Tuesday, November 6, 2012

Familia Ya Mwangosi Kuishtaki Serikali, Polisi

FAMILIA ya aliyekuwa mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daud Mwangosi anayedaiwa kuuawa na polisi akiwa kazini, inakusudia kuishtaki serikali na Idara ya Polisi kwa kusababisha mauaji hayo.

Mwangosi aliuawa Septemba 2, mwaka huu wakati akikusanya habari za ufunguzi wa tawi la Chadema Kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi.

Kusudio la kuishtaki serikali limekuja huku askari anayedaiwa kumuua Mwangosi,  Pacificius Cleophase Simon akiwa amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa, kesi inaendelea.
Akizungumza kwa simu jana, mke wa Mwangosi, Itika alisema familia hiyo imeamua kuchukua uamuzi huo baada ya kuona viongozi wa serikali hawajali.

Itika alisema hadi sasa familia hiyo inajiuliza maswali ya kilichosababisha polisi watumie nguvu kubwa kumuua mume wake na kwamba, wanadhani wanao wajibu wa kuishtaki serikali na polisi.

“ Ukiangalia picha ile unaona kwamba Mwangosi kabla ya kuuawa alikuwa amezungukwa na askari saba, ni kwanini aliuawa kama jambazi, bado wingu zito limetanda katika familia na tunadhani haki itapatikana mahakamani,” alisema Itika.

Alisema wako katika mazungumzo na wanasheria watakaowasaidia katika kesi hiyo na kwamba, wakikamilisha wananchi watajulishwa.

Ripoti ya kamati iliyoundwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuchunguza kifo hicho, ilisema Mwangosi aliuawa kwa makusudi na polisi chini ya usimamizi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.

 Na: Raymond Kaminyoge,Mwananchi.

Mnyika Amuwashia Moto Waziri Muhongo

 Mbunge wa Ubungo Mh. John Mnyika bungeni leo akiwasilisha hoja kuhusiana na Uhaba wa Mafuta nchini.
                        Waziri Mkuu Mizengo Pinda (aliyesimama) akijibu hoja ya Mh. John Mnyika.

Mbunge wa Ubungo (Chadema) John Mnyika akihoji Kiti cha Spika juu ya serikali kushindwa kuleta bungeni kauli ya serikali juu ya mkakati wa kukabiliana na uhaba wa mafuta nchini Tanzania.

Uhaba wa mafuta leo umewakimbiza kwenye kikao cha Bunge mjini Dodoma asubuhi, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na naibu mawaziri wake George Simbachawene na Steven Masele.

Waziri huyo na naibu mawaziri wake hawakuwepo bungeni leo wakati Mbunge wa Ubungo (Chadema) John Mnyika akiitaka serikali itoe sababu ya kutokuja bungeni leo kutoa tamko la serikali jinsi inavyoshughulikia suala la uhaba wa mafuta nchini.

Spika wa Bunge Anne Makinda alimlazimisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kusimama na kujibu hoja ya Mnyika aliyemtaka Spika kulazimisha serikali ijibu hoja yake pamoja na mkakati wa serikali wa kutatua uhaba wa mafuta nchini.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda alilazimika kunyanyuka na kusema kwa ufupi kuwa serikali ilikuwa ikijiandaa na kuja na hoja nzito ya kueleza umma mikakati kabambe ya kutatua uhaba wa mafuta nchini.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

JINSI MASHABIKI WA SIMBA WALIVYOANDAMANA, NA MAJINA YA WANAOTAKA WAONDOKE SIMBA.

Mashabiki wa Simba novemba 5 2012 waliandamana mpaka makao makuu ya club hiyo Msimbazi Kariakoo Dar es salaam wakiwa na mabango mbalimbali yanayomaanisha wamechoka na ishu mbalimbali za club hiyo.

Mabango mengine yalisomeka kwamba mamluki wajirekebishe Simba mmeikuta, mengine Ndugu Kaburu kocha wetu Milovan mchango wake mkubwa bado tunamuhitaji, Kaseja tuachie timu yetu.

Hiyo yote imetokana na Simba kufungwa 2-0 na Mtibwa Sugar novemba 4 2012 Morogoro.

Baada ya kichapo hicho katika msimamo wa ligi kwa timu kongwe jijini Dar es Salaam, YANGA SC imepanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuifunga Azam FC 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo unaifanya Yanga iongoze Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 26 ikiwa imebakiza mechi moja ya mzunguko wa kwanza dhidi ya Caostal Union mjini Tanga ikifuatiwa na Simba SC yenye pointi 23 ambayo  imefungwa 2-0 na Mtibwa Sugar Morogoro.

Nawakariri baadhi ya mashabiki walioandamana wakisema “tumefungwa kwa sababu ya Kaseja, kamuingilia kocha kapanga timu tumefungwa, huyu mtoto mpaka anapata dhambi… alikua hadaki mechi ya jana, kwanza tunajua kiwango chake kimeshuka na inasemekana na yeye anahusika kwenye kababu, kama anachukua hela imani yake yeye mwenyewe ila sisi tunachojua uwezo hana wa kuidakia timu yetu ya Simba, sio swala la kufungwa tu isipokua ni mwenendo mzima wa Simba Sc kuwa na matatizo ambayo yako sehemu mbili, kwa wachezaji ambao wana matabaka na viongozi pia wana matabaka, viongozi wameshindwa kuiongoza timu”

Magazeti ya leo Jumanne ya 6th November 2012