Mwili wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow (52), utaagwa leo, Oktoba 15, 2012, katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa jeshi hilo mkoani humo Lilian Matola, imesema kwamba shughuli ya kuaga mwili huo itaongozwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Inpsekta Jenerali Saidi Mwema.
Matola alisema kwamba, viongozi wengine wa kiserikali watakaoshiriki ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge, William Lukuvi, Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Evarist Ndikilo, wakuu wa wilaya na viongozi waandamizi wa jeshi hilo.
Alisema kuwa shughuli za kuaga zitaanza saa 3:00 asubuhi baada ya mwili kutolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando na kupelekwa kwanza nyumbani kwake Pasiansi. Baadaye saa 4:00 hadi saa 6:00 mchana itafanyika Ibada ya kumuombea kabla ya kusomwa kwa wasifu wake na salamu kutoka kwa IGP, Makamanda wa mikoa mingine na viongozi mbalimbali vya Vyama vya siasa.
Matola alisema kuwa, mwili wa marehemu Barlow utasafirishwa mchana kwenda jijini Dar es Salaam ambako taraibu nyingine za kuomboleza zitafuata kabla ya kusafirishwa kwenda mkoani Kilimanjaro kwa taratibu za maziko.
No comments:
Post a Comment