MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imewaachia huru wanafunzi 51 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kufanya mkusanyiko usio halali na kukaidi amri halali ya askari wa Jeshi la Polisi iliyowataka watawanyike.
Akiwaachia huru wanafunzi hao jana, Hakimu Mkazi Waliarwande Lema alisema anawaachia huru washtakiwa hao, kwa mujibu wa kifungu cha 225 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), sura ya 20 kwa sababu upande wa mashtaka ulishindwa kuliendesha shtaka hilo.
Wanafunzi hao waliachiwa huru baada ya Wakili wa Serikali, Prosper Mwangamila kudai kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa na kubainisha kuwa mahakama ilikwisha toa ahirisho la mwisho Agosti 13, mwaka huu.
Mwangamila alidai kuwa waliwasiliana na mashahidi wao ambao ni askari kupitia kwa RCO wa Wilaya ya Kinondoni ,lakini aliwaambiwa kuwa askari hao ni moja kati ya askari waliopo kwenye Sensa ambayo ni muhimu kama kesi hiyo.
Hivyo Wakili huyo wa Serikali aliiomba mahakama itoe ahirisho lingine la mwisho hadi Jumatatu kwa sababu askari hao bado wapo kwenye Sensa ambayo inaisha Jumapili.
Baada ya kutolewa kwa hoja hizo, Wakili wa Utetezi, Regnal Martin alipinga ombi la kuahirishwa kwa kesi hiyo na kuutaka upande wa mashtaka kuheshimu amri ya mahakama.
Wakili Martin alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo imekuwa ikiahirishwa kwa sababu tofauti ikiwemo ya askari hao kuwepo kwenye mgomo wa madaktari wa Julai 12, mwaka huu.
Akitoa uamuzi juu ya hoja hizo, Hakimu Lema alisema baada ya kupitia mwenendo mzima wa kesi , mahakama inajiuliza swali kuwa mashahidi pekee ni hao hao maaskari na kama ni hao upande wa mashtaka ulipaswa kuwasilisha hati chini ya kifungu cha sheria cha 225 (4) cha CPA ambacho kinaeleza tarabu kama shahidi hayupo nini kifuatwe.
Hakimu Lema alisema sababu zilizotolewa na upande wa mashtaka ni za msingi lakini hazikubaliki na kwamba walichokifanya wameidharau mahakama kwa kutofuata taratibu zilizopo.
Aliongeza kuw ana wasiwasi hata kutoa ahirisho lingine la mwisho kwa upande wa mashtaka kwa sababu akitoa ahirisho hadi Jumatatu wanaweza kwenda na sababu nyingine kuwa askari hao wapo kwenye matukio yaliyotokea baada ya Sensa.
Baada ya kuangalia mwenendo mzima wa kesi hiyo, Hakimu aliliondoa shauri hilo kwa mujibu wa kifungu cha 225 (5) sura ya 20 kwa sababu upande wa mashtaka ulishindwa kuliendesha shtaka hilo.
Wanafunzi walioachiwa huru ni Mwambapa Elias,Evalist Elias, Baraka Monesi, Hellen Mushi, Alphonce Lusako, Matrona Babu, Rolana Wilfred, Godfrey Deogratius , Munisi Denis,Evanos Gumbi pamoja na wenzao 40.
Awali Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya alidai kuwa mnamo Novemba 11 mwaka huu, eneo la Mlimani la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walifanya mkusanyiko usio halali na kusababisha uvunjifu wa amani eneo hilo.
Komanya alidai kuwa washtakiwa hao wakiwa kwenye mkusanyiko huo haramu kwa lengo la kufanya mgomo, askari wa Jeshi la Polisi waliwataka watawanyike, lakini hata hivyo wanafunzi hao walikaidi amri hiyo na kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Hata hivyo washtakiwa hao ambao walifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi, walikana mashtaka hayo na waliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika ambaye alisaini bondi ya Sh1milioni
www.mwananchi.co.tz