Saturday, November 10, 2012

Hoja Ya Mdee ‘Kaa La Moto’ Kwa Serikali

MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee amewasilisha hoja binafsi bungeni akiitaka Serikali kusitisha ugawaji wa ardhi hadi tathmini ifanyike, huku akimtuhumu Waziri Mkuu kuwa anashiriki katika kuwakumbatia wawekezaji wanaopora ardhi wananchi.

Mdee amesema kuwa bila kufanya hivyo, ardhi yote ya nchi hii itachukuliwa na wawekezaji huku wananchi wakiachwa masikini.

Akiwasilisha bungeni hoja binafsi kuhusu kusitishwa ugawaji ardhi nchini, Mdee aliitaka Serikali kusitisha ugawaji wa ardhi hadi hapo tathmini ya kina itakapofanyika kujua kiasi cha ardhi kilichopo mikononi mwa wawekezaji.

Vile vile, alitaka tathmini ya kina ifanyike kubaini raia wa kigeni na wa ndani waliojipatia ardhi kinyemela kupitia Serikali za vijiji kinyume na matakwa ya sheria ya ardhi namba 5 ya mwaka 1999.

“Kwa mujibu wa Kanuni  namba  54(1), (2)  na (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007 naomba kutoa hoja binafsi ya kuitaka Serikali kusitisha ugawaji wa ardhi kwa wawekezaji wa ndani na wa nje mpaka hapo tathmini ya kina itakapofanyika kubaini ni kiwango gani cha ardhi kiko mikononi  mwa wawekezaji,” alisema Mdee.

Alisema katika miaka ya hivi karibuni, kutokana mtikisiko wa uchumi duniani, tumeshuhudia wimbi la wawekezaji kutoka nje wakingia nchini kuwekeza katika kilimo kwa maelezo kwamba watasaidia kuinua uzalishaji katika sekta ya kilimo.

Hata hivyo, alisema uwekezaji huo wa wageni katika ardhi umegeuka kuwa shubiri kwa wananchi hususan wakulima wadogo.

Alisema wakulima hao wamekuwa wakiondolewa katika maeneo yao ya asili ili kuwapisha wageni huku wakiachwa katika lindi la umasikini mkubwa.

Mdee alisema ardhi hiyo imekuwa ikichukuliwa na Serikali kuwa haina mwenyewe au haitumiki.

“Hii inatokana na ukweli kwamba kumekuwa na tafsiri ambayo sio sahihi, kwamba ardhi wanayopewa wawekezaji haina wenyewe, haina mtu, haitumiki. Wakati ukweli ni kwamba maeneo mengi kama sio yote yalikuwa yanatumiwa na wakulima wadogo,” alisema.

Mdee alisema wawekezaji wamechukua maeneo makubwa ambayo wameshindwa kuyaendeleza na hata yale ambayo wanayaendeleza ni kwa kiasi kidogo.

Alisema baadhi ya waewekezaji wengine baada ya kumilikishwa ardhi kwa bei ya kutupa wamekuwa wakikaa nayo na baadaye kuiza kwa wawekezaji wengine.

Mdee aliliomba Bunge kukubali Serikali kusitisha ugawaji wa ardhi ili kuangalia wapi ilipokosea kwa manufaa ya nchi.

Mbunge huyo kupitia Chadema, alisema hata wizara ya ardhi na maendeleo ya makazi wakitakiwa leo kutoa taarifa sahihi ya ardhi kiasi gani iko chini ya miliki ya wageni hawana taarifa hizo.

Alisema kutokana na waewekezaji kupewa ardhi bila ya kufuata taratibu, hivi sasa migogoro mingi ya ardhi iliyopo nchini inatokana na wananchi kuporwa ardhi kwa kisingizio cha uwekezaji.

Alitoa mfano wa Kampuni ya Kigoma inayofahamika kama Agrisol na FELISA ambayo imenunua hekari 3,000 katika Kijiji cha Basanza Kata ya Uvinza wilayani ya Uvinza.

Alisema wawekezaji hao ambao wanakingiwa kifua na Waziri Mkuu, wamewakuta wakulima na wafugaji katika maeneo haya.

Alisema mwekezaji kwa kushirikiana na vyombo vya dola aliwatoa kwa nguvu wananchi akitumia askari mgambo kupiga wananchi, kuchoma nyumba, kuharibu mazao na halikadhalika kuwafungulia wananchi mashtaka.

Alitaja maeneo mengine yenye migogoro kuwa ni wananchi na wawekezaji kuwa ni Rufiji, Kilombero, Bagamoyo, Kisarawe, Muheza, Pangani, Katavi ,Meatu, Kinondoni, Njombe na Ngorogoro.

Moto wa hoja hiyo uliwafanya baadhi ya mawaziri kuinuka kuchangia akiwamo, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Tibaijuka, Waziri Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, (Uwekezaji na Uwezeshaji), Mary Nagu na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais (Mahusiano), Steven Wassira.

Akichangia hoja hiyo, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Tibaijuka alikubali kufanya marekebisho katika sheria ya ardhi ili iweze kuwanifaisha watanzania.

Alisema hakubaliani na hoja ya Mbunge Mdee ya kutaka kusitisha utoaji wa ardhi kwa wawekezaji akisema hali hiyo inaweza kuleta matatizo zaidi.

Profesa Tibaijuka alisema ni aibu kwa nchi yenye ardhi kubwa na yenye rutuba kushindwa kujitosheleza kwa chakula.

Hivyo, alisema kuwapa wageni wenye mitaji ardhi kwa ajili ya kilimo kutasaidia kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao na hivyo kujitosheleza kwa chakula.

Profesa Tibaijuka alisema ili watanzania waweze kunufaika na uwekezaji mkubwa wa ardhi nchini, Serikali itakuwa inachukua hisa katika mshamaba hayo na kuziuza kwa wananachi.

“Serikali hii haiwezi kukukbali wananchi wake kuporwa ardhi na wawekezaji,” alisema.

Alisema anakubalina kufanyiwa marekebisho sheria hiyo ili iweze kumsiadia mwananchi.

Waziri Nagu, alisema hatuwezi kusitisha uwekezaji kwa wageni kwa sababu itasabisha kurudisha nyuma maendeleo katika sekta ya kilimo.

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari/siasa

No comments: