TIMU ya Simba inatarajia kucheza mechi dhidi ya timu ya soka ya NAIROBI CITY STARS siku ya Jumapili ijayo katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta jijini Arusha.
Timu hiyo kutoka Kenya ndiyo iliyocheza na Simba jijini Dar es Salaam katika tamasha la Simba Day.
Awali Simba ilikuwa imepanga kucheza mjini Tanga WIKIENDI HII lakini kutokana na mabadiliko ya programu ya mazoezi ya benchi la Ufundi, Wekundu wa Msimbazi sasa watabaki Arusha hadi Septemba nne mwaka huu ili kukamilisha programu yote bila ya usumbufu.
Hali ya kikosi cha Simba ni ya utulivu kabisa na mazoezi yanafanyika kwa mchanganyiko wa mazoezi ya uwanjani na GYM.
Hakuna majeruhi yoyote hadi sasa na wachezaji wote wanafanya mazoezi kama kawaida.
Juma Kaseja
Kwenye mechi mbili za kirafiki zilizopita jijini Arusha, mlinda mlango namba moja wa Simba, Juma Kaseja, hakudaka na badala yake waliodaka ni Wilbert Mweta na Waziri Hamadi Mwinyiamani.
Kudaka kwa makipa hao ni mipango tu ya mwalimu na Kaseja hana maumivu yoyote na anafanya mazoezi kwa nguvu sana kujiandaa na msimu ujao.
Kama ilivyo ada, Kaseja atadaka siku ambayo mwalimu ataamua akae langoni
Felix Sunzu
Kuna baadhi ya vyombo vya habari vimeanza kuandika vichwa vya habari vyenye lengo la kuuza magazeti kutokana na kufiwa kwa mchezaji wetu huyu.
Simba SC inapenda kutumia nafasi hii kuviomba vyombo vya habari na wadau wengine kumuacha mchezaji huyu aomboleze msiba huu na siku yake ya kurudi itakapofika, klabu itatangaza.
Mussa Mudde
Simba SC inafahamu kiu ya vyombo vya habari kuhusiana na kutaka kujua masuala ya usajili wa wachezaji wake wa kigeni. Ukweli ni kwamba taarifa yoyote itakayotoka leo au kesho itakuwa haijaiva bado na klabu isingependa kutoa taarifa ambazo hazijaiva bado.
Tutatoa taarifa rasmi na kamili wakati mchakato mzima utakapokuwa umekamilika. Kwa hiyo, Simba haitatoa tamko lolote kwa sasa kuhusu usajili wa wachezaji wake wa kigeni hadi kila kitu kikamilike.
Tunaahidi kwamba hilo litafanyika haraka iwezekanavyo ili kiu yenu itimizwe.
Tunatanguliza shukrani
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC
30/08/2012
No comments:
Post a Comment