Friday, November 30, 2012

UVUMI KIFO CHA RAY C

WAKATI msanii Hussein Ramadhan Mkieti ‘Sharo Milionea’ akizikwa kijijini kwao, Muheza, Tanga Jumatano iliyopita, uvumi mkubwa umelitikisa Jiji la Dar es Salaam kuwa, mwanamuziki wa  Kizazi Kipya, Rehema Chalamila ‘Ray C’ naye ameaga dunia ghafla.

Uvumi huo ulizagaa kwa kasi kuanzia saa kumi na mbili jioni kupitia mitandao ya kijamii na ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kupitia simu za mkononi huku wengine wakidai ni ‘komfemdi’.
Baadhi ya watu walianza kuamini uzushi huo na kujiuliza kulikoni katika burudani Bongo kuwapoteza mastaa wao mfululizo.
“Juzi tu Mlopelo, halafu John Maganga, jana (Jumatatu) Sharo Milionea. Leo tena Ray C, kuna nini kwa mastaa wetu?” alihoji mmoja wa  watu waliotumiwa ujumbe huo huku akishika kichwa kuonesha hali ya majonzi.

Hata hivyo, hadi kufikia saa 4 usiku, mama mzazi wa Ray C, Margaret Mtweve alijitokeza hadharani kupitia Radio Clouds FM na kukanusha vikali taarifa hizo huku akisema:
 “Mwanangu ni mzima, tena anaendelea vizuri kwa sasa. Hao wanaoneza uzushi huo washindwe kwa jina la Yesu.”
Awali, mchana wa siku
hiyo, zilienea tetesi eti msanii nyota wa sinema Bongo, Juma Sadiki Kilowoko ‘Sajuki’ naye amefariki dunia wakari si kweli.

Watu waliozungumza na gazeti hili jana walionesha wasiwasi wao mkubwa juu ya ufahamu wa baadhi ya Watanzania ambao wamekuwa na tabia ya kueneza uvumi mara kwa mara kwamba mtu f’lani, hasa maarufu amefariki dunia.
“Nahisi kuna Watanzania si wazima vichwani kwani sasa imekuwa fasheni. Mtu anaamua tu, anaandika ujumbe kwenye simu kwamba staa f’lani amefariki dunia wakati si kweli,” alisema Hamad Hussein, mkazi wa Magomeni-Kagera, Dar.

No comments: