Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoundwa na wabunge wa Chadema, Freeman Mbowe amedai kuwa ugomvi ndani ya Bunge unatokana na meza ya Spika pamoja na wasaidizi wake kuwaonea wabunge wa upinzani na kuwapendelea wabunge wa CCM.
Mbowe, ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema, alitoa hoja hiyo jana ndani ya Bunge wakati akichangia hotuba ya Bajeti ya Serikali na pia alisisitiza suala hilo wakati alipofanya mkutano na waandishi wa habari.
Wakati anatoa hoja hiyo bungeni, Spika wa Bunge Anne Makinda alimjibu kuwa yeye pamoja na wasaidizi wake ambao ni Naibu Spika na wenyeviti watatu wa Bunge hilo wanatimiza majukumu yao kwa kuzingatia kanuni namba nane ya Bunge.
“Kuna mkakati wa makusudi wa kuwalinda wabunge wa CCM hata pale wanapovunja kanuni za Bunge na wanapowadhalilisha wabunge wa Chadema, na sisi tunapojibu kwa nguvu ile ile, meza ya Spika wanakuwa wakali kuchukua hatua,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema hatua hiyo inawafanya wabunge wa upinzani wawe na hasira kwani hata pale wanapoomba mwongozo inamchukua muda mrefu kwa Spika au wasaidizi wake kuwaruhusu kufanya hivyo.
“Meza yako Spika ikiyumba pamoja na wasaidizi wako na ikikubali kuubeba upande mmoja na kuchukua hatua kali upande mwingine, ni wazi kuwa hapo hakuwezi kuwepo amani,” alisema Mbowe.
Alitoa mfano Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba (CCM) akidai alitoa dhihaka juu ya maoni ya Kambi ya Upinzani ya Bajeti hadi akaitupa lakini hakuna hatua zilizochukuliwa na kiti cha Spika.
No comments:
Post a Comment