Thursday, May 23, 2013

RASLIMALI ZA NCHI NI MALI YA TAIFA ZIMA....WALIOANDAMANA HUKO MTWARA TUTAWASHITAKI'... RAIS KIKWETE

                                                    Polisi wawasaka waandamanaji Mtwara
Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewaonya watu wanaosababisha uvunjifu wa amani nchini humo kuwa watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Onyo hilo linafuatia ghasia ambapo ofisi kadha, maduka na nyumba zimechomwa katika mkoa wa Mtwara ulioko kusini mashariki mwa Tanzania jana

Akihutubia kupitia televisheni ya taifa, TBC1, Rais Kikwete amesema wale waliokamatwa na polisi wakati wa ghasia hizo watashitakiwa.

Ghasia hizo zilianza muda mfupi baada ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kuwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni. Akizungumzia madai ya waandamanaji hao, Rais Kikwete amesisitiza kuwa raslimali za nchi ni mali ya taifa zima.


Amesema mkoa wa Mtwara haujatelekezwa na kusema kwamba kuna mipango ya kutumia gesi hiyo kujenga viwanda vya mbolea na kutumia gesi hiyo asilia kuzalisha nishati ya umeme kwa mikoa ya Mtwara, Lindi, na Ruvuma ili kuunganishwa katika gridi ya taifa.

Ofisi zachomwa

Kwa mujibu wa mkuu wa polisi wa mkoa wa Mtwara kamanda Linus Sinzumwa, vurugu hizo zilitokea jana asubuhi mara baada ya Wizara ya Madini na Nishati kusoma bajeti yake ya makadirio ya mapato na matumizi huko Bungeni mjini Dodoma na kusababisha uharibifu wa mali.

Ametaja uharibifu huo kuwa ni pamoja na kuchomwa kwa majengo ya serikali kama mahakama, nyumba za watendaji wa serikali, baadhi ya majengo ya chama tawala na nyumba za watu binafsi.

Hata hivyo, kamanda huyo, amekanusha taarifa za kuuawa kwa mtu mmoja katika eneo hilo na kubomolewa kwa daraja linalounganisha mji wa Mtwara na maeneo mengine.

Kamanda Sinzumwa amesema watu wapatao tisini na mmoja wanashikiliwa na jeshi na polisi kuhusiana na matukio mbalimbali ya ghasia hizo.

Ghasia hizo, zinahusishwa na madai ya muda mrefu sasa ya wananchi wa mkoa huo kupinga ujenzi wa bomba la gesi iliyogunduliwa mkoani humo kusafirishwa hadi Dar es Salaam, kaskazini mwa Mkoa wa Mtwara, kwa ajili ya kuzalisha nishati ya umeme.

Hii ni mara ya pili mkoani Mtwara kutokea kwa ghasia zinazohusisha maafa kwa binadamu na uharibifu wa mali kama ilivyotokea mapema mwaka huu.

 BBC

No comments: