Tuesday, July 31, 2012

Serikali Yahaha Kuzima Mgomo Wa Walimu

Mwanafunzi akipakizwa katika gari la Polisi baada kwenye kuvunjwa maandamano ya kuelekea kwa Mkuu wa Wilaya Kindononi kwa Wanafunzi kutoka shule za Msingi za Mtongani,Kunduchi,Mtakuja na Wazo kushinikiza walimu warudi kazini baada ya kusambaratishwa na Polisi katika eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam.Picha na Fidelis Felix


POLISI WAWATIA MBARONI VIONGOZI CWT, FFU WADHIBITI  WANAFUNZI DAR, TUCTA YAUNGA MKONO MGOMO

Waandishi Wetu
SERIKALI imelazimika kutumia Jeshi la Polisi katika harakati zake za kudhibiti mgomo wa walimu ambao jana uliingia katika siku yake ya pili, huku maandamano ya wanafunzi yakiendelea katika baadhi ya maeneo na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kulazimika kuwadhibiti.

Taarifa kutoka mikoa kadhaa zinaonyesha kuwa polisi waliwakamata viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), ngazi za mikoa na wilaya, huku baadhi yao wakifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuchochea mgomo ambao Serikali tayari imesema kuwa ni haramu.

Kukamatwa kwa viongozi hao kulikwenda sambamba na tamko la baadhi ya wakuu wa mikoa na baadhi ya makamanda wa polisi ambao walionya kwamba wangewachukulia hatua za kisheria walimu ambao wangeendelea kugoma.

Wakati Serikali ikichukua hatua hiyo, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limeitaka Serikali kuacha kujitetea katika suala hilo na kulipa madai ya wanataaluma hao wa sekta ya elimu.

Mkoani Dar es Salaam, FFU walitawanya maandamano ya wanafunzi katika eneo la Kunduchi, Kinondoni na kuwakamata baadhi yao. Waliandamana kwa madai ya kudai haki yao ya kufundishwa.
Kundi kubwa la wanafunzi waliodaiwa kwamba walikuwa wakitoka katika shule mbalimbali za Manispaa ya Kinondoni waliandamana katika maeneo ya Mbezi Machimbo, huku askari wa FFU wakijaribu kuwazuia na kuwaelekeza kurudi nyumbani.

Mmoja wa wanafunzi hao, Jamila Dadi alisema walimu wao wanaendelea kukusanya fedha za mafunzo ya ziada bila ya kuwafundisha, hivyo wameamua kuandamana ili kudai haki yao.

“Walimu wanakuja kila siku asubuhi wanachukua Sh200 kwa kila mwanafunzi, halafu wanaondoka bila kutufundisha ndiyo maana tumeamua kuandamana ili kudai haki yetu,” alisema Jamila.
Wanafunzi walioshiriki kwenye maandamano hayo wanatoka kwenye Shule za Msingi Wazo, Mtakuja, Mtongani, Kunduchi, Bwawani na Jangwani.

Wilayani Ilala, wanafunzi wa Shule ya Msingi Tabata walisababisha msongamano barabarani baada ya kuandamana kwa lengo la kwenda kwa Mkuu wa Mkoa ili awasaidie kuwarudisha walimu kazini ambao wapo kwenye mgomo.

Wanafunzi hao ambao walijikusanya asubuhi baada ya kufika shuleni hapo, walichukua uamuzi huo kutokana na kutosoma tangu juzi. Hata hivyo, waliishia Kituo cha Polisi cha Buguruni baada ya Mkuu wa Kituo, Inspekta Batseba  Kasanga kuwarejesha shuleni.

Mkoa wa Mbeya
Polisi mkoani Mbeya waliwakamata walimu wanne, Katibu wa CWT Wilaya ya Kyela, Petro Mangula (52) na Akso Kibona (52) ambaye ni Katibu wa chama hicho Wilaya ya Rungwe kwa tuhuma za kupita katika shule za msingi na sekondari kuhamasisha walimu waliokuwa wakiendelea na kazi washiriki mgomo.

Wengine waliokamatwa ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Mbebe wilayani, Ileje Emmanuel Kyejo (45) na Mwalimu wa Shule ya Msingi Mkumbukwa, Anyangigwe Lwingwa (54).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Athuman Diwani alisema kukamatwa kwa walimu hao kulitokana na taarifa za siri ambazo polisi walizipata kwamba walikuwa wakipita katika shule na kuwatishia walimu waliokuwa wakiendelea na kazi.

Diwani alisema watuhumiwa wote walifikishwa mahakamani jana katika mahakama za wilaya kujibu tuhuma zinazowakabili.

Alisema polisi pia inawashikilia watu tisa kwa tuhuma za  kufanya vurugu na kuvamia ofisi ya Mkurugenzi wa Mji mdogo wa Tunduma  na kuchoma nyaraka na  kupora mali mbalimbali  zenye thamani ya zaidi ya Sh117.515 milioni.

Vurugu hizo ni zile zilizotokea juzi saa 5.30 za asubuhi wakati wahalifu walipojichanganya katika maandamano ya wanafunzi waliokuwa wakipinga mgomo wa walimu.
Naye  Diwani wa Kata ya Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema) jana aliitisha mkutano wa hadhara ili kuzungumzia suala hilo na kulaani vikali vitendo vya uporaji  vilivyofanywa kwa mwamvuli wa maandamano ya wanafunzi.

Mwanza na Mara
Katika Mkoa wa Mwanza, Katibu wa CWT mkoani humo, Isaack Mashahushi alilalamika kwamba polisi wamekuwa wakiwakatama walimu kwa madai kwamba mgomo wao ni batili.
Mashahushi alisema wamepokea taarifa za kukamatwa kwa walimu watatu katika baadhi ya maeneo mkoani humo na kwamba ofisi yake ilikuwa ikiendelea kufanya mawasiliano zaidi ili kubaini kama wapo wengine waliokamatwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow alikataa kuzungumzia suala hilo, lakini akasema jeshi lake limejipanga kuhakikisha hakutokei vurugu.
Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya wanamshikilia Mwalimu wa Shule ya Msingi Rebu, wilayani Tarime, Esther Kasika (40) kwa mahojiano baada ya kudaiwa kuhusika kuchochea watoto kufanya maandamano.

Kamanda wa Polisi katika mkoa huo, Justaus Kamugisha alisema mwalimu huyo anatuhumiwa kuwachochea wanafunzi wa Shule ya Msingi Rebu walioandamana juzi kwenda Ofisi Mkuu wa Wilaya Tarime kudai haki yao ya kusoma.
Kamugisha aliwataka walimu wote wanaotaka kufundisha kufanya kazi zao na endapo yeyote ataonekana kuwatishia, au kuharibu mali wanapaswa kutoa taarifa mara moja.

Tucta wang’aka
Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholas Mgaya amesema Serikali inapaswa kutafuta ufumbuzi wa mgomo huo kwani unaathiri maendeleo ya wanafunzi.
Mgaya alisema Serikali haipaswi kujitetea katika suala hilo kwani walimu wana madai ya msingi ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuwawezesha kufanya kazi yao vizuri bila malalamiko ya mara kwa mara.

“Tunaitaka Serikali kulichukulia suala hili kwa uzito wa hali ya juu, kwani walimu wana madai ya msingi ambayo yanatakiwa kutekelezwa haraka. Kama haitakubali kulipa madai ya walimu, basi mgomo huo utawaathiri kwa kiasi kikubwa wanafunzi hasa darasa la saba na kwamba hata walimu hawatakuwa na moyo wa kufundisha vizuri,” alisema.

Mgaya alisema walimu wana haki ya kugoma na wanastahili kupewa haki zao kutokana na mazingira magumu wanayofanyia kazi, hasa ukizingatia hali ya maisha ilivyo wakati huu.

“Walimu wanafanya kazi katika mazingira magumu, sasa iweje wanapodai haki zao kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi mwajiri ambaye ni Serikali anajitetea kwa kutoa visingizio jambo ambalo haliwezi kukubalika. Tucta inaunga mkono mgomo huo kwa asilimia 100 kwani ni haki yao kufanya hivyo mpaka watakapopata stahili zao za msingi  wanazodai.”
Alisema mgomo huo ambao ulianza juzi umeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya elimu, jambo ambalo si jema kwa maendeleo ya nchi.

“Kwa siku moja tumeshuhudia mgomo huo ukiathiri sehemu mbalimbali za nchi sasa Serikali inapaswa kuliangalia hilo kwa kufikia makubaliano na walimu ikiwa ni pamoja na kulipa madai wanayoyataka,” alisema. SSoma zaidi; http://www.mwananchi.co.tz

No comments: