Thursday, August 2, 2012

Wakimbizi Wa Burundi Wavuliwa Hadhi Ya Ukimbizi

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali, kuanzia tarehe 01 Agosti, 2012, imewavua hadhi ya ukimbizi wakimbizi 38,050 wa kutoka Burundi wanaohifadhiwa katika kambi ya wakimbizi ya Mtabila iliyoko wilayani Kasulu mkoani Kigoma.Uamuzi huu wa kuwavua hadhi ya ukimbizi umefanywa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi kwa Mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 4 cha Sheria ya Wakimbizi.

Kufuatana na Sheria hiyo mkimbizi anapoteza hadhi ya ukimbizi kama mazingira yaliyomfanya kuwa mkimbizi yatakuwa hayapo tena, na atavuliwa hadhi hiyo kama ataendelea kukaidi maagizo halali ya kumtaka kurejea kwao kwa hiari.

Hatua ya kuwavua hadhi ya ukimbizi wakimbizi hawa imefikiwa baada ya Serikali za Tanzania na Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kujiridhisha kuwa hapakuwa tena na sababu ya kuendelea kuwahifadhi wakimbizi hao baada ya hali ya amani kurejea nchini mwao na hivyo kuwataka kurejea kwao.

Zoezi la kuwasaili wakimbizi waliopo katika kambi ya wakimbizi ya Mtabila lilifanyika kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba mwaka 2011 kwa lengo la kubaini kama walikuwepo wakimbizi wenye sababu za msingi za kuendelea kuwepo nchini, ambapo ilibainika kuwa wakimbizi 38,050 hawakuwa na sababu za kuendelea kuwa wakimbizi.

Kufuatia matokeo ya zoezi hilo, Kikao cha Pande Tatu, kilichojumuisha wawakilishi wa Serikali za Tanzania na Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), kilifanyika jijini Bujumbura nchini Burundi tarehe 22 Februari, 2012 na kukubaliana kwa pamoja kuifunga kambi ya Mtabila ifikapo tarehe 31 Desemba, 2012.

Baada ya kuwavua hadhi ya ukimbizi, raia hawa wa Burundi sasa wataendelea kusaidiwa kurejea kwao kwa hiari hadi tarehe 31 Desemba mwaka huu, ambapo Kambi hiyo ya Mtabila itafungwa rasmi, na wale ambao watakuwa hawajaondoka baada ya tarehe hiyo watachukuliwa kuwa ni wahamiaji haramu, na kushughulikiwa kufuatana na Sheria ya Uhamiaji.

Historia ya hifadhi ya wakimbizi hapa nchini ilianza tangu mwaka 1961 ambapo Tanzania ilikuwa na idadi kubwa ya wakimbizi kutoka nchi mbalimbali za Afrika, idadi ambayo katika miaka ya tisini ilifikia takribani milioni moja, 641,386 kati yao wakiwa ni wakimbizi kutoka Burundi.

Zoezi la kuwarejesha kwao wakimbizi wa Burundi lilianza rasmi mwaka 2002 baada ya nchi yao kurejea katika hali ya amani na hadi sasa kambi nane zilizokuwa zikihifadhi wakimbizi toka Burundi zimefungwa. Kambi hizo ni Karago, Mtendeli, Kanembwa na Nduta zilizokuwa wilayani Kibondo, na Muyovosi iliyokuwa wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.

Kambi nyingine zilizofungwa ni Kitali iliyokuwa wilayani Biharamulo, Lukole A na B zilizokuwa wilayani Ngara, mkoani Kigoma.Kambi ya wakimbizi ya Mtabila ndiyo itakuwa ya mwisho kufungwa katika mlolongo wa kambi zilizokuwa zikihifadhi wakimbizi kutoka Burundi hapa nchini.

Imetolewa na Isaac J. Nantanga:
MSEMAJI WA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

No comments: