Siku chache kabla ya kifo chake askari polisi mwenye namba F 3276, Donald Mathew (33), aliyejinyonga juu ya mti katika daraja la Shani, mkoani Morogoro alimwandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani kueleza kinachodaiwa kuwa ni ufisadi unaofanywa na vigogo wa polisi nchini, imebainika.
Polisi huyo aliyefahamika sana kwa jina la Dunga aliwahi kutoa tuhuma nzito dhidi ya maofisa, wakaguzi na polisi wa kawaida, mkoani Morogoro mwaka jana lakini hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya maofisa hao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fustine Shilogile, jana alisema jeshi hilo, lilipokea taarifa za kujinyonga Mathew jana asubuhi.
Alisema askari huyo, aijinyonga kwa kutumia vipande vya kamba ya kanga ambavyo viliunganishwa na hakuacha ujumbe wowote unaoeleza sababu ya kuchukua uwamuzi huo.
Alisema askari huyo kabla ya kufanya tukio hilo, alionekana mitaani akinywa pombe katika Baa ya Shani.
Alisema baada ya kuonekana amelewa, Mathew aliamua kuvua nguo zote na kubaki mtupu, kitendo kilichofanya baadhi ya askari polisi waliokuwa eneo hilo, kumfuata na kumsihi avae nguo.
Alisema marehemu, alihamishiwa mkoani Singida kikazi, lakini Novemba, mwaka jana aliamua kuacha jeshi.
“Pamoja na kwamba marehemu aliacha kazi mwaka jana, sisi kama jeshi bado tunamtambua kama askari mwenzetu… kwa msingi huo tutasafirisha mwili wake Agosti 8, mwaka huu kwenda nyumbani kwake mkoani Kilimanjaro,” alisema Kamanda Shilogile.
Alipoulizwa kama kifo cha Mathew kimesababishwa na baadhi ya askari waliohusishwa kwenye tuhuma za kuhusika na biashara za dawa za kulevya, Kamanda Shilogile alisema uchunguzi unaendelea, na kwamba ikibainika kama kuna askari aliyehusika atachukuliwa hatua kali.
Hata hivyo, askari huyo mwishoni mwa mwaka jana, alitoa tuhuma mbalimbali ambazo zilichapishwa katika moja ya magazeti linalotoka mara mbili kwa wiki, zikiwatuhumu askari 9 wa kikosi cha kupambana na majambazi wa kutumia silaha kupokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Tuhuma nyingine alizotoa ni polisi kukamata majambazi wenye silaha, lakini huachiwa baada ya kupewa fedha na mali mbalimbali, hivyo kushindwa kuwafikisha kituoni.
Alisema tuhuma nyingine ni polisi kuwakamata wafanyabiashara wa pombe haramu aina ya gongo na bangi bila kuwachukulia hatua zozote baada ya kuhongwa.
Tuhuma nyingine, zinazodaiwa kufanywa na askari hao ni kushirikiana na matapeli, kutapeli raia wa kigeni na kushirikiana na majambazi kuvunja maduka na kuiba mali za wafanyabiashara nyakati za usiku
No comments:
Post a Comment