Basi lililokuwa limewabeba raia wa Kenya waliokuwa wakielekea jijini Dar
es salaam kwa ajili ya mikutano ya injili likiwa limetumbukia katika
korongo jirani na Mto Wami na kuua watu 11 katika Kijiji cha Makole Mkoa
wa Pwani.
Baadhi ya abiria walionusurika wakiwa katika eneo la tukio kabla ya kupata msaada.
WATU 11 wanaoaminika kuwa raia wa Kenya wamefariki dunia papo hapo, huku wengine saba wakiwa mahututi baada ya mabasi waliyokuwa wakisafiria kutoka Nairobi kwenda Dar es Salaam kupata ajali katika Mto Wami mkoani Pwani.Mbali na vifo hivyo, ajali hiyo pia ilisababisha majeruhi 25 na saba kati yao waliripotiwa kuwa mahututi na walipelekwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha kwa matibabu.
Ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Makole, wilayani Bagamoyo wakati abiria hao ambao ni wanakwaya walipokuwa wakisafiri kutoka Kenya kwenda Dar es Salaam kushiriki katika tamasha la uimbaji.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 11 alfajiri ikihusisha magari manne, mawili kati yake yakiwa ni mabasi hayo yakitokea Kenya na malori mawili ya hapa nchini.Tukio hilo pia lilifunga Barabara Kuu ya Chalinze - Segera kwa zaidi ya saa nane hivyo abiria waliokuwa wakisafiri kuelekea na kutoka mikoa ya Kaskazini ikiwamo nchi ya Kenya kwenda na kutoka Dar es Salaam kukwama.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu alisema raia hao wa Kenya ni waumini wa Kikristo na walikuwa wakielekea Dar es Salaam kwenye tamasha la kwaya.
Ajali ilivyotokea
Mangu alisema awali, mabasi hayo yalikuwa yametokea Segera, huku yakiwa yameongozana na moja ilipofika eneo la Makole ghafla liliyumba na kupinduka kisha kutumbukia kwenye korongo.Alisema basi la pili lililokuwa likifuatia nyuma lilipita eneo hilo, lakini baada ya mita 500, dereva alipigiwa simu na mwenzake kuwa amepata ajali na wametumbukia korongoni hivyo ikawalazimu kugeuza kurudi nyuma ili wakawasaidie wenzao.
“Haikuwa rahisi kwa mtu ama gari kuliona haraka hivyo wenzao walipofika hapo nao walipita bila kujua kama kuna gari limeanguka, lakini muda mfupi tu dereva alipigiwa simu na mwenzake akimjulisha kuwa amepata ajali na wametumbukia mtaroni,” alisema Kamanda Mangu.
Alisema baada ya kugeuza na kurudi eneo la ajali, baadhi ya abiria walishuka ili kuwasaidia wenzao na wakati wakiwa kwenye harakati hizo, ghafla lilitokea lori ambalo lililiparamia basi la pili ambalo pia lilitumbukia kwenye korongo.Kamanda huyo aliongeza kuwa, wakati basi hilo likigongwa, tayari lilikuwa limegeuzwa kuangalia uelekeo wa Chalinze na kwamba baadhi ya abiria walikuwamo ndani.
Alisema baada ya lori hilo kuligonga basi hilo, liliendelea mbele kwa kasi na kugongana uso kwa uso na lori jingine lililokuwa likitokea uelekeo wa Segera, hivyo kufunga barabara hiyo kwa zaidi ya nane.“Kwa hiyo njia ilikuwa imefungwa kuanzia saa 11:00 alfajiri hadi saa 6:30 mchana baada ya askari wetu kufanikiwa kuyaondoa malori hayo kwenye barabara kuu na sasa (jana) safari zinaendelea kama kawaida,” alisema Mangu.
Majeruhi
Baadhi ya majeruhi walitibiwa katika Zahanati ya Chalinze na baadaye kuhamishiwa katika Hospitali ya Tumbi.Hata hivyo, RPC Mangu alisema baadaye majeruhi na miili ya marehemu wote walihamishwa na kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na maombi ya Ubalozi wa Kenya nchini.
Habari zilizopatikana jana jioni zinasema kuwa Serikali ya Kenya kupitia ubalozi wake hapa nchini ilikuwa ikifanya mipango ya kuwarejesha nyumbani majeruhi na baadaye maiti kwa ajili ya mazishi.
Ajali hiyo ni kati ya saba ambazo kwa mujibu wa Mangu zilizotokea usiku wa kuamkia jana na baadhi yake zilisababisha majeruhi zaidi ya 20 katika maeneo ya Msata, Chalinze na Mbala, wilayani Bagamoyo.
Kutoka Morogoro; watu 45 wamenusurika kufa kwa ajali baada ya mabasi matatu waliyokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka eneo la Mkundi kwa Makunganya nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro, katika Barabara ya Morogoro - Dodoma.
Ajali hiyo ilitokea saa 2:30 asubuhi kwa kuhusisha mabasi matatu, Kampuni ya Shabiby lililokuwa likitokea Dodoma kwenda Dar es Salaam, Allys Sport na Sumry yaliyokuwa yakitokea Morogoro kwenda Mwanza.
Baadhi ya majeruhi waliokuwa wakisafiri na basi la Shabiby walisema basi hilo lilianza kuyumba na baadaye kuacha njia kisha kupinduka.Mmoja wa abiria hao, Rashid Shaaban alisema baada ya basi hilo kupinduka, ghafla waliona basi jingine la Sumry likiacha njia na kupinduka wakati lilipojaribu kulipita gari jingine jirani na eneo hilo.Alisema kuwa wakati kukiwa na msongamano wa magari katika eneo hilo la ajali, basi jingine la Allys Sport liliacha njia na kupinduka na hivyo kutokea ajali tatu katika muda usiozidi dakika 10.
Shaaban alisema baada ya ajali hizo walitokea watu waliokuwa wakijifanya kutaka kutoa msaada, lakini lengo lao lilikuwa ni kuiba mali za majeruhi. Hata hivyo, alisema lengo lao hilo halikufanikiwa kwani muda mfupi baada ya kutokea, askari walifika na kuimarisha ulinzi.
Katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, madaktari na wauguzi walionekana kuzidiwa na wagonjwa kutokana na idadi kubwa ya majeruhi waliokuwa wakihitaji huduma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alithibitisha kutokea kwa ajali hizo na kusema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa zimetokana na utelezi na mwendo kasi. Hata hivyo, alisema kuwa uchunguzi unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwahoji madereva wa mabasi hayo.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment