Platini anasema huenda ikawa bora michuano ya Euro 2020 kufanyika katika miji mbalimbali ya Ulaya
Michel Platini, rais wa shirikisho la soka barani Ulaya, UEFA, amesema michuano ya Euro 2020 huenda ikafanyika katika miji mbalimbali mwaka 2020, badala ya kuwa na mji mmoja ambao utakuwa ni mwenyeji.
Utamaduni wa mashindano hayo huwa ni nchi moja, au mbili, kushirikiana katika kuwa mwenyeji, kama ilivyo wakati huu michuano hiyo kufanyika Poland na Ukraine.
Mashindano yajayo yatafanyika nchini Ufaransa, mwaka 2016.
"Euro 2020 inaweza kufanyika popote barani Ulaya," alielezea Platini. "Yanaweza kufanyika katika nchi moja yenye viwanja 12, au kufanyika katika uwanja mmoja katika miji 12 au 13 ya Ulaya."
Platini ameelezea kwamba wazo hilo pia linaweza kuokoa senti katika kuepuka gharama kubwa za ukarabati, na juhudi za kujenga viwanja vipya na kuimarisha viwanja vya ndege.
Uturuki ilitazamiwa na wengi kupata nafasi ya kuandaa mashindano ya mwaka 2020, lakini ombi la nchi hiyo limekumbwa na tatizo, kwa kuwa nchi hiyo pia ina nia ya kuandaa michezo ya Olimpiki mjini Istanbul, mwaka huohuo wa 2020.
Mataifa ya Uskochi, Wales na Jamhuri ya Ireland, rasmi pia yameelezea nia yao ya kuandaa michuano ya 2020.
Platini ametangaza kwamba uamuzi kamili utatangazwa kati ya mwezi Januari hadi Februari mwaka ujao.
Chanzo:BBC
No comments:
Post a Comment