Mwanafunzi, Fikiri Mtasimwa (20) akiwa wodini kwenye Hospitali ya Mkoa wa Geita alikolazwa akitibu majeraha baada ya kukatwa mapanga.
Kiganja cha Fikiri Mtasimwa kilichokatwa kwa panga.
Mwanadada Machiwa Ramadhan (21) akiwa amelazwa katika Kituo cha Afya cha Miono baada ya kujeruhiwa katika fumanizi.
WIKI iliyopita watu wa familia mbili tofauti walijikuta wakijiingiza katika matatizo makubwa baada ya kutokea walichodai fumanizi ambapo binti mmoja na mwanaume walijikuta wakijeruhiwa baada ya kukatwa na wanaodai waliowafumania.
Waliopata majeraha ni mvulana wa Geita na msichana wa Miono, Bagamoyo.
BINTI MIAKA 21
Tukio la kwanza lilimpata binti wa miaka 21, Machiwa Ramadhan mkazi wa Kijiji cha Mandela, Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani ambaye sasa amelazwa katika Kituo cha Afya cha Miono baada ya kujeruhiwa katika fumanizi.
Vyanzo vyetu vya habari vilidai kwamba mwanadada huyo alijeruhiwa Alhamisi ya wiki iliyopita saa 3.00 usiku kwa baba yake mdogo aliyetambulika kwa jina la Mwinyijuma Paulo baada ya kukutwa na mume wa mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la mama Hema wakiwa gizani huku wakizungumza kwa sauti za kimahaba.
Habari zaidi zilidai kwamba mwanaume huyo aliyejulikana kwa jina la Walter Emili maarufu kwa jina la Kojoka aliyekutwa na Machiwa, baada ya kufumwa alitimua mbio huku mwanamke huyo akishambuliwa hadi kupasuliwa shavuni na kitu chenye ncha kali na kushonwa nyuzi 12 katika Kituo cha Afya cha Miono.
Taarifa hizo ziliendelea kudai kwamba mke wa Emili alipata taarifa kwa marafiki zake kwamba Machiwa yupo na mumewe hivyo aliwafuma wakiwa pamoja ndipo alipoamua kumpiga mgoni wake.
Mwandishi wa habari hii alienda hadi Kituo cha Afya Miono na kumkuta Machiwa akiwa amelazwa na alipoulizwa kulikoni, alisema kuwa amejeruhiwa na mama Hema.
Machiwa alikataa katakata kwamba alifumaniwa na huyo mwanaume akadai kuwa huyo mwanamke alimvamia njiani wakati akitoka katika biashara zake karibu na nyumbani kwa baba yake mdogo.
“Aliponijeruhi niliamua kwenda kwa dada yangu aitwaye Tatu Ramadhan ambaye alinipeleka kwa mwenyekiti wao wa Kitongoji cha Chemichemi na akatuandikia barua ya kwenda Kituo cha Polisi Wami tulikopata PF 3 kwa ajili ya kutibiwa,” alisema.
Aliendelea kusema kwamba alifika katika Kituo cha Afya Miono akashonwa nyuzi 12 na hadi sasa bado amelazwa.
Kwa upande wake Paulo ambaye ni baba mdogo wa Machiwa alipoulizwa juu ya tukio hilo alisema kwamba yeye ni kipofu bali alikuja kupata taarifa za tukio hilo baadaye.
Mama Hema ambaye ni mtuhumiwa hakupatikana kwa kile kilichoelezwa kuwa bado anashikiliwa na polisi kutokana na hali ya Machiwa kuwa mbaya huku mumewe akiwa hajulikani alipo.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mandela, Andrew Semiono alipoulizwa na gazeti hili kuhusu tukio hilo, alisema uchunguzi unaonesha kuwa fumanizi hilo lina mazingira ya ukweli kutokana na kwamba hata Machiwa alipokuwa anashambuliwa hakupiga kelele kuhitaji msaada.
Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Mandela, Wema Ali Nzenzi alikiri kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa wivu wa kimapenzi umesababisha yote hayo na kwamba mama Hema alikuwa akimtafuta mgoni wake siku nyingi.
“Siku hiyo mama Hema aliposikia kuwa mumewe yupo na Machiwa alichukua tochi na kuwavizia hatimaye kuwafumania na kufanya alichofanya,” alisema Nzenzi.
MWANAUME AKATWA MKONO
Naye Victor Bariety wa Geita anaripoti kuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Nyakamwaga wilayani hapa, amenusurika kifo baada ya kudaiwa kufumaniwa na mke wa mtu japokuwa mwenyewe amekanusha.
Kijana huyo alijeruhiwa kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na kukatwa kiganja cha mkono wa kushoto na mwanaume mmoja aliyedai kuwa anatembea na mke wake na siku ya tukio alionekana akiwa na mke wa mwanaume huyo.
Akisimulia mkasa huo akiwa wodini kwenye Hospitali ya Mkoa wa Geita alikolazwa akitibu majeraha, mwanafunzi huyo Fikiri Mtasimwa (20), mkazi wa Kijiji cha Gengetano, Kata ya Nyakamwaga mkoani hapa alidai kuwa alikutwa na balaa hilo usiku wa Juni 17, mwaka huu wakati akinywa uji kwenye kijiwe chao.
Alidai mwanaume huyo anayemfahamu kwa jina la baba Neema alimvamia kwenye kijiwe hicho kinachomilikiwa na binti aliyemtaja kwa jina moja la Mektirida na kuanza kumshambulia kwa mapanga sehemu za kichwani, mgongoni na begani kabla ya kumkata mapanga katika mkono wake wa kushoto na kusababisha kiganja cha mkono huo kunyofoka akimtuhumu kutembea na mkewe aliyemtaja kwa jina la mama Neema.
“Wakati nakunywa uji nilimuona baba Neema akichomoa panga kiunoni mwake na kuanza kunikata kwa kunilenga shingoni, nilikwepa lakini bahati mbaya lilitua kisogoni na kunijeruhi ndipo nilipoamua kukimbia lakini sikufika mbali kwani nilidondoka, akanifuata na kunikata panga jingine la pili kichwani.
“Nilinyanyuka tena na kukimbia huku damu zikivuja...nikadondoka tena, akanikata begani.
“Inavyoonekana alikuwa na lengo la kuniua kwani alianza kunikata mkono wangu wa kushoto mara kadhaa na kiganja changu kikadondoka ndipo rafiki yangu aitwaye Fikiri William ninayesoma naye kidato cha tatu, alipofika kunisaidia na njemba hilo likatoweka na kwenda kusikojulikana nami nikapoteza fahamu,” alisema Mtasimwa.
Alisema alijikuta yupo hospitali akiwa hana kiganja na kufafanua:
“Siku moja kabla ya tukio nilikutana na baba Neema na kumsalimia lakini akaniambia kuwa mimi nina dharau sana wala hahitaji salamu yangu na akanitishia kuwa maisha yangu yapo hatarini, aliondoka bila kunieleza sababu.”
MGANGA MKUU
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Ndallo Ndallo alithibitisha kuwepo kwa majeruhi huyo katika hospitali hiyo na kuongeza kuwa hali yake ni mbaya kutokana na majeraha aliyoyapata sehemu mbalimbali za mwili.
KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Kamishna Msaidizi wa Polisi, Leonard Paulo alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kuongeza kuwa juhudi za kumsaka mtuhumiwa huyo zinaendelea. Picha Hisani Ya Global Publishers.
No comments:
Post a Comment