuwezesha kupata tunzo ya Womex, wamefanikiwa kukusanya shilingi milioni 36 zilizotokana na maonyesho mbali mbali yaliyosimamiwa na Sauti za busara, mauzo ya CD na mahojiano aliyofanya na vyombo vya Habari.

Ameongeza kuwa fedha hizo amekuwa akizutumia mwenyewe, kusimamia kuitengeneza nyumba yake na wamekuwa wakizitumia kwa matibabu yake anapoumwa na hivi sasa fedha zilizobakia  ni shilling Millioni tatu  laki sita na elfu nne (3,604,000) ambazo zimo mikononi mwake na  hivyo alitaka fedha hizo azikabidhi kwa mtu wa familia ambae Bi Kidude ataridhia mwenyewe.

Hata hivyo shughuli ya kukabidhi fedha hizo kwa wanafamilia ilishindikana kutokana na wanafamilia kukataa kuhudhuria katika kikao hicho cha leo.

Mkuu wa miradi wa Sauti za Busara Janny Ramadhani amedai kuwa chanzo cha mzozo ni pale Bi Kidude alipomtambulisha mwanafamilia Baraka Abdalla kuwa ndie atakuwa dhamana wa kumchukulia fedha za kila wiki shilingi 50,000 ambazo walikubaliana lakini baadhi ya wiki kijana huyo alikuwa hazipeleki kwa Bi Kidude.

Amesema familia ya Bi Kidude imechangia kwa kiasi kikubwa katika kumuangusha mzazi wao licha ya juhudi walizokuwa wakizichukua katika kumtangaza na kumpatia safari za mara kwa mara nje na ndani ya nchi.

Viongozi hao wa Sauti za Busra wamewataka wasanii wote nchini wawe pamoja na kujenga  moyo wa  kushirikiana na kusaidiana ili  waweze kukuza vipaji vyao na kuinua sanaa zao na kufikia maendeleo waliyokusudia.

Na: Ramadhan Ali na Mwanaisha Mohamed-Maelezo Zanzibar 09/11/2012

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR 9/11/2011

Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari...!

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania limeteua wadau 10 kwa ajili ya kusaidia timu ya taifa ya vijana walio na umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys itakayopambana na Congo (Brazaville) katika mechi ya raundi ya tatu ya michuano ya awali ya Mataifa ya Afrika.

Uteuzi huo umefanywa na Rais wa TFF, Leodegar Tenga baada ya Kamati ya Vijana ya TFF kufanya kikao chake kujadili kwa umakini ushiriki wa timu hiyo na kupeleka mapendekezo yake kwa rais huyo wa shirikisho.

Kutokana na umuhimu wa mechi hiyo itakayoamua timu itakayofuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, TFF imeona umuhimu wa kuwa na kamati ambayo itakuwa na majukumu mawili makubwa ambayo ni:

1.       Kuhamasisha vijana waone umuhimu na kuwa na ari ya kushinda mechi hiyo
2.       Kuhamasisha umma uone umuhimu wa mechi hiyo na hivyo kuisaidia iweze kufuzu.
Walioteuliwa kuunda kamati hiyo ni:
1.       Ridhiwani Kikwete                                           Mwenyekiti
2.       Ahmed Seif (Magari)                                      Mjumbe
3.       Nassoro Bin Slum                                             Mjumbe
4.       Henry Tandau                                                    Katibu
5.       Ahmed Mgoyi                                                   Mjumbe
6.       Aboubakar Bakhresa                                      Mjumbe
7.       Angetile Osiah                                                   Mjumbe
8.       Kassim Dewji                                                     Mjumbe
9.       Abdallah Bin Kleb                                             Mjumbe
10.   Salim Said                                                            Mjumbe
Baada ya kuvuka raundi mbili za kwanza bila ya kucheza mechi kutokana na wapinzani wake kujitoa, timu ya Serengeti Boys inahitaji kufanya kila iwezalo kuweza kuiondoa Congo kwenye mashindano hayo na kuweka rekodi ya kufuzu kucheza fainali hizo za Afrika ambazo pia zitatoa wawakilishi wa Afrika kwenye mashindano ya Kombe la Dunia.

Mechi za kwanza za raundi ya tatu zitachezwa kati ya Novemba 16 na 18, 2012 na mechi za marudiano zitachezwa kuanzia Novemba 30, 2012 hadi Desemba 2, 2012

*Kuhusu suala la Azam FC kuwasimamisha wachezaji watatu kwa tuhuma za kuhusika kuhujumu timu, tayari TFF imepokea barua hiyo ya Novemba 8, 2012 na inalishughulikia na kulifuatilia kwa makini.

*TFF inapenda kukipongeza Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Mwanza kwa kufanya uchaguzi wake kwa amani na kufanikiwa kupata viongozi wapya watakaokuwa chini ya uenyekiti wa Jackson Songora.

Rais wa TFF amewapongeza viongozi waliorekjea madarakani na viongozi wapya akieleza magtumaini yake kuwa kamati mpya ya Utendaji ya MRFA itaelekeza nguvu zake katika kuendeleza mikakati iliyokuwepo ya kuinua kiwango cha mpira wa miguu na kubuni mikakati mingine kwenye mkoa huo na Tanzania kwa ujumla ikishirikiana na TFF.
*Ligi Kuu ya Vodacom inatazamiwa kuendelea kesho kwenye viwanja tofauti

1. Simba                               v Toto Africans                                  Uwanja wa Taifa
2. T. Prisons                        v JKT Ruvu                                           Sokoine
3. Kagera Sugar                 v Polisi Moro                                      Kaitaba
4. African Lyon                  v Mtibwa Sugar                                 Azam Complex
5. Oljoro JKT                       v Ruvu Shooting                               Sheikh Amri Abeid
6. Mgambo JKT                 v Azam FC                                           Mkwakwani
Jumapili
1.       Coastal Union    v Young Africans                               Mkwakwani

Magazeti ya leo Ijumaa ya 9th November 2012