Wednesday, November 14, 2012

Wanafunzi Wa Kitanzania Nchini Urusi Wakosa Malazi Na Chakula...!

Sisi wanafunzi wa kitanzania nchini Urusi ,tunakosa huduma za msingi kama vile malazi , chakula na bima ya afya.

   Serikali kupitia bodi ya mikopo ya elimu ya juu na Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi ,kwania njema iliamua kusomesha wanafunzi wa kitanzania katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Urusi.
Lakini kutokana na utendaji mbovu na ubinafsi wa baadhi ya watendaji wa Bodi ya mikopo, kumekua na ucheleweshwaji wa ulipaji wa pesa za kujikimu , malazi na bima ya afya kwa zaidi ya miezi mitatu sasa bila sababu za msingi toka kuanza kwa mwaka wa masomo 2012/13.

Hali hii imetupelekea wanafunzi kuanza kufukuzwa katika hosteli tunazoishi pamoja na kutopatiwa huduma za afya pindi tunapo ugua.Ikumbukwe kuwa katika nchi za ulaya huwezi pata matibabu kama huna bima ya afya.

Shukrani zetu za dhati ziende kwa Ubalozi wa Tanzania nchi Urusi kwa kushirikiana bega kwa bega na Wanafunzi katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili linalotukabili katika kipindi hiki kigumu pamoja na majuku mengi waliyonayo, pamoja na jitihada hizo mpaka sasa hakuna ufumbuzi wowote uliopatikana.

Tunaandika waraka huu kwa huzuni na masikitiko makubwa sana kwa sababu kutopatiwa mikopo mpaka sasa sio tu kunafanya wanafunzi waishi maisha magumu na hatari, vilevile kunatia aibu Taifa kwa kutolipa ada kwa wakati.

Tunaamini kabisa Serikali kupitia bodi ya mikopo ,wizara ya elimu na mafunzo stadi na ufundi na ubalozi wa Tanzania Nchini Urusi una  nia njema kabisa kusomesha vijana wake nje ya nchi, ispokua tu kuna baadhi ya watendaji wa bodi ya mikopo wamekua wazembe na kutowajibika kwani wamekua wakitoa majibu ya uongo na jeuri kwa uongozi wa wanafunzi na maafisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Urusi.

Ombi letu kwenu ni kutufikishia ujumbe huu kwa wahusika na watendaji wa ngazi za juu za bodi ili waweze kutusaidia sisi wanafunzi wa Urusi ambao tupo hatarini huku ugenini.

Tunatumaini kutokana na Uzito wa tatizo letu wahusika watalishughurikia na kulitatua tatizo hili kwa haraka zaidi na kutupa ufafanuzi wa ucheleweshwaji wa mikopo ya wanafunzi kwa zaidi ya miezi mitatu(3)

WANAFUNZI NCHINI URUSI.

No comments: