SENSA ya Watu na Makazi jana iliingia siku yake ya pili, huku kasoro kadhaa ikiwamo ukosefu wa vifaa, upungufu wa makarani na watu kugoma kuhesabiwa vikiripotiwa.Katika baadhi ya maeneo hadi jana, wananchi walikuwa hawajaanza kuhesabiwa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na ukosefu wa vifaa na makarani.
Ofisa Uhamasishaji wa Sensa Taifa, Said Ameir alikiri kupata taarifa za kasoro hizo lakini akaeleza kushangazwa na chanzo chake, akisema: “Vifaa tulivigawa maeneo mbalimbali nchini kulingana na mahitaji. Tunashangazwa na taarifa hizo kwamba hata wengine wamekosa reflector (makoti ya kuakisi mwanga) na vitambulisho.”
“Tunachofanya sasa ni kuchunguza tatizo hilo limeanzia wapi na limesababishwa na nini. Vilevile tunajitahidi kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vinapelekwa sehemu hizo ili kazi hiyo iendelee kama kawaida.”
Alisema pamoja na kasoro hizo, kazi hiyo inaendelea vizuri na itakamilika ndani ya siku saba kama ilivyopangwa.
Kasoro
Baadhi ya makarani wa Kata ya Ubungo wamesema baadhi ya wajumbe wa nyumba kumi wamekataa kushirikiana nao.
Mratibu Msaidizi wa Sensa kata hiyo, Pertronia Lyamuya alisema tatizo jingine ni baadhi ya waumini wa Kiislamu kugoma kuhesabiwa kama ilivyokuwa kwa baadhi ya wakazi wa Kinondoni Shamba, Dar es Salaam.
Katika baadhi ya maeneo, makarani, walilazimika kutumia polisi kutekeleza majukumu yao. Baadhi ya mitaa ambayo polisi walitumika ni Juhudi, Kingugi na Kiburugwa iliyoko Temeke. Mitaa hiyo ilikuwa imebandikwa matangazo ya kuwahamasisha watu wasishiriki Sensa.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiburugwa, Engerasia Lyimo alisema kazi ya kuhesabu watu ilisimama kwa muda kusubiri polisi wa kuwasindikiza makarani hao kwenye nyumba hizo ili kulinda usalama wao.
Lyimo alisema katika Mtaa wa Kingugi, alijitokeza mjumbe wa shina wa CCM (jina tunalo),ambaye aliwahamasisha wakazi wa eneo lake wasijitokeze kuhesabiwa.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Basihaya, Kinondoni, Daniel Aron alisema kaya nane zilikataa kuhesabiwa kwa maelezo kwamba hazioni umuhimu wake. Alisema baada ya tukio hilo alitoa taarifa Ofisi ya Kata ya Boko.
Alisema kimsingi, changamoto kubwa katika eneo lake ni uchache wa vifaa kiasi cha makarani kushindwa kuanza kazi hiyo.
Msimamizi wa Kata ya Buguruni, Wilaya ya Ilala, Stella Mshana amesema kuwa baadhi ya watu wamekataa kuhesabiwa, wengine kutokana na imani za kidini na wengine kwa kutoelewa umuhimu wake.
“Maeneo ya Mnyamani tumekutana na vikwazo lakini kusema ukweli idadi yao ni ndogo kuliko wanaotupa ushirikiano. Unaweza ukakuta labda katika watu sabini, mmoja ndiye anakataa,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki amesema Serikali itaendelea kupambana na kundi la watu wanaojihusisha na kusambaza ujumbe wa kupinga kushiriki Sensa.
Alisema jana kwamba hadi sasa Polisi inawashikilia watu wanne kutoka Wilaya za Temeke na Kinondoni.... “Kijana mmoja alijulikana kwa jina la Yusuph Ernest alikamatwa akisambaza ujumbe huo maeneo ya Magomeni Kagera.”
Arusha
Watu wasiojulikana, juzi walibandika mabango yanayowazuia makarani wa Sensa kutekeleza wajibu wao katika Kata za Ngarenaro na Unga Ltd. Mabango hayo yalibandikwa katika eneo la Daraja la Ngarenaro.Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo pamoja na Mratibu wa Sensa Mkoa wa Arusha, Magreth Martin walisema hadi jana hakukuwa na tukio la kukwamisha Sensa licha ya kuwapo kwa tukio hilo.
“Nawashukuru sana wananchi wa Arusha kwa kushiriki vyema Sensa katika siku hizi mbili za mwanzo baada ya kuelimishwa na kuelezwa umuhimu wake kwa mipango ya Serikali na maendeleo ya taifa licha kuwapo baadhi ya watu waliojaribu kuwashawishi kususia.”
Tanga
Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Ibrahim Matovu wamewaagiza makarani wa Sensa kwenda kuwahesabu wanawake ambao waume zao wanadaiwa kukimbilia kusikojulikana kukwepa kuhesabiwa.Walitoa amri hiyo baada ya kuripotiwa kuwa baadhi ya Waislamu wa Kijiji cha Kigombe, Muheza, wamekimbilia porini kukwepa kuhesabiwa.
Inadaiwa kuwa baadhi ya wanaume waliondoka na kutoa amri kwa wake zao kutohesabiwa vinginevyo wangepewa talaka.Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Kigombe, Mashauri Kanyama alisema tatizo hilo limesababisha baadhi ya makarani kushindwa kutekeleza kazi zao kikamilifu.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kigombe, Mohamedi Hatibu alisema baadhi ya wakuu wa kaya wametishia pia kuwapa talaka wake zao iwapo watahesabiwa.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari
No comments:
Post a Comment