Thursday, November 15, 2012

DIAMOND KAANDIKA KWENYE WEBSITE YAKE, KILICHOSABABISHA AJALI YAKE NI HIKI.



HII NDIO LIST ILIYOVUJA YA MISHAHARA WANAYOLIPWA WACHEZAJI WA MANCHESTER CITY



Mgazeti ya Leo Alhamisi 15th November 2012

Kaseja na Mashabiki wa Simba

Ndugu zangu wanamichezo wa nchi hii, ni ukweli usiofichika hii filamu ya mashabiki wa simba juu ya tuhuma za kipa wao aliyetumikia timu yao kwa  kipindi kirefu na kuwapa mafanikio mengi ikiwemo ubingwa ligi kuu ni filamu mbovu kuwahi kutokea katika nchi hii,

Filamu hii niliyoibatiza jina Kaseja & Simba Fans ni filamu ambayo haina mvuto haileweki washiriki inaonekana hawakujiandaa vyema kushiriki filamu hii inaonyesha wazi washiriki wasivyo na talent kama ilivyokuwa kwa kina marehemu steven kanumba, vicent kigosi, Monalisa na wengine wengi wa kwenye tasnia ya Bongo Movie.

Filamu hii imebeba ujumbe wa ya kuwa kaseja sasa hatakiwi kuitumia timu ya simba, haina utofauti na filamu fulani ya nchini Nigeria mtoto ambaye alikataliwa kwao ila wale wanaigeria waliweza kufikisha ujumbe katika jamii kupitia filamu yao ile, maana katika jamii wapo watu wanaofukuza watoto zao hata kwa kisa ambacho kinavumilika leo usishangae mama kamchoma mwanae tena wa kumzaa mikono kwasababu kadokoa nyama jikoni.

Tujiulize ndugu zangu watanzania mashabiki wa soka je kupitia filamu hii ya kaseja & simba fans tumepata ujumbe gani kama jamii ya wapenda michezo je hali hii inafundisha nini kizazi cha kesho katika tasnia ya michezo ya nchi hii, mimi nashauri mashabiki wa simba warudi kwa director wao wa Filamu hii waandike upya script watoe part 2 itakayoonyesha kurudisha imani kwa kipa wao namba moja Juma Kaseja ili mzunguko wa pili wa ligi hali isije kuwa mbaya zaidi.

Pamoja tujenge michezo

Capt Mkami Jr

JK: Akutana Na Viongozi Wa Matawi Ya CCM Ughaibuni (DIASPORA)

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na mkewe mama Salma Kikwete wakiwa katika picha ya kumbukumbu na viongozi wa matawi ya CCM ughaibuni (Diaspora) waliowaalika kwa chakula cha mchana Ikulu ndogo mjini Dodoma Jumatano Novemba 14, 2012. Viongozi hao kutoka Marekani, Italy, India, Uingereza , Afrika kusini na India walihudhuria katika Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM uliomalizika juzi Kizota.

                                       PICHA NA IKULU

JK: CCM Msitegemee Polisi

RAIS Jakaya Kikwete juzi aliwaonya wanachama wa CCM akiwataka waache kubweteka kwa kuwategemea askari polisi katika masuala ya kisiasa, kwani kufanya hivyo watakuwa wanajidanganya.

Kikwete alitoa kauli hiyo wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM uliofanyika kwa siku tatu mfululizo katika Ukumbi wa Kizota mjini Dodoma.

Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alisema kitendo cha wanaCCM kuishi katika siasa kwa kutegemea Jeshi la Polisi hakipaswi kukubaliwa kwani kimepitwa na wakati.

“Mnaishia kulalamika tu kila siku, eti wanatukana halafu mnaishia kusema ndiyo kawaida yao…au utasikia mtu anasema eti Serikali haipo! Kazi ya Serikali siyo hiyo, hiyo ni kazi ya kisiasa maana hao ndio wenzenu,”alisema Kikwete na kuongeza:

“Sasa mnataka wakisema Serikali ya CCM haijafanya kitu polisi wawafuate, au wakisema Kikwete nchi imemshinda, polisi wakawakamate? Kama wakisema hatujafanya kitu ni kazi yenu kusema kwamba tumefanya kitu, waonyesheni barabara, shule na mambo mengine.”

Licha ya kwamba hakuwataja moja kwa moja, kauli za Rais Kikwete zilikuwa zikielekezwa kwa uogozi wa Chadema ambao kimsingi kinaonekana kuwaumiza vichwa CCM.

Huku akirudia mara kadhaa maneno hayo alisema, “Nataka mfahamu ndugu zangu kuwa tukiishi kwa kutegemea Jeshi la Polisi kufanikisha mambo yetu, tutakwisha na tutakwisha kweli.”

Kikwete aliwatuhumu viongozi wa upinzani kwamba ni waongo na kwamba wakati mwingine wamekuwa wakizusha mambo ambayo hayapo, huku wakijifanya kuwa na ushahidi wa kimaandishi.

Alimtaja Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kwamba kuna wakati aliwahi kuzusha kwamba yeye (Kikwete), na makada kadhaa wa chama hicho wakiwamo Rostam Aziz walikuwa jijini Mwanza usiku, wakati si kweli kwani siku waliyodai alikuwa Nachingwea mkoani Lindi kwenye mikutano ya kampeni za urais.

Katika mazingira hayo, aliwataka wanaCCM kila mahali kujibu hoja za wapinzani kwa kauli na vitendo na wasikubali kuburutwa kwani uongo ukiachwa kwa muda mrefu unageuka kuwa ni ukweli.

Aliwaeleza kuwa ukimya wao katika kujibu hoja za wapinzani ni sumu kwao na kwamba wenzao wameanza kuaminika zaidi yao licha ya kuwa CCM ndio wenye majibu yote.

“Mkijibu kwa hoja wanatulia, sio Polisi. Nakumbuka Mwigulu aliwajibu pale bungeni kuhusu bajeti yao mbadala. Walipoitoa kijana wetu akasimama na kupiga msumari kweli wakachanganyikiwa sasa hizo ndio kazi zinazotakiwa jamani,” alisisitiza Kikwete.

Mbali na hilo aliwaonya kuacha malumbano ya mara kwa mara akieleza kuwa hali hiyo inakibomoa chama.

Alisema baadhi ya wanaCCM wamekuwa wakitumia muda mwingi kukosoana wao kwa wao, huku wakitoa nafasi kwa adui zao.

Mwenyekiti huyo alisema hakuna mtu kutoka nje ya chama anayeweza kukidhoofisha CCM kwa hoja isipokuwa chama hicho kinaumizwa na wanachama wake ambao wamekuwa wakilumbana bila sababu.

Akizungumzia suala la wagombea urais aliwataka wanachama wenye nia kufuata taratibu zote za chama pamoja na kuvumiliana ili ifikapo Mei 2015, mkutano utafanya uamuzi wa nani anasimama kupeperusha bendera ya chama hicho.

“Kwa wale mnaotaka kugombea, andikeni hiyo tarehe tutakuja hapa kuteua, lakini msituvuruge lazima mfuate utaratibu. Utaratibu huo utatangazwa, maana mkianza kupita huko na huko ndiko tunakopata matatizo,” alisema Kikwete.

Kikwete juzi alichaguliwa kwa mara nyingine kuwa Mwenyekiti wa CCM baada ya kupata asilimia 99.92 ya kura zilizopigwa, huku kura mbili zikimkataa. Kadhalika mkutano huo uliwachagua Dk Ali Mohamed Shein kuwa Makamu Mwenyekiti (Tanzania – Zanzibar) na Phillip Mangula kuwa Makamu Mwenyekiti (Tanzania Bara).

 Na :  Julius Magodi na Habel Chidawali, Dodoma

CCM Wamhusisha Karume Na Uamsho

RAIS Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Aman Karume juzi usiku alizomewa na baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku wakimwita kwamba ni mmoja wa wanakundi la Uamsho.

Uamsho ni kundi ambalo katika siku za hivi karibuni limekuwa likihusishwa na vurugu ambazo zimekuwa zikitokea Tanzania Visiwani, ambazo zimesababisha watu kadhaa kukamatwa na kufikishwa mahakamani.

Rais Karume alikutana na zahama hiyo wakati akitoa hotuba ya kuwaaga wanaCCM baada ya kumaliza ngwe yake ya utumishi ndani ya chama hicho akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar.

Dalili za Rais Karume kuzomewa zilianza baada ya baadhi ya wajumbe kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi kuanza kutaja neno ‘Uamsho’ kila alipokuwa akizungumzia matatizo yaliyopo Zanzibar.

Hali ilikuwa mbaya zaidi pale alipokuwa akizungumzia vurugu za kidini ambazo ziliikumba Zanzibar hivi karibuni zikiongozwa na kikundi cha Uamsho.

Karume alisema kuwa kikundi cha Uamsho kina haki ya kutoa maoni yake kuhusu muungano, lakini hakipaswi kufanya vurugu kama ambavyo kimekuwa kikifanya.

Wakati akiendelea kuzungumzia suala hilo, kelele nyingi zilienea katoka kwa wajumbe wa mikoa ya Zanzibar ambao walikuwa wakipaza sauti, “ Uamsho huyo….Uamsho huyo… Uamsho huyo….”

Hali hiyo ilimfanya wakati mwingine kukatiza hotuba yake na kulazimisha kuwatuliza watu hao kwa kusema “CCM oyeee….CCM…..oyeee…Mapinduziii….”
Hata hivyo, baada ya kelele hizo kuendelea Karume alionekana kuhamaki na kuwaambia wajumbe hao kwamba amechoka kusikia akiitwa jina hilo la Uamsho.

“Nimechoka kusikia naitwa jina hilo ati,” alisema Karume na kuongeza:
“Hivi wengine wana vichwa vya samaki kwa nini mnapiga kelele wakati mimi ninapozungumza, si mniache nizungumze mambo ambayo ni muhimu zaidi kwa masilahi ya chama chetu.”

Hata hivyo, licha ya kutafuta namna ya kuwatuliza wanachama hao kwa maneno mengi na historia ya maisha yake tangu alipojiunga na Chama cha ASP mwaka 1970, bado hakukuwa na utulivu na safari hii kelele zilianza kwa pande zote za wajumbe.

Kwa upande wa wajumbe wa Bara, baadhi yao walikuwa wakipiga kelele za kumtaka kumaliza hotuba yake ambayo walisema ilishachukua muda mrefu huku wakisema hakuna cha ajabu alichokuwa akizungumza.

Mara baada ya kumaliza hotuba yake, Karume alihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Redio Deutche Welle ya Ujerumani, na alisisitiza kuwa Uamsho wana haki ya kutoa maoni yao kuhusu muungano, lakini hawaruhusiwi kuvunja sheria.

Aliwataka wanachama wa kikundi hicho kujenga hoja, kwani alisema wengine wana hoja za msingi, lakini wasitumie vitisho.

Karume alistaafu uongozi wa CCM katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti (Tanzania Visiwani) na nafasi yake ilichukuliwa na Rais wa sasa wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein.

Tofauti na utamaduni ambao CCM kimeujenga kwa viongozi wake wakuu, Karume aliendelea kuwa makamu mwenyekiti hata baada ya kustaafu urais wa Zanzibar, hivyo kumlazimisha Dk Shein kusubiri hadi juzi kuchukua nafasi hiyo.

Kwa kawaida, viongozi wa ngazi ya Rais wa Muungano na Zanzibar, baada ya kuondoka katika nafasi zao za uongozi wa nchi, pia huachia madaraka ndani ya chama na kumwachia Rais mpya.

 Na : Julius Magodi na Habel Chidawali, Dodoma
Chanzo:  http://www.mwananchi.co.tz/habari/kitaifa