Friday, October 12, 2012

MATOKEO YA CHAGUZI ZA CCM - WAZAZI MKOANI ARUSHA...!

CHAMA cha mapinduzi mkoa wa arusha  kimemchagua mbunge  wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Bernard Murunya,  kuwa Mwenyekiti wa Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Arusha.

Aidha  uchaguzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa makao makuu ya CCM Mkoa wa Arusha jana, Murunya aliwashinda wenzake watatu kwa kupata kura 169 kati ya kura 334 zilizopigwa.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Mary Chatanda, ambaye ni Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha na Mbunge wa Viti Maalum, aliwataja wagombea wengine katika nafasi hiyo na kura walizopata kwenye mabano kuwa ni Edwin Seneu (1), Mohammed Festo (68) na Musa Mkanga (69).

Kwa upande wa  nafasi ya Baraza Kuu la Taifa Wazazi/Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, aliyechaguliwa kuchukua nafasi hiyo ni John Pallangyo kwa kupata kura 211 na kuwashinda Mbunge wa Viti Maalum, Namelok Sokoine (112), Harun Matagane (6) na Baltazar Lymo (4).

Aidha nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa ilikwenda kwa Fatuma Ngairo aliyepata kura 312 dhidi ya Mohammed Said Hassan (21) na Jonas Lubulu (6) na kwa upande wa Baraza la Wazazi la Mkoa ilinyakuliwa na Lucy Bongole (239) dhidi ya Mariam Athman Majengo (78) na Filemon Amo (7).

Akizungumza baada ya kuchaguliwa kwake, Murunya ambaye ni Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA), lisema Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Arusha, inakabiliwa na tatizo la ukata ambapo ulisababisha ugumu kuwasafirisha wajumbe kutoka maeneo mbali mbali wilayani kuhudhuria uchaguzi huo muhimu.

Hata hivyo, alisema chini ya uongozi wake atahakikisha kwamba analitafutia ufumbuzi tatizo hilo ndani ya kipindi cha miaka miwili, “Tutafanya mikakati kuhakikisha Jumuiya inaondokana na ukata, tutabuni miradi ya kupata fedha na ndani ya miaka miwili mtakuja hapa mkiwa kifua mbele,” alitamba Murunya.

No comments: