Wednesday, August 15, 2012
Polisi: Tuko Tayari Kumlinda Ulimboka
HOFU YATANDA NYUMBANI KWAKE, MILANGO YATIWA KUFULI
JESHI la Polisi limesema liko tayari kumlinda kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka iwapo atahitaji ulinzi huo.Kauli hiyo imekuja siku mbili tangu daktari huyo wa magonjwa ya binadamu arejee nchini, huku usiri ukiwa umetawala taarifa zake kutokana na kutokuwapo kwa ndugu, jamaa au rafiki aliyekuwa tayari kusema chochote kumhusu.
“Nitachoweza kusema ni kwamba nashukuru mwanangu amerejea salama, lakini siwezi kusema chochote kuhusu mambo yanayomuhusu yeye,” alisema baba mzazi wa Dk Ulimboka, Mzee Mwaitenda.
Tofauti na juzi ambapo nyumbani kwake kulikuwa na watu kadhaa akiwamo Mweitenda, jana mageti yote ya nyumba hiyo iliyoko eneo la Kibangu, Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, yalifungwa na hapakuwa na mtu yeyote ndani.
Katikati ya hofu hiyo ya usalama, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema Jeshi lake haliwezi kutoa ulinzi kwa Dk Ulimboka bila yeye mwenyewe kuomba.
"Kwanza walishaamua (madaktari) kuchagua ulinzi, sisi tufanyeje? Atakapoona kuna ulazima atatujulisha," alisema Kenyela na kuongeza;
"Hatuwezi kupeleka askari bila kuombwa. Ukipeleka halafu akasema hawahitaji, itakuwa embarrasing (fedheha) sana. Sisi tunajua amerudi na tunamtakia heri aendelee vizuri, apone na aungane na wenzake,"
Kamanda Kenyela alifafanua kuwa nyumbani kwa mtu ni eneo la faragha ambalo polisi hawawezi kwenda bila kuombwa na kufanya hivyo, ni kitu kisichokubalika.
"Mimi kama kamanda sijapokea ombi lolote kutoka kwa Ulimboka wala kusikia tishio lolote dhidi ya usalama wake. Akiona kuna haja ya kulindwa, aseme tutakwenda," alisema.
Awali Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleman Kova alisema hawezi kuzungumzia ulinzi wa Dk Ulimboka kwa sababu tayari madaktari waliomba ulinzi UN.
UN wagoma kuongea
Msemaji wa Mwakilishi Mkazi wa UN nchini, Hoyce Temu hakutaka kueleza endapo taasisi hiyo ya kimataifa ilikubali ombi hilo au la akisema, suala la ulinzi halipaswi kuwekwa hadharani.
Alifafanua kuwa iwapo suala hilo litawekwa hadharani ni sawa na kuwapa nafasi maadui kujua namna mipango ya ulinzi ilivyopangwa.
"Suala la security (usalama) kama lilivyo si suala la kuwekwa wazi kwa public (umma)," alisema Temu.
Mwanzoni mwa Julai mwaka huu, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kiliomba ulinzi kutoka ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) jijini Dar es Salaam kikieleza kuwa hakina imani na polisi.
Chama hicho kiliomba ulinzi huo baada ya kuwapo na madai kwamba kuna kikundi cha watu kimekusudia kumuua Dk Ulimboka wakati akiwa kwenye matibabu nchini Afrika Kusini.
Katibu Mkuu wa MAT, Dk Rodrick Kabangila alipoulizwa endapo UN ilikubali kutoa ulinzi kwa Dk Ulimboka alijibu "haikuwa lazima kwa UN kutujibu."
Aliongeza, "Sisi tuliwasilisha barua, tukitoa malalamiko yetu, namna gani watafanya kazi ya ulinzi siyo lazima watujibu, wao wanataratibu zao za kufanya kazi."
Daktari wake anena
Profesa Joseph Kahamba alisema hajaonana na Dk Ulimboka tangu arejee nchini Jumapili ila anaamini anaendelea vizuri.Alipoulizwa imekuaje hajaonana na mgonjwa wake wakati yeye ndiye aliyemwandikia rufaa ya kutibiwa nje ya nchi alisema, "Siyo ajabu".
Alisema siyo lazima daktari aliyemwandikia mgonjwa rufaa ya kwenda kutibiwa nje ya nchi kuwasiliana naye anaporudi kwa kuwa hili linategemea hali aliyonayo mgonjwa husika.
"Hapa kuna mambo mawili; kuna kurudi akitakiwa tena kulazwa na kurudi kwa maana ya kupona," alieleza Profesa Kahamba baada ya kuulizwa kama ni lazima daktari aliyetoa rufaa awasiliane na mgonjwa baada ya kurudi kwenye matibabu.
Aliendelea "Angerudi (Dk Ulimboka) kwa state (hali) ya kulazwa, lazima angefikia kwangu nimwone, lakini kama amepona, anaweza kwenda kusalimia ndugu na kunywa bia kwanza halafu baada ya siku, wiki au mwezi akaja nikaonana naye."
Profesa Kahamba alieleza "Tangu Ulimboka arudi sijaonana naye zaidi ya kufanya mawasiliano na wenzake kwenye simu ila amepona kwa kuwa hajarudi kwangu."
MAT: Mwacheni apumzike
MAT kimewataka waandishi wa habari kutoendelea kumfuatilia Dk Ulimboka ambaye ni kiongozi wa jumuiya hiyo kwa kile walichoeeleza anatakiwa kupata fursa ya kupumzika.Makamu wa Rais wa MAT, Dk Prinus Saidia alipotakiwa kueleza ni lini atajitokeza hadharani kufuta kiu ya Watanzania kuhusu kilichomsibu, alisema:“Yeye mwenyewe ametuomba tumwache apumuzike kwa muda na sisi tumeona hili ni sahihi. Tumemwacha kwanza hadi hapo atakapotuambia kuwa yuko tayari kuungana nasi.”
Dk Saidia alisema madaktari kwa umoja wao wamefurahi kuona Dk Ulimboka amerejea akiwa mzima na kwamba hilo ndilo jambo bora zaidi kuliko kitu kingine chochote kwa sasa.
“Tunamshukuru Mungu Dk Ulimboka amerudi akiwa mzima, hili ndilo lilikuwa la msingi. Hata hivyo, suala liko wazi mgogoro baina yetu (madaktari) na Serikali haujafikia mwafaka. Inatakiwa pande zote zikae na kukubaliana na si upande mmoja kutumia nguvu,” alisema Dk Saidia.
Katika hatua nyingine habari kutoka ndani ya MAT zinasema viongozi wake wamekuwa wakifanya vikao vya ndani tangu juzi kujadili mambo mbalimbali likiwamo la kuandaa mazingira yatakayomwezesha Dk Ulimboka kuzungumza hadharani.
“Kuna vikao vinaendelea tangu jana (juzi), viongozi wanakutana kujadili mambo mbalimbali likiwamo namna Dk Ulimboka atakavyopata fursa ya kuzungumza,” kilisema chanzo hicho.
Dk Ulimboka alitekwa, kuteswa na kutupwa kwenye Msitu wa Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam usiku wa kuamkia Juni 26 mwaka huu.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment