
Mshikamano wa pamoja unahitajika baina ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea ili kuhakikisha kuwa mtoto wa kike ambaye hajapata nafasi ya kwenda shule anapata elimu, kuwainua wanawake kiuchumi na kupunguza vifo vya kinamama wajawazito na watoto vinavyotokana na tatizo la uzazi na ugonjwa wa kansa.
Hayo yamesemwa jana na Mke wa rais Mama Salma Kikwete wakati akichangia mada kwenye mkutano wa The RAND African First Ladies Initiative uliofanyika makao Makuu ya Taasisi ya Ford mjini New York nchini Marekani.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa taasisi mbalimbali za Kiserikali na zisizo za kiserikali zinafanya jitihada kubwa ya kuhakikisha kuwa zinawasaidia wanawake wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha tatizo lililopo ni upungufu wa rasilimai fedha za kuweza kukabiliana na changamoto hizo hivyo basi ushirikiano wa pamoja unahitajika ili kuweza kufanikisha malengo hayo.
Aliendelea kusema kuwa watoto wa kike wakipata elimu ya kutosha watakuwa na silaha muhimu katika maisha yao ya kuweza kupambana na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na maradhi, ujinga na umaskini kwani elimu ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa lolote Duniani bila ya watu kuwa na na elimu nchi haiwezi kuendelea.