ULIMI ni silaha inayoweza kuharibu au kuujenga uhusiano imara. Inategemea wewe mwenyewe unajipanga vipi na unautumiaje. Aina ya watu wanaotajwa kwamba wana gubu, ni matokeo ya matumizi mabaya ya ulimi.
Wiki iliyopita nilikushauri uchunge sana ulimi wako. Nikiwa na maana kuwa unapaswa kuzungumza mambo mazuri na hata pale unapotakiwa kunena kwa ukali, basi angalia usipitilize. Inawezekana una hoja nzito lakini uwasilishaji wako ukawa maumivu kwa mwenzi wako mpaka akakuona ni tatizo.
Maneno yako yanaweza kumfanya mpenzi aliyekupenda kwa moyo mmoja, akimbie. Tamka maneno matamu kwake, siyo ya kumkera. Hata kama amekukosea, zungumza naye umalize. Siyo muda wote uwe unamsemasema. Hakuna adhabu kubwa kwa mtu kama kumsemasema. Atakukimbia tu.
Atajitahidi kukuvumilia kadiri anavyoweza lakini mwisho ataachana na wewe. Kwa hiyo ulimi wako unapaswa kuuchunga na kuuelekeza kutamka maneno mazuri. Siyo ugeuke kero na kumdhalilisha mpenzi wako. Ulimi wako unaweza kutoa picha wewe ni mtu wa aina gani.
Maneno mabaya unayotamka, yatatoa picha kwamba wewe ni kiburi, jeuri na usiye na heshima kwa mwenzako. Kama utafanikiwa kuudhibiti ulimi wako, utakuwa umefanikiwa kukishinda kirusi hatari mno kwenye uhusiano wako. Nakusisitiza uuchunge ulimi wako, ni rahisi kuteleza.
Uungwana ni kuomba radhi pale unapobaini umeteleza ulimi. Unapoendelea kushikilia msimamo wako huku ukitetea kauli mbaya uliyoitoa, ni muendelezo wa matumizi mabaya ya ulimi. Laiti kama kila mtu angetambua umuhimu na thamani ya ulimi, maisha yangekuwa murua sana.
Ulimi unaweza kumfanya aliyefumaniwa asamehewe. Inategemea namna ambavyo anaweza kuutumia ulimi wake kujieleza na kuonesha jinsi anavyojutia kosa lake. Usichokijua ni kama usiku wa giza, utashangaa mtu kafumaniwa lakini uhusiano unaendelea.
Usishangae pia mtu ambaye alikutwa na SMS ya bahati mbaya na uhusiano ukavunjika. Inategemea aliyekutwa nayo alizungumza nini. Ni kweli SMS ilikosea njia ikaingia kwenye simu yake lakini alishindwa kujieleza. Badala ya kumfanya mwenzi wake aelewe, yeye akawa mkali.
Mwenzi wake atajiuliza, yaani amemnasa na SMS halafu anageuziwa kibao. Mfano, umekutwa na SMS ambayo kuna mtu alikuwa anamtumia mpenzi wake, sasa kwa bahati mbaya ikaja kwako. Kama mpenzi wako ameiona, unatakiwa umueleweshe mpaka akuelewe.
Kuna mtu alikutwa na tukio kama hilo, alipoulizwa na mwenzi wake hakutoa majibu, badala yake akaanza kumfokea mpenzi wake eti kwa nini ameshika simu yake. “Wewe nilishakwambia achana kabisa na simu yangu. Mjinga nini wewe!” Kwa nini mwenzi wake asikimbie?
Unaweza kuona tofauti kwamba aliyekutwa ‘live’ akisaliti, anasamehewa kwa sababu aliomba radhi, akaonesha kujuta. Alipokataliwa siku ya kwanza, akajaribu tena na tena, huku akisisitiza yale yaliyotokea hayatajirudia tena. Ni ulimi tu, ingawa wanasema majuto ni mjukuu lakini anayejuta husamehewa.
TAFAKARI SASA
Badala ya kujuta, kusaga meno kwa imani kwamba unaonewa, ni vizuri kutuliza kichwa, upate majibu ya mzizi wa tatizo. Inawezekana ukawa ni wewe mwenyewe, kwa hiyo hutakiwi kulia, badala yake futa machozi utazame mbele. Maisha yanaendelea.
Siku zote weka akilini kuwa jawabu la kila changamoto inayoweza kukukabili, ipo ndani ya uwezo wako mwenyewe. Kama mapenzi ni magumu kwa upande wako, ni jukumu lako kuhakikisha yanakuwa mepesi ama kwa kujirekebisha wewe mwenyewe au kuachana na mpenzi msumbufu.
Machozi yako yana thamani kubwa, hutakiwi kuyatoa kwa mtu ambaye hathamini upendo wako kwake. Amekuacha, hupaswi kujiinamia muda wote na kushindwa kufanya shughuli zako. Hebu piga moyo konde, tazama mbele kwa matumaini kwamba kila kitu kizuri kinakuja.
Makosa yako yarekebishe. Kama ulikosea na ukajirekebisha, ukaomba msamaha lakini bado hujasamehewa, vilevile usijute, tazama mbele. Hupaswi kumlimlia mpenzi aliyepita bali jenga picha tamu juu ya mwenzi wako anayekuja. Zingatia kwamba kuna waliolia Farao alipozama Bahari ya Shamu bila kujua kuwa kifo chake ndiyo ukombozi wa wana wa Israel.
Nakutakia kila la heri kwenye maisha yako.
No comments:
Post a Comment