Saturday, July 28, 2012

Bunge Lanuka Rushwa(Fedha za mafisadi zawatokea puani wabunge)

BUNGE jana liliwaka moto baada ya baadhi ya wabunge kuwanyooshea vidole wenzao kwa madai kupokea rushwa kwa lengo la kuwapigia debe mafisadi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wanaowafilisi Watanzania.

Wabunge hao wanadaiwa kuwaunga mkono mafisadi ili Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, na Katibu Mkuu wake, Eliakimu Maswi, waonekane hawafai.

Akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti kwa wizara hiyo jana, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA), alisema kwa wiki nzima waziri na watendaji wake walikuwa wakidhalilishwa na baadhi ya watu kwa kupitia wabunge wakitaka Rais Jakaya Kikwete awaondoe kwa madai kuwa walikiuka sheria ya manunuzi ya umma na kuipa zabuni kampuni ya PUMA Energy.

“Mheshimiwa mwenyekiti baadhi ya makampuni ya mafuta yalikuwa hapa Dodoma na kutoa chochote kwa wabunge na hili si kwa upande wa serikali ya CCM bali wabunge wa pande zote tukiwemo wapinzani. Msione watu wanazungumza kwa nguvu hapa kutetea, hawa wamepewa chochote,” alisema.

Huku akishangiliwa na karibu wabunge wote, Selasiani alisema wanaohoji kuwepo ukiukwaji wa sheria ya manunuzi ya umma anawashangaa kwani katika jambo la msingi lazima uamuzi uwe mgumu huku akitolea mfano wa Yesu Kristo alivyoivunja Sabato aliyoiweka mwenyewe.

“Mheshimiwa mwenyekiti Maswi ametishwa tunajua hilo, ametumiwa meseji za vitisho, ameombwa rushwa na baadhi ya wabunge wenzetu hapa. Tunawajua wako wabunge wanafanya biashara na TANESCO, lakini humu waongea kwa nguvu na jazba wakijifanya watetezi wa wananchi kumbe ni nguvu ya rushwa,” alisema.

Selasini alimtadharisha Waziri Muhongo kuwa yeye ni msomi asiyetokana na siasa hivyo hawajui wanasiasa lakini ni vema afanye kazi kwa nguvu bila kutetereka na atawazoea.

Mbunge huyo pia alipendekeza sheria ya wahujumu uchumi irejeshwe ili wahusika wakiwemo wabunge waliohusika katika sakata hilo wahukumiwe kama wahaini.

“Wako wenzetu humu wamekuwa wakijifanya wapambanaji wanaongea kwa nguvu kuhusu ufisadi lakini leo wamekuwa madalali wa mafisadi na hawa wako kote CCM na huku kwetu wapinzani,” alisema.

Selasini alizungumza baada ya kutanguliwa na wabunge wenzake, Anne Killango Malecela wa Same Mashariki na Christopher Ole Sendeka wa Simanjiro (CCM), ambao walionekana kupishana katika kuwaunga mkono waziri na watendaji wake. soma zaidi http://freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=38649

No comments: