ASEMA ATAFANYA HIVYO BUNGE LA OKTOBA KAMA SERIKALI ITASHINDWA, MABILIONI HAYO YAHUSISHWA NA UFISADI WA MEREMETA
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe ameahidi kuwataja wanaohusika kuficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi katika kikao kijacho cha Bunge Oktoba, mwaka huu iwapo Serikali itashindwa kufanya hivyo hadi muda huo.
Wakati Zitto akisema hayo, kashfa hiyo imechukua sura mpya na sasa fedha hizo zinahusishwa na ufisadi katika Kampuni ya Meremeta.
Kauli ya Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, imekuja siku chache tangu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta kuwataka wanaowafahamu walioficha fedha hizo kuwataja hadharani ili iwe rahisi kwa Serikali kuwachukulia hatua.
Hata hivyo, Zitto akizungumza na gazeti hili jana alisema: “Mimi ni mbunge makini ninayefahamu taratibu za Bunge na kuheshimu haki za watu wengine, siwezi kukurupuka katika suala hili. Ninaiachia Serikali na vyombo vyake iendelee kulifanyia kazi na ikiwa watashindwa kuwataja wahusika, basi wasubiri kikao kijacho, nitaweka hadharani majina ya wahusika wote.”
Zitto alisisitiza kuwa Serikali ina uwezo wa kupata taarifa zozote inazozihitaji kutoka Uswisi na kwamba ndiyo maana ameipa muda wa kulifanyia kazi suala hilo kabla yeye hajachukua hatua ya kuwataja wahusika.
“Sikia, lazima tukubaliane jambo moja kwamba mimi siyo Serikali, wala sina dola, ndiyo maana nasema kwamba tusubiri utekelezaji wa ahadi ya Serikali, lakini wakishindwa kuwataja, basi mimi nitatumia nafasi yangu kama mbunge kuwataja na nitafanya hivyo ndani ya Bunge na wala siyo nje ya hapo,” alisema.
Uchunguzi zaidi wa gazeti hili umebaini kuwa kiasi cha Dola za Marekani 186 milioni (takriban Sh300 bilioni) kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni Sh1,600 kwa Dola ya Marekani, kimefichwa katika benki tatu tofauti za Uswisi.
Uchunguzi zaidi unabainisha kuwa takwimu hizo ni rasmi kwani zimetolewa na Benki Kuu ya Uswisi, lakini taarifa zaidi zinadai kuwa kuna fedha nyingi zaidi zilizofichwa na Watanzania katika benki nyingine nchini humo ambazo taarifa zake zinaweza kupatikana ikiwa Serikali itasimamia vizuri suala hilo.
Watanzania 27 wameripotiwa kumiliki fedha nchini humo, na mmoja wao anadaiwa kwamba anamiliki Dola za Marekani 56 milioni (wastani wa Sh89.6 bilioni).
Kashfa ya kuwapo kwa vigogo walioficha fedha zao Uswisi iliibuliwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini Juni mwaka huu na baadaye mwangwi wake kulitikisa Bunge katika Mkutano wake wa Nane uliomalizika hivi karibuni.
Habari hizo zilikuwa zikinukuu taarifa ya Benki Kuu ya Uswisi iliyoitoa na kuonyesha kuwapo kwa kiasi cha Sh315.5 bilioni zilizotoroshwa Tanzania na kufichwa nchini humo na vigogo ambao ni wanasiasa pamoja na wafanyabiashara.
Suala hilo pia lilijadiliwa katika kikao cha Bunge kilichopita, huku ikidaiwa kwamba fedha hizo zinatokana na biashara (deals) zilizofanywa na watendaji wa Serikali na wafanyabiashara kwenye sekta za nishati na madini na kwamba sehemu kubwa ya fedha zililipwa na kampuni za utafutaji mafuta na gesi katika Pwani ya Mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.
chanzo:http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment