ASEMA HATA CCM INAJUA MSIMAMO WAKE.
Na: Peter Edson, Mwananchi.
WAKATI Serikali ikielekeza nguvu nyingi kutekeleza mkakati wa kuendeleza sekta ya kilimo nchini uliopewa jina la Kilimo Kwanza, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ameibuka na kusema haungi mkono mkakati huo.Alisema mkakati huo wa Kilimo Kwanza umekosa mashiko hivyo ili auunge mkono, kuna haja ya kubadili dhana yake na kuwa, elimu kabla ya kilimo kwanza.
“Ni vyema nikaeleweka hapa. Ninachomaanisha ni kuongeza elimu katika Kilimo Kwanza ili wananchi wawe na elimu kwanza ndipo waweze kuboresha kilimo,” alisema Lowassa.
Akizungumza katika Kipindi cha Dakika 45 kilichorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV juzi usiku, Lowassa alisema pamoja na Serikali kuwa na nia nzuri ya kumkomboa mwananchi kwa kuboresha mazingira ya kilimo, jambo hilo litakuwa si chochote kama hatapatiwa elimu itakayomwongoza kwenye mapinduzi hayo ya kijani.
“Mpango huu wa Kilimo Kwanza umekosa nguvu kwa sababu kuanzishwa kwake hakukuzingatia dhana ya ukombozi wa mwananchi wa kawaida. Tangu awali ndani ya chama (CCM) nilieleza kuwa sitaunga mkono hoja hiyo mpaka kuongezwe mashiko na kuwa Elimu Kabla ya Kilimo Kwanza,” alisema Lowasa na kuongeza:
“Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alitoa uamuzi mgumu na wenye busara, ndiyo maana kilimo cha pamba, kahawa, mkonge na mazao mengine vikaanzishwa. Hivyo ipo haja ya kufanyika mchakato wa kuona mbali zaidi ili viongozi wetu waweze kutoa uamuzi sahihi katika hoja hii ya Kilimo Kwanza, kwani nguvu nyingi pasipo elimu inaweza kuligharimu taifa.”
Alisema kuwa ili mwananchi wa kawaida aweze kunufaika na Kilimo Kwanza, anahitaji kupatiwa elimu ya kutosha ya namna ya kuandaa mazingira ya kilimo na uelewa wa vifaa na pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea na dawa.
Alisema pamoja na kuwa na mabwana shamba wachache, wananchi wamejikuta wakitumia mawazo yao kufanikisha miradi ya kilimo katika maeneo yao na matokeo yake wanapata mazao kidogo ambayo hayawakwamui kiuchumi.
Alitoa mfano wa nchi ya Indonesia akisema inaendesha uchumi wake kwa kilimo cha michikichi, ambayo mbegu zake zimetoka Tanzania... “Lakini Tanzania iliyotoa michikichi hiyo sasa ni moja ya wateja wa mafuta hayo yanayotoka Indonesia.”
Alishauri Serikali kuanzisha mashamba ya michikichi maeneo mbalimbali nchini kwa kuwa ardhi ipo ya kutosha hivyo kujitosheleza kwa mafuta hata ya kuuza nje.
“Ningelikuwa na uwezo wa kutoa uamuzi, vijana wetu wa JKT (Jeshi la Kujenga Taifa), ningewapa kazi ya kuanzisha mashamba ya michikichi nchi nzima kwani nchi yetu imejaliwa kuwa na ardhi kubwa na yenye rutuba, mapori yapo mengi,” alisema Lowassa.
Alisema wananchi wanaweza kupewa matrekta na pembejeo mbalimbali za kilimo, lakini bila kupewa elimu elekezi ya namna ya kuzitumia pembejeo hizo kuzalisha mazao bora, itakuwa kazi bure kwa kuwa ongezeko la mazao litakuwa dogo kama ilivyo kwa kilimo cha jembe la mkono.
Alitoa wito kwa Serikali kutumia fursa zilizopo za miradi ya kilimo kuwaelimisha Watanzania ili baadaye waweze kupewa au kukopeshwa zana za kilimo, akieleza kuwa nguvu kazi na elimu, ndivyo vitakavyomkomboa mwananchi katika umaskini wa kipato.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment