Tuesday, July 10, 2012

Mgomo Wa Wenye Mabasi Watikisa Arusha, Kilimanjaro

MGOMO mkubwa wa wamiliki wa mabasi jana uliathiri huduma za usafiri kati ya Miji ya Arusha na Moshi mkoani Kilimanjaro, na kusababisha adha ya usafiri kwa abiria na ulanguzi wa nauli kutoka Sh2,500 ya kusafiri kati ya miji hiyo miwili hadi kufikia Sh10,000.

Juzi, mgomo huo ulitikisa zaidi usafiri wa mabasi ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro baada ya wamiliki kupinga hatua ya Halmashauri ya Manispaa ya  Moshi kuongeza ushuru kutoka kiasi cha Sh1,000 hadi kufikia Sh2,000 bila kushirikishwa.

Mgomo huo jana, uliingia katika hatua mpya baada ya wamiliki wenzao wa Mkoa wa Arusha nao kuingia katika mgomo na kusababisha msururu wa watu barabarani, huku watoa huduma za pikipiki maarufu kama bodaboda wakineemeka na mgomo huo.

Mbali ya bodaboda kutoa huduma, baadhi ya abiria waliokuwa wakisafiri kati ya Arusha na Moshi  walilazimika kutumia usafiri wa magari madogo aina ya Naoh, ambayo yalikuwa yakipakia abiria kwa kificho pembezoni mwa miji hiyo kuepuka kushambuliwa na wasafirishaji waliokuwa kwenye mgomo.

Abiria walioathiriwa zaidi na mgomo huo ulioanza saa 11:00 alfajiri ni wale waliokuwa wakisafiri kati ya Moshi-Arusha na wilaya nyingine za Mkoa wa  Kilimanjaro na wanaotegemea usafiri wa daladala.

Misururu mirefu ya abiria wakiwamo wanafunzi walionekana wakitembea kwa miguu kutoka majumbani kwenda shuleni, huku watu wengine wanaokwenda kazini nao wakijikuta katika adha hiyo na kulazimika kutumia usafiri wa malori na toyota aina ya Pick-Up.


Manispaa ya Moshi imepandisha ushuru kutoka Sh1,000 kwa siku kwa basi dogo hadi Sh1,500 na kutoka Sh1,000 hadi Sh2,000, sawa na ongezeko la asilimia 100.

Kauli ya Akiboa
Katibu wa Chama cha Wasafirishaji abiria Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro (Akiboa), Locken Adolf alithibitisha jana wanachama wake
kugoma kushinikiza Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kukaa nao mezani kujadili ongezeko hilo.

“Kimsingi, hatupingi ushuru wa Serikali, tunachopinga ni manispaa kuongeza ushuru wa maegesho kwenye stendi za Moshi kwa asilimia 100 kutoka Sh1,000 ya awali hadi Sh2,000 bila hata kushauriana na sisi wadau wa usafirishaji,” alisema Locken.

Alifafanua kwamba, baada ya juhudi zao kutafuta ufumbuzi wa suala hilo kupitia
vikao walivyofanya kati yao na uongozi wa Manispaa ya Moshi pamoja na
ofisi ya mkuu wa wilaya kushindikana, wameamua kusitisha huduma hadi mwafaka utakapopatikana.

Katibu huyo wa Akiboa alisema, kilichowasukuma kugoma ni kauli aliyodai kutolewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Ibrahim Msengi na
uongozi wa Manispaa kuwa mfanyabiashara asiyemudu kulipa ushuru huo
aegeshe gari lake nyumbani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Akiboa, Hussein Mfinanga alisema mgomo huo unatarajiwa kudumu kwa siku tatu mfululizo.Mfinanga alisema kwa ongezeko hilo la ushuru kwa halmashauri hizo mbili, kunaamaanisha kuwa mmiliki wa mabasi atalipa ushuru mkubwa kuliko unaotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA).

“TRA ambako ndio sheria mama ya kodi ipo na inapitishwa na Bunge tunalipa Sh190,000 kwa Hiace na 520,000 kwa mabasi makubwa kwa mwaka, iweje ushuru wa halmashauri uwe juu ya TRA?,”alihoji.

Kiongozi huyo alisema kwa siku ya jana baadhi ya mabasi makubwa ya abiria kwenda Dar es Salaam  na Morogoro, yaliendelea na safari kwa kuwa tayari walikuwa wamewakatia abiria wao tiketi.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani  Kilimanjaro, Peter Simma alipoulizwa juu ya msimamo huo, alisema wanaopaswa kubebeshwa mzigo wa suala hilo ni Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.

Meya wa Manispaa hiyo, Jaffar Michael alisema ushuru huo ulipandishwa kwa nia njema ili kupanua wigo wa mapato ambayo yatatumika katika shughuli za miradi ya maendeleo ya wananchi.

Alifafanua kwamba kwa sasa wapo kwenye mazungumzo na mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuangalia kama wasitishe viwango hivyo vipya kwa muda wakati wakiendelea kujadiliana na wadau

Hata hivyo, kwa Arusha magari madogo ya abiria maarufu kama daladala yanayofanya safari zake ndani ya jiji hilo na vitongoji vyake, yaliendelea kutoa huduma wakati usafiri wa ndani ya Mkoa ya  Kilimanjaro hakukuwa na huduma hizo za usafiri baada ya daladala nazo kuingia kwenye mgomo huo.

Kwa upande wao wamiliki wa daladala, wanapinga ongezeko la ushuru kutoka Sh1,000 hadi Sh1,500 kwa madai hayo ya kutoshirikishwa kabla ya uamuzi huo kufikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.

Wakati hali ikiwa hivyo, kuna madai kuwa mgomo huo una mkono wa vyama vya siasa huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikituhumiwa kuhujumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho kinaongoza halmashauri hiyo.

Hata hivyo, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi, Alu Sigamba alikanusha tuhuma hizo akisema, chama hicho kiliingilia kati kutafuta ufumbuzi wa
mgomo huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wasafirishaji kupitia chama chao cha Akibo

Rais wa Chama cha Madaktari Afikishwa Mahakamani Leo

Rais wa Chama cha madaktari Tanzania MAT Dr Namala Nkopi hii leo amefikishwa katika mahakama ya hakim kazi kisutu kujibu mashtaka yanayohusiana na mgomo wa madaktari.

Kwa mujibu hakimu anayesikiliza kesi hiyo Faisal Kahama, Dr Mkopi amesomewa mashtaka 2 ambayo ni
1) Kutotii amri ya mahakama ya kutangaza kusitisha mgomo
2) kuhamasisha mgomo

Hata hivyo mshtakiwa amekana mashitaka hayo na kuachiwa kwa dhamana ya watu wawili ambao ni watumishi wa serikali wakiwa na vitambulisho vya kazi na shillingi laki 5 kila mmoja.

Mawakili wa serikali walipinga masharti hayo na kuomba Hakim aongeze masharti ikiwa ni pamoja na Dr Nkopi kusalimisha hati yake ya kusafiria lakini hakim aliyakataa maombi hayo na kusisitiza kuwa maamuzi aliyoyafanya yatabaki kama yalivyo.

Saintfiet kuvuna Sh288 mil Yanga

KOCHA mpya Yanga, Tom Saintfiet aliyeingia mkataba wa kufundisha klabu hiyo ya Jangwani, atavuna Sh288 milioni iwapo mkataba wake hautaishia njiani.

Katika kipindi cha miaka mitano, Yanga imekuwa na makocha tofauti, baadhi wakishindwa kudumu klabuni kama mikataba yao ilivyokuwa ikielekeza.

Makocha waliofundisha Jangwani tangu 2007 na kuondoka kwa sababu mbalimbali, nyingi kutokana na kushindwa kutekelezwa kwa makubaliano ni Milutin Sredojovic, Dusan Kondic, Kostadin Papic na Sam Timbe.

Hata hivyo, Papic aliyekuja nchini mara ya kwanza mwaka 2009, alirejea mwaka jana baada ya Timbe aliyeipa jangwani taji la Ligi Kuu na Kombe la Kagame kutimuliwa.

Katikati ya wiki iliyopita Kocha, Saintfiet raia wa Ubelgiji
aliingia mkataba wa miaka miwili kuifundisha Yanga kwa mshahara wa Sh12 milioni.

Ina maana, katika kipindi cha mwaka mmoja, Saintfiet aliyetamba kuleta mafanikio Jangwani, tavuva Sh144 milioni.

Mshahara huo unamzidi kwa Sh730,000 kocha aliyeondoa muda mfupi baada ya kumalizika kwa msimu, Kostadin Papic kutoka nchini Serbia.

Habari za uhakika toka ndani ya klabu hiyo zimedaiwa kupanda kwa mishahara ya wachezaji, ambapo wa chini utakuwa Sh800,000 na wa juu Sh1.5milioni.

Micho ambaye sasa ni Kocha wa timu ya taifa ya Rwanda (Amavubi), aliondoka nchini baada ya timu hiyo kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Ndogo mwaka 2007.
Mtihani wa kwanza wa Saintfiet katika utekelezaji wa ahadi yake ya kuleta mafanikio, Jangwani unaanza leo kwa mechi ya kirafiki dhidi ya JKT Ruvu

Yanga inashuka Uwanja wa Taifa kupambana na maafande hao katika mchezo wenye sura ya maandalizi kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame inayoanza Jumamosi wiki hii.

Lakini pia Bosi, Saintfiet ataitumia mechi hiyo kuwachambua wachezaji wake walioonyesha uwezo ili aweze kujenga mhimili wa kikosi cha kwanza.

Kwenye kikosi hicho kuna wachezaji wengi wameonyesha uwezo jambo ambalo ni wazi litampa wakati mgumu kuchagua kikosi cha kwanza.

Kumekuwa na ushindani mkubwa kwenye kikosi hicho chenye mchanganyiko wa wachezaji na chipukizi kadhaa wapya kama Frank Domayo, Simon Msuva na David Luhende.

Domayo na Msuva wametishia nafasi za wakongwe kama Nurdin Bakari, Juma Seif na Hamis Kiiza baada ya kuonyesha kiwango kikubwa katika pambano la kirafiki dhidi ya Express ya Uganda hivi karibuni.

Naye Luhende anayecheza nafasi beki ya kushoto ameonekana kumkuna Saintfiet baada ya kutisha katika mazoezi ya timu hiyo hivu karibuni, hivyo kuwafanya wapinzani wake wa nafasi hiyo Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua na Godfrey Taifa kuwa mtegoni.

Nayo JKT ambayo msimu uliopita ilishindwa kutamba itautumia mtanange huo kama sehemu ya kuona makali yake kabla ya kuingia katika hekaheka za Ligi Kuu msimu ujao.

POLISI KUWAHOJI KWA MATAMSHI KWAMBA WANATISHIWA MAISHA, DK NCHIMBI ASEMA WANASABABISHA CHUKI

KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Godbless Lema huenda wakajikuta matatani kutokana na madai waliyoyatoa juzi kwamba wanatishiwa kuuawa na kigogo mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa.Kutokana na matamshi hayo, jana Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi ameliagiza Jeshi la Polisi kuwahoji viongozi hao ambao walidai kuwa mauaji hayo yamepangwa kufanywa kwa kuwekewa sumu kwenye chakula au kwa kutumiwa makundi ya ujambazi.

Akizungumza na waandishi wa mjini hapa jana, Dk Nchimbi alisema licha ya kudai kwamba wanatishiwa, ameshangazwa na msimamo wa viongozi hao kukataa kupeleka suala hilo polisi kwa madai ya kuhofia suala hilo halitafanyiwa kazi.

Alisema watawahoji viongozi hao kwa sababu suala la usalama wa Mtanzania yeyote si la hiari, bali ni la kikatiba na la kisheria hivyo, ni lazima polisi watimize wajibu wao.

“Ni lazima tuwahoji ili tujue ni nani amewatisha na kwa sababu zipi. Hatutamuomba mtu ruhusa ya kumlinda kwa sababu huo ni wajibu na kazi yetu kuwalinda raia, hilo halina mjadala. Hatua zitachukuliwa endapo itabainika kuwa madai yao yana ukweli,” alisema Dk Nchimbi.

Aliwataka viongozi wote wa kisiasa wakiwamo wa Chadema wanapohisi kutishiwa usalama wao, watoe taarifa polisi ili vyombo vya dola viyafanyie uchunguzi malalamiko yao ili utaratibu ufanyike kuhusu usalama wao kama sheria inavyotaka.

Alionya tabia ya viongozi kuzungumza nje ya utaratibu akisema haikubaliki kwani inaweza kuwa ni mbinu za kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

Dk Nchimbi alisema jambo hilo si jema kwani linajenga hofu miongoni mwa Watanzania na kuwafanya wasiviamini vyombo vyao vinavyowalinda kwa mujibu wa sheria.
“Ni kweli kuwa kila mwanasiasa anataka kukubalika na umma lakini, akubalike katika taratibu zinazokubalika,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza:

“Ingekuwa Serikali inataka kukubali umaarufu kama huo, basi ingetumia mwanya wa haohao Chadema wakati mitandao ya kijamii iliposambaza taarifa kuwa Chadema ilihusika na kifo cha marehemu, Chacha Wangwe.”

Alisema Serikali haikukurupuka na kuwakamata, badala yake ilifanya uchunguzi kwanza na matokeo yake alikamatwa dereva wake ambaye ameshachukuliwa hatua.
Alisema kama Serikali ingekuwa inatafuta umaarufu, ilikuwa ni fursa nzuri kwake kujipatia umaarufu na kukivuruga chama hicho kwa kuwakamata viongozi wa Chadema hasa baada ya kuwapo kwa uvumi kwamba wamemuua kiongozi huyo.

“Viongozi wetu wa kisiasa ni lazima wafanye mambo ambayo kesho na keshokutwa watakiri mchango wao, ama katika ujenzi au uharibifu wa nchi yetu. Kila siku wakilalamika kuwa wanataka kuuawa basi ni lazima watu watawashangaa kwani badala ya kutatua matatizo ya wananchi wanabaki wakilalama wanataka kuuawa. Watu kama hawa wanafanya hivi kwa masilahi yao, wanaweza kuwagombanisha wananchi.”

Waziri Nchimbi aliwataka wananchi na viongozi wa kisiasa kuondoa hofu kwani Serikali ina wajibu wa kuwalinda na hakuna mtu atakayenufaika kwa mauaji ya wanasiasa hao.

Kuhusu madai kwamba polisi wamekuwa wakipuuza malalamiko ya wapinzani, Dk Nchimbi alikiri kuwapo kwa baadhi ya polisi wenye kasoro katika utendaji wao lakini akasema wengi ni waadilifu.
Alisema ikiwa kuna mtu haridhishwi na utendaji wa polisi kwa kutopata huduma kama inavyostahili, ana uhuru wa kutoa taarifa katika ngazi za juu hata ikiwa ni kwake.

Ikulu nayo yatoa tamko
Katika hatua nyingine, Ikulu imesema hakuna mpango wowote unaoratibiwa na Idara ya Usalama wa Taifa kwa lengo la kuwaua viongozi hao wa Chadema.
Jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alihoji sababu za Serikali kutaka kuwaua viongozi hao wakati si tishio lolote kwa nchi.

Balozi Sefue alisema Idara ya Usalama wa Taifa haiko kwa ajili ya kuua raia au viongozi, bali kulinda masilahi ya taifa na kuhoji: “Sasa kwa nini wauawe? Wana nini hasa hadi Idara ya Usalama ifanye hivyo?”

Alisema ni vyema wakati mwingine kukawa na umakini kwa kuangalia namna siasa zinavyoweza kufanya kazi... “Hii inaweza kuwa siasa tu. Sisi serikalini hatuna mambo ya vyama, tunafanya kazi kwa ajili ya watu wote.”

Alisema Idara ya Usalama wa Taifa na Serikali hazifanyi kazi kisiasa, bali kwa kuangalia masilahi ya Watanzania wote: “Huku serikalini sisi hatuna ugomvi na wanasiasa. Tunafanya kazi na watu wote.”
Alisema wanaoweza kufikiria kuwa kuna siasa katika Serikali na vyombo vyake wao ndiyo wanaweza wakawa wanafanya siasa.

Tuhuma za Chadema
Kauli hizo za Serikali zinatokana na tuhuma za Chadema kwamba kimebaini njama za kuwaua viongozi wake hao waandamizi ambazo zinaratibiwa na kigogo mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa na kwamba nyendo zao zimekuwa zikifuatiliwa kwa saa 24.

Tuhuma hizo za Chadema zilitolewa juzi na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni akisema: “Sisi Chadema hatuna mambo ya siri tunayotaka kufanya katika nchi hii. Matatizo ya Watanzania yapo wazi na yanajulikana na kila mmoja, Serikali ya CCM itekeleze sera na ahadi zao kwa wananchi na si vitisho.”Chanzo. Mwananchi

KOCHA MKUU WA TAIFA STARS KUWA MGENI RASMI LIGI YA KUIBUA VIPAJI

  KOCHA mkuu wa timu ya Tanzania(Taifa Stars),Kim Poulsen anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mashindano ya ligi ya ya kuibua vipaji vya soka la vijana inayojulikana kama Moivaro Youth Football League(MYFL) ambayo itatimua vumbi mnamo septemba 29 mwaka huu mkoani Arusha.

Pia,viongozi mbalimbali wa ngazi za soka mkoani Arusha na nchini kwa ujumla akiwemo mtaalamu wa masuala ya ufundi wa shirikisho la soka nchini(TFF),Sunday Kayuni anatarajiwa kuwa miongoni mwa wageni walioalikwa katika ligi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkurugenzi na mwasisi wa Taasisi ya Future Stars Aademy ya jijini hapa,Alfred Itaeli alisema kwamba ligi hiyo itashirikisha timu za wanawake pia ambapo usajili wa timzu zitakazoshiriki  unataraji kuanza Agosti 18 mwaka huu.

Itaeli ,alisema kwamba kabla ya  ligi hiyo kutimua vumbi wameandaa mafunzo ya wiki mbili kwa waamuzi  wenye umri  kati ya miaka 8 hadi 15 ambao watatumika kuchezesha ligi hiyo ili kuepuka gharama za kukodi waamuzi mbalimbali ambapo mafunzo hayo yatandeshwa na mwamuzi mkongwe nchini Billy Mwilima.

Alitaja lengo kuu la ligi hiyo ni kukuza vipaji vya soka nchini na kuweka ushindani kwa kila rika huku akisisitiza kuwa kwa kuwa ligi hiyo haina wadhamini wameamua kutoza kiasi cha sh,100,000 kama ada za kiingilio.

Na Ashura Mohamed-Arusha

NASSARI AIPONGEZA HALMASHAURI YA MERU KUPATA HATI SAFI

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki Bw.Joshua Nassari ameipongeza halmashauri ya Meru kwa kupata hati safi kutokana na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) baada ya halmashauri hiyo kuwa na usimamizi mzuri wa fedha za umma.

Akizungumza katika baraza la madiwani la lililofanyika katika halmashauri hiyo bw.Nassari alisema kuwa halmashauri nyingi zinashindwa kusimamia matumizi bora ya fedha halia ambayo inapelekea hamlashauri hizo kupata hatia chafu ama za mashaka.

Bw.Nassari alieleza kuwa ili kuhakikisha kuwa halmashauri hiyo iweze kuendelea kufanya vizuri ni wazi kuwa ushirikiano wa karibu wa viongozi hao unahitajika bila kujali  itikadi za vyama vya siasa ili wananchi wa jimbo hilo waweze kupata maendeleo.

Aidha alisema kuwa pindi halmashauri inapopata hati chafu serikali kupiti Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) hupunguza fedha za miradi ya maendeleo ama kutopeleka kabisa kutokana na kuona kuwa kama halmashauri hizo hazina mahitaji ya fedha kutokana na matumizi mabaya hali ambayo inapelekea miradi ya maendeleo kurudi nyuma.

Pia alieleza kuwa swala la fedha  ni tatizo katika halmashauri nyingi hivyo ni vyema kama kuhakikisha kuwa halmashauri inakuwa na mipango madhubuti na mikakati ili miradi mbalimbali ya maendeleo isirudi nyuma wala kuyumba.

Lakini hata hivyo bw.Nassari alieleza wazi kero ya gari la Zimamoto katika halmashauri ya Meru ni kubwa lakini jitihada za makusudi zinahitajika ili kwa kushirikiana na halmashauri hiyo ili gari liweze kupatikana ili kupunguza madhara pindi ajali za moto zinapojitokeza.

Halmashauri ya Meru ni moja kati ya halmashauri zilizopatiwa hati safi pamoja na kuongoza katika nafasi ya kwanza kitaifa kwa upande wa Usafi sherehe zilizofanyika mkoani Kilimanjaro na Mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete.

Imeandaliwa Na Ashura Mohamed-Arumeru

TAARIFA KUHUSU MADAKTARI WALIO KATIKA MAFUNZO KWA VITENDO (INTERNS)


Wizara imepokea malalamiko kuwa kati ya tarehe 23 juni, 2012 hadi  tarehe  29 juni, 2012, Madaktari walio katika mafunzo kwa vitendo 372 kati ya 763 katika hospitali mbalimbali nchini, waligoma kutoa huduma kwa wagonjwa ikiwa ni wajibu wao  kama madaktari.Kitendo hicho sio tu kilihatarisha usalama wa wagonjwa waliohitaji huduma za matibabu katika hospitali hizo, bali kilikuwa ni ukiukwaji wa maadili ya taaluma

Madaktari hao waliogoma walirejeshwa Wizarani kwa barua kutoka kwenye mamlaka za hospitali walikokuwa wakifanyia mafunzo kwa vitendo.

Kwa kuwa Wizara ndio yenye dhamana ya usimamizi wa huduma za afya nchini, na kwa kuwa madaktari hao wamesajiliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika, hivyo Wizara imewasilisha malalamiko haya huko ili Baraza liwachunguze na kuamua hatma yao kitaaluma.

Kwa hivi sasa madaktari hao hawako maeneo yao ya kazi, na suala hili limepelekwa Baraza la Madaktari kwa uchunguzi kuhusu kitendo walichokifanya, hivyo Wizara inasitisha posho zao kuanzia Tarehe 1 Julai, 2012 hadi hapo itakapopata taarifa ya uchunguzi wa Baraza la Madaktari.

Madaktari wengine waliogoma, taratibu za kiutumishi zitachukuliwa na mamlaka ya ajira zao kwa mujibu wa sheria na taratibu husika.

Regina L. Kikuli
KAIMU KATIBU MKUU
09.10.2012

Magazeti ya Leo 10th July


KAMISHNA WA POLISI ANAEDAIWA KWAMBA DR ULIMBOKA KAMTAMBUA ALIHUSIKA KUMPIGA NDIO HUYU.

Habari zilizoenea katika mitandao ya kijamii inayotumiwa sana na watanzania wengi muda mfupi baada ya kamishna msaidizi wa polisi Ahmed Msangi kumtembelea hospitali kiongozi wa Madaktari Dr UlimbokaSteve ambapo mistari kadhaa imesambazwa kwenye mitandao hiyo ikimuhusu Kamanda Msangi.

Mistari ambayo ni maarufu ambayo inadaiwa kutolewa na mtu anaedai alisikia kila kitu ni kwamba Dr Ulimboka alipomuona tu Kamanda Msangi amekwenda kumtembelea hospitalini, alianza kumwambia ampe viatu vyake pamoja na simu yake, ikimaanisha kwamba Ahmed Msangi alikuepo wakati Dr Ulimboka akifanyiwa huo ukatili.

 Msangi amesema “hata mimi hizo habari nimezisikia na kuzisoma kwenye mitandao na msg zinazotumwa, kiukweli taarifa hizo zote sio za kweli kuna mtu tu amekaa na kuona atunge kitu labda kwa malengo yake mwenyewe, ni kweli nilikwenda kumtembelea hospitalini na nilipitia kwa mkurugenzi wa Moi na ndio tukaambatana pamoja kwenda wodini kumuona Ulimboka, ananifahamu na mara nyingi tunakutana hata kwenye sehemu za kufurahi hivyo akanihadhia jinsi ilivyokua na nikamuuliza maswali kwa ajili ya upelelezi”

Haijawezekana kumpata dr Ulimboka sasa hivi kwa sababu ya taratibu za hospitali, lakini nitaitumia nafasi kwa saa chache zijazo… mpango ukifanikiwa ripoti utaipata manake neno lake yeye ni muhimu sana kwenye hii ishu. Chanzo: Exclusive na millardayo.com


DR. ASHA ROSE MIGIRO AREJEA NCHINI

Mratibu Mkazi wa Umoja Mataifa nchini Dr. Alberic Kacou (katikati) akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere kumpokea Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dr. Asha Rose Migiro aliyemaliza muda wake leo wakati akirejea nchini Tanzania. Kushoto ni Afisa wa Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa nchini Hoyce Temu.
Baadhi ya Mabalozi, Wahadhiri na Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakiwa wamejipanga kumpokea Dr. Asha Rose Migiro.
Msafara wa Dr. Asha Rose Migiro ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje Mh. Benard Membe (gari la pili) kuelekea sehemu maalum ya mapokezi.
 Dr. Asha Rose Migiro akishuka kwenye gari yake baada ya kukanyaga Ardhi ya Tanzania.
Dr. Asha Rose Migiro akipokelewa kwa shangwe na zawadi za maua kutoka kwa ndugu, jamaa, marafiki na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje waliofika kumlaki.
Dr. Asha Rose Migiro akisalimiana na baadhi ya mabalozi wapya walioteuliwa na Mh. Rais hivi karibuni. Kushoto ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Dr. Alberic Kacou.
Dr. Asha Rose Migiro akiendelea kusalimiana na Baadhi ya Mabalozi. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Benard Membe sambamba na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Dr. Alberic Kacou.
Waziri Membe na Dr. Migiro wakielekea kwenye chumba maalum cha mapumziko kabla ya mkutano na waandishi wa habari.
Dr. Asha Rose Migiro (katikati), akizungumza na waandishi wa habari nchini Tanzania baada ya kumaliza muda wake kama Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambapo pamoja na mambo Mengi amesisitiza kwamba hatojihusisha na siasa kwa sasa. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Benard Membe na Kulia ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Dr. Alberic Kacou.
Dr. Asha Rose Migiro (katikati) akiteta jambo Waziri Membe sambamba na Viongozi mbalimbali wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini wakiongozwa na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Dr. Alberi Kacou (kushoto) waliofika kumlaki katika Uwanja wa Ndege wa Mwl. J.K Nyerere.
Pichani Juu na Chini ni wakinamama wakimwimbia Happy Birthday Dr. Asha Rose Migiro ikiwa ni maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa aliporejea nyumbani leo.
                                   Kikundi cha Ngoma kikitoa burudani kwa Dr. Migiro
Dr. Asha Rose Migiro akizungumza Jambo na Dr. Alberic Kacou wakati wakitizama burudani ya ngoma iliyoandaliwa maalum kwa ajili yake. Kushoto ni Waziri Membe.
                                  Dr. Migiro akiwasalimia wasanii wa kikundi cha ngoma.
                  Dr. Asha Rose Migiro akiagana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa Dr. Alberic Kacou.

     "Karibu tena Nyumba Mama"... Waziri Membe akiagana na Dr. Asha Rose Migiro baada ya mapokezi.
Dr. Asha Rose Migiro akiondoka katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere sambamba na ulinzi mkali wakiwemo maafisa wa kimataifa kutoka Ufilipino waliohakikisha ametua nchini Salama.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) ambaye amemaliza muda wake, Dk. Asha Rose Migiro, amerejea nyumbani leo na kusema kwamba anatarajia kurudi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alikuwa akifundisha kabla ya kuingia kwenye ulingo wa siasa. Kinyume na matarijio ya watu wengi, Dk. Migiro amesema kuwa kwa sasa hatarajii kujishughulisha katika mambo ya siasa na wala hana mipango ya kugombea urais siku za mbele.

Amesema kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amamteua kuwa Balozi Maalum wa Malaria katika Bara la Afrika na kuongeza kuwa pamoja na kwamba shughuli hizo atakuwa anazifanya kwa muda wake mchache, bado kuna uwezekano mkubwa zikambana na kushindwa kujishughilisha na mambo ya kisiasa. Chanzo: globalpublishers