Tuesday, October 9, 2012

JK Arejea Nchini Leo

  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, akiongea na Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya kurejea nchini leo Jumanne Oktoba 10, 2012 akitokea katika ziara ya Kikazi ya Marekani na Ziara Rasmi ya Kiserikali ya Canada
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, akilakiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya kurejea nchini leo Jumanne Oktoba 10, 2012 akitokea katika ziara ya Kikazi ya Marekani na Ziara Rasmi ya Kiserikali ya Canada.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, akiongea na Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda, Waziri wa Sheria na Katiba Mhe Celina Kombani, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mhe Steven Wassira, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Adama Malima na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Said Meck Sadiki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya kurejea nchini leo Jumanne Oktoba 10, 2012 akitokea katika ziara ya Kikazi ya Marekani na Ziara Rasmi ya Kiserikali ya Canada.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, akipokewa  na Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya kurejea nchini leo Jumanne Oktoba 10, 2012 akitokea katika ziara ya Kikazi ya Marekani na Ziara Rasmi ya Kiserikali ya Canada.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, akilakiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Said Meck Sadiki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baada ya kurejea nchini leo Jumanne Oktoba 10, 2012 akitokea katika ziara ya Kikazi ya Marekani na Ziara Rasmi ya Kiserikali ya Canada.

PICHA NA IKULU

MWANAFUNZI AFANYA MTIHANI WA TAIFA WA KIDATO CHA 4 AKIWA WODINI MOROGORO


Mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya Sekondari ya Alfa Germ, Morogoro, Jesca Kiliani (17) akifanya mtihani wa taifa akiwa wodi namba 7B  katika hospitali ya rufaa ya mkoa huo jana, baada ya kulazwa kufuatia kufanyiwa operesheni ya uvimbe.

MWANAFUNZI wa kidato cha nne katika Sekondari ya Alfa Germ, Morogoro, Jessica Kiliani (17), amelazimika kufanya mtihani wake wa kuhitimu elimu  hiyo akiwa wodini baada ya kufanyiwa upasuaji.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya mwanafunzi huyo, kuomba aruhusiwe kufanya mtihani huo licha ya kuwa  wodini akiugulia maumivu ya upasuaji aliofanyiwa na madaktari wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa zaidi ya saa mbili na kulazwa katika wodi ya wazazi namba 7B.

Picha na KALULUNGA BLOG

Washiriki Redds Miss Tanzania 2012 wakaribishwa Monduli kwa shangwe

Dada wa Mbunge wa jimbo la Monduli na Waziri Mkuu mstaafu Kalaine Lowasa akiwavisha warembo wanaoshiriki shindano la Redds Miss Tanzania 2011, mgolole wa kimasai wakati warembo hao walipoandaliwa tafrija maalum ya kuwakaribisha katika mji wa Monduli.Kushoto ni Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge w Monduli, Regina Lowasa.Warembo hao wapo Kanda ya Kaskazini kutembelea vivutio mbalimbali vya Utalii vilivyopo katika mikoa hiyo






Dada wa Mbunge wa jimbo la Monduli na Waziri Mkuu mstaafu Kalaine Lowasa akiwavisha warembo wanaoshiriki shindano la Redds Miss Tanzania 2011, mgolole wa kimasai wakati warembo hao walipoandaliwa tafrija maalum ya kuwakaribisha katika mji wa Monduli.Kushoto ni Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge w Monduli, Regina Lowasa.Warembo hao wapo Kanda ya Kaskazini kutembelea vivutio mbalimbali vya Utalii vilivyopo katika mikoa hiyo
 Robert Lowasa nae alivishwa Mgolole kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa kufanikisha warembo hao kufika Monduli
                                                Warembo wakiwa wamekaa na mavazi yao yakimasaai
                                              Baadhi ya wadau waliohudhuria tafrija hiyo
                                                     Viongozi wa kamati ya Miss Tanzania
                                                                        Picha ya pamoja
 Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu,Regina Lowasa akicheza mziki wa Kwaito na Warembo wanaoshiriki shindano la Redds  Miss Tanzania 2012, wakati wa tafrija maalum ya kuwakaribisha warembo hao katika mji wa Monduli jana mkoani Arusha.
Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu, Regina Lowasa na mtoto wake Robert Lowasa 'Bob" wakicheza mziki wa Kwaito na Warembo wanaoshiriki shindano la Redds  Miss Tanzania 2012, wakati wa tafrija maalum ya kuwakaribisha warembo hao katika mji wa Monduli jana mkoani Arusha.

Warembo wa Redds  Miss Tanzania wapo Kanda ya Kaskazini kutembelea vivutio mbalimbali vya Utalii vilivyopo katika mikoa hiyo.

Magazeti ya leo Jumanne 9th October 2012

                         
 

Uwekezaji wa Barrick Waleta Manufaa Makubwa Kwa Taifa - Serikali

SERIKALI imeipongeza kampuni ya African Barrick Gold (ABG) kwa kuleta manufaa makubwa kwa taifa kutokana na uwekezaji unaoendelea kufanywa na migodi yake nchini katika nyanja mbalimbali ikiwemo uchumi wa nchi na maendeleo ya jamii. Kampuni ya ABG inamiliki migodi minne ya dhahabu nchini -- Bulyanhulu, North Mara, Buzwagi na Tulawaka -- na ndiyo kampuni kubwa kuliko zote kwenye sekta ya madini. “Nimejifunza mambo mengi sana baada ya kutembelea mgodi wa North Mara,” alisema Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, siku ya Ijumaa baada ya kufanya ziara ya mgodi huo wa ABG ulioko wilaya ya Tarime, mkoa wa Mara.

Katika ziara hiyo, Masele pamoja na Naibu Waziri wa Nchi kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Charles Kitwanga, walitembelea miradi mikubwa ya jamii ambayo inatekelezwa na mgodi huo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo elimu, maji na afya. Masele alisema kuwa mgodi wa North Mara kihistoria umekuwa na matatizo ya mahusiano na jamii inayoizunguka, lakini hatua kubwa zimepigwa sasa kuboresha mahusiano na vijiji vinavyozunguka mgodi huo.

“Mimi binafsi Bungeni nimeskia pale wabunge wa huku wakilalamika kwamba kuna shule za msingi ziko jirani sana na mgodi. Kazi za mgodi zinapoendelea, ile milipuko inakuwa ikiwaathiri
wanafunzi,” alisema. “Lakini leo nimetembelea shule ambayo inatakiwa kujengwa ili kuhamisha ile ambayo inaathiriwa na shughuli za mgodi.

Nimejionea kazi ambayo inaendelea pale. Wakandarasi wako saiti wanajenga hizo shule.” Masele alisema kuwa kipindi cha nyuma kulikuwa na tatizo la wanafunzi kukaa chini katika shule zilizopo katika maeneo hayo ya mgodi, lakini mgodi wa North Mara sasa unatekeleza mradi kabambe wa kuzipatia shule hizo madawati.

“Nimejionea kwamba mgodi umeweza kutekeleza ahadi ya kuweka madawati katika shule zote ambazo zinazunguka mgodi na wanafunzi wamekaa kwenye madawati,” alisema. Hivi karibuni, mgodi wa North Mara ulitoa msaada wa zaidi ya madawati 1,000 kwa shule za msingi za Wilaya ya Tarime ambazo zinazunguka mgodi huo.

MIRADI YA MAJI
 Waziri Masele pia ameipongeza ABG kwa jitihada zake za kutoa msaada kwa wananchi kuhakikisha kuwa wanapata huduma ya maji safi na salama ya kunywa. “Palikuwa na wasiwasi mkubwa wa maji … wananchi walikuwa wakilalamika wanachota maji mbali. Leo nimeshuhudia tukizindua kisima cha maji ambacho ni moja ya mwendelezo wa visima vya maji vingine na miradi ya maji mingine ambayo mgodi inaendelea kutekeleza kwa wananchi,” alisema. “Akina mama ambao walikuwa wakiamka saa saba au saa nane usiku kwenda kutafuta maji sasa wanaweza kuamka saa mbili au saa moja asubuhi. Nimeona bowsers (malori ya maji), maji wanaletewa mlangoni kitu ambacho maeneo mengi tungependa kuletewa maji mlangoni lakini eneo hili la Nyamongo sasa wananchi wanapelekewa maji mlangoni (na mgodi wa Barrick).”

SEKTA YA AFYA
Mawaziri hao pia walitembelea hospitali ya Sungusungu ambayo mgodi wa North Mara ulikabidhi kwa serikali baada ya kutumia zaidi ya dola za Marekani 330,000 (zaidi ya shilingi milioni 500) kufanya ukarabati mkubwa katika hospitali hiyo. “Vijana wengi hapa wanajishughulisha na shughuli za uchimbaji madini na wanapata ajali nyingi. Tumeshuhudia pale vijana wanapata ajali lakini wanatibiwa katika hospitali ambayo imejengwa na mgodi ambayo zamani ilikuwa ni hospitali ndogo sana,” alisema. Masele alitaka migodi mingine nchini iige mfano wa mgodi wa North Mara wa ABG kwenye kuboresha mahusiano na jamii na kuwekeza kwenye miradi mikubwa ya maendeleo ya jamii. “Tumeona shughuli zile za kijamii kama community development projects zinafanyika kwa ufanisi na kwa kasi kubwa. Hili binafsi mimi limenifariji kwa sababu yale ambayo tumeyaahidi kwa wananchi kwamba tutahakikisha tunaisimamia migodi hii ilete manufaa kwenye jamii zote ambazo zinazoizunguka,” alisema.

KODI ZA MADINI
 Masele aliipongeza ABG kwa kutoa mchango mkubwa kwa pato la taifa kupitia kwenye kodi mbalimbali ambazo migodi yake inalipa serikalini. “Kwa upande wa shughuli za kodi, tunaendelea na mazungumzo na tunaishukuru Barrick kwa ujumla na migodi yao yote siyo tu North Mara, hata mingine yote kwa ujumla wameweza kuhama kutoka kwenye kulipa mrabaha wa asilimia 3 na sasa wanalipa asilimia 4 ya mapato yote,” alisema. “Hii ni hatua kubwa ambayo wameifanya ambayo iko nje ya mikataba yao ambayo waliifunga huko nyuma. Sasa unaweza kuona kuwa wametoa ushirikiano mkubwa kwa serikali kuweza kukubali kulipa asilimia 4 ya mrabaha, jambo ambalo limeongeza mapato katika makusanyo ya serikali.”

TAARIFA YA KUUZWA KWA ABG

 Masele alikanusha tetesi kuwa tayari kampuni ya ABG imekwishauzwa kwa kampuni ya taifa ya dhahabu ya China na kusisitiza kuwa serikali inafuatilia kwa karibu mazungumzo kati ya kampuni hizo. “Kuna taarifa nyingi zimesikika kwenye vyombo mbalimbali vya habari kwamba mgodi utanunuliwa na wengine wameshasema kuwa umeshauzwa. Naomba niseme tu kuwa mgodi bado haujauzwa lakini mazungumzo ya kuuzwa mgodi na kununuliwa na kampuni ya taifa ya China yanaendelea kati yao,” alisema. “Sisi kama serikali la kwetu ni moja tu, maslahi yetu kama nchi kwenye kodi na maslahi mengine yote. Zipo kodi nyingi sana ambazo serikali inazipata kutoka kwenye mgodi.”

 UWEKEZAJI WA ABG
Makamu wa Rais wa ABG wa shughuli za shirika, Deo Mwanyika, alisema kuwa mgodi wa North Mara umeingia mkataba na vijiji vyote vinavyouzunguka wa kuwekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 8.5 (zaidi ya shilingi bilioni 13) kwenye miradi mbalimbali ya jamii ikiwemo kwenye sekta za elimu, afya na maji. Mwanyika alisema kuwa mgodi wa North Mara unakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo tatizo la uvamizi wa mara kwa mara unaofanywa na baadhi ya wananchi kwenye eneo la mgodi huo. “Changamoto kubwa sana ya mgodi huu pamoja na uzalishaji ni mahusiano na jamii. Kulikuwa na malamiko makubwa sana kuhusu kutotekeleza mikataba ambao mgodi ulikuwa umeingia huko siku za nyuma. Sisi tumetoa ahadi kuwa tutatekeleza hiyo mikataba yote na tumeanza,” alisema. “Changamoto zipo, bado tuna tatizo kubwa la uvamizi lakini kwa kiasi kikubwa tunafanya kazi na serikali na ujio wa hawa mawaziri wawili mojawapo ni kuangalia kwa kiasi gani tunaweza kukaa kwa pamoja tukapunguza haya mambo ya uvamizi bila kuleta madhara kwa wananchi.”

MWANDISHI WETU Tarime

Ripoti Za Kifo Cha Mwangosi Kuwekwa Hadharani Leo

SERIKALI leo inatoa hadharani ripoti ya Kamati iliyoundwa kupata taarifa kuhusu vurugu zilizotokea mkoani Iringa na kusababisha kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi. Wakati ripoti hiyo ikitarajiwa kutolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Kamati nyingine iliyoundwa na Baraza la Habari (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), nayo leo inatarajiwa kuweka hadharani ripoti yake.

 Kamati hizo ziliundwa kwa nyakati tofauti baada ya vurugu zilizotokea Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi wakati polisi walipowatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakifungua tawi la chama hicho katika kijiji hicho.

 Juzi, Makamu Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Dk Nchimbi, Theophil Makunga alimkabidhi waziri huyo na kusema Kamati yake ilifanya ziara Iringa na pia mahojiano na wadau mbalimbali Dar es Salaam.Kamati ya Nchimbi ilikuwa ikiongozwa na Mwenyekiti Jaji Steven Ihema, Makunga na Ofisa wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike, Kanali Wema Wapo wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) pamoja na Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi, Isaya Mngullu.

Tofauti na taarifa nyingine, ripoti ya mauaji ya Mwangosi inatarajiwa kutolewa hadharani ili umma uweze kuisoma, kuichambua na kutoa maoni kuhusu hatua za kuchukua ili matukio ya aina hiyo yasitokee tena. Ripoti ya MCT Katibu Mkuu wa Tef, Neville Meena alisema timu ya uchunguzi imeshamaliza kazi yake na leo itatoa rasmi ripoti kuhusiana na mazingira ya kifo cha Mwangosi.

Kamati hiyo iliundwa na watu watatu, John Mirenyi kutoka MCT, Hawra Shamte kutoka Tef na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Saimon Berege. “Sisi tukiwa wanahabari tuliunda Kamati yetu ili ifanye uchunguzi kuhusiana na mauaji ya mwanahabari mwenzetu, baada ya kukamilisha uchunguzi huo, sasa tupo tayari kuiwasilisha ripoti yetu hadharani,” alisema Meena.

Chanzo:  http://www.mwananchi.co.tz

Dkt.Bilal Aiwakilisha Nchi Mkutano Wa Maziwa Makuu

MHESHIMIWA MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MKUTANO MAALUM WA WAKUU WA NCHI ZA MAZIWA MAKUU, KAMPALA UGANDA

Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amemuwakilisha Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika mkutano maalum wa wakuu wa nchi za Maziwa Makuu mjini Kampala Uganda. Oktoba 08, 2012.

Mkutano huu maalum una agenda moja kubwa ambayo ni kujadili na kisha kupitisha maamuzi kuhusu mustakhbali wa hali ya usalama wa kudumu katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo.

 Mheshimiwa Makamu wa Rais na ujumbe wake umewasili nchini hapa salama na moja kwa moja kushiriki kupata taarifa za mikutano ya ngazi ya Mawaziri ambapo Tanzania iliwakilishwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Omari Juma Mahadhi.

 Katika mazungumzo hayo ya awali, Mheshimiwa Waziri Vuai alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, Tanzania inabakia kuwa na sifa yake ya siku zote ya kuthamini na kujitoa kusaidia kupatikana kwa amani katika nchi zinazoizunguka sambamba na zile zinazohitaji msaada wake.

 Akifafanua kuhusu makubaliano katika ngazi ya Mawaziri, Waziri Vuai alimhakikishia Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa Tanzania imewakilishwa vizuri na kwamba nchi nyingine wanachama zinategemea sana mchango wa Tanzania katika kuisaidia Congo (DRC) kufikia amani ya kudumu na hivyo wananchi wake kuendelea na shughuli za kunyanyua vipato vyao bila hofu ya usalama wa maisha yao.

 Kwa upande wake, Mheshimiwa Naibu Waziri Mahadhi alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuhusu ushiriki wa Tanzania katika nchi za Maziwa Makuu na akafafanua kuwa nchi hizi zinategemeana sana katika hali mbalimbali za maisha hivyo Tanzania bado inayo fursa nzuri ya kuendeleza mahusiano na nchi hizi kwa angalizo kubwa la kutazama fursa za kiuchumi.

Katika mkutano wa leo wa wakuu wa nchi uliofanyika katika eneo la Munyonyo nje kidogo ya jiji la Kampala, Wakuu na Wawakilishi wa wa nchi mbalimbali, walikutana majira ya saa tano na kisha mwenyeji wa Mkutano huo, Rais Yoweri Kaguta Museveni kuufungua.

Rais Museveni alitumia nafasi hiyo, kuwashukuru viongozi wote akianza na Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye alimpongeza kutokana na ushiriki wake katika mazungumzo ya kufanikisha amani Congo (DRC) na kisha akamshukuru Rais Joseph Kabila wa Congo (DRC) kwa kukubali kuzieleza nchi wanachama wa nchi za Maziwa Makuu kuhusu hali mbaya ya kiusalama nchini kwake na kukubali kutaka msaada kutoka kwa nchi hizi.

 Mjadala mkubwa katika mkutano huu ulikuwa kuhusu kuundwa kwa jeshi lisilofungamana na upande wowote ili lisaidie kumaliza mapigano katika Congo (DRC) na kisha kuiwekea nchi hiyo misingi ya kuwa na amani ya kudumu.

Mkutano huu pia ulihudhuriwa na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir ambaye alikuja na hoja ya kutaka nchi yake iharakishiwe nafasi ya uanachama katika umoja huu, jambo ambalo baadhi ya nchi limeona ni bora, lakini zikatoa angalizo kuwa lazima nchi hiyo licha ya kuwa na nia na sifa ya kuwa mwanachama, ifuate utaratibu wa kawaida wa kutafuta nafasi ya uanachama na sio kuruka taratibu.

Mkutano huu unafanyika nchini Uganda wakati nchi hii ikijitayarisha kuadhimisha sherehe za miaka 50 ya uhuru wake, huku hali vya usalama nchini hapa vikionesha kila sababu ya kulinda amani katika tukio hili nyeti katika historia ya Uganda na Afrika Mashariki.
 IMETOLEWA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS ,