HAYAKUISHIA hapo, siku moja Mataba alikutana na Idrisa. Bila woga wala aibu, mzee huyo akaanza kumshambulia kwamba amekuwa tajiri hamthamini, wakati yeye ndiye aliwezesha akasoma. Idrisa akiwa anashangaa, Mataba akamwambia: “Mimi nilikuwa namhonga mama yako fedha ili wewe upate karo na nauli ya kwenda shule.”
Hapo utaona kuwa ubinafsi wa mama yake Idrisa, kusaliti ndoa yake na kwenda kutembea na Mataba, inakuwa taadhira kwa mtoto wake. Anatukanwa, anafedheheshwa kwa makosa ambayo si ya kwake. Tafadhali sana, usijifikirie peke yako, fikiria na kizazi chako.
SHINDA UBINAFSI, KOMESHA UCHAFU
Ukivaa mavazi chakavu, machafu, usijifikirie wewe binafsi, fikiria kuwa mwenzi wako utamuaibishaje kwa muonekano wako usio na mvuto. Huwezi kupinga ukweli kwamba mpenzi wako akiwa amevaa ‘malapulapu’, utaona aibu hata kumtambulisha kwa marafiki zako.
Kama inakuwa hivyo, basi nawe jiwekee utaratibu wa kuvaa vizuri kwa lengo la kumlindia heshima mwenzi wako. Usafi wako ni fundisho kwake, vilevile itakuwa rahisi kumrekebisha. Utawezaje kumrekebisha mwenzio kwamba ni mchafu, ikiwa wewe mwenyewe hutamaniki?
Muonekano wako mzuri ni nguo kwa mwenzi wako au familia yako kama tayari wewe ni baba au mama. Kadiri unavyokuwa msafi, ndivyo heshima yako inavyokuwa juu. Usmati ni sanaa inayoweza kumpa hadhi mtu sehemu yoyote ile.
Matapeli wengi mjini ili kuwaibia watu huvaa vizuri. Ukiwaona utadhani ni maofisa fulani kumbe wezi tu. Kama matapeli wanapendeza angalau nao waonekane ni watu wenye heshima zao ni kwa nini wewe mwenye heshima zako usivae vizuri.
Inawezekana nyumbani kwako wewe ni msafi na unazingatia maadili. Hata hivyo, hayo ni matunda ya ndani kwao, nje pia unapaswa kujiweka vizuri, kwani huko ndiko unakoweza kuheshimiwa na kumpa thamani mwenzi wa maisha yako.
Haina maana kwamba nyumbani ndiyo unaruhusiwa kupaacha vululuvululu. Hapana, nako panahitaji umakini wake. Isiwe kama simulizi za Wakongo, kwamba anaweza kupita barabarani ananukia pafyum za bei mbaya, amevaa dhahabu na nguo za gharama, kumbe nyumbani analalia jamvi au boksi.
Siku zote zingatia kwamba heshima ya mwenzi wako itatokana na wewe mwenyewe unavyoonekana mbele za watu. Wakati mwingine uhusiano wa watu wengi unavunjika kwa sababu ndogondogo mno. Pengine mmoja ni mchafu, kwa hiyo mwenzake akashawishika alipomuona msafi.
Ingawa siku zote nimekuwa nikikutaka umjenge mpenzi wako, kwamba kama unaona ni mchafu na we hupendi alivyo, basi fanya jitihada za kumfanya awe na muonekano mzuri mbele yako na kwa wengine. Nenda madukani ukanunue mavazi ambayo unaona yatamfanya apendeze, hivyo kulinda heshima yako.
Kama mpenzi wako ananuka kikwapa, usimuache akachekwa mitaani. Unayo nafasi ya kumlinda kwa kumfanya badala ya kunuka awe ananukia. Hii ni kwa sababu mnapokuwa wawili, ujenzi wa thamani yenu unategemeana. Unamjenga mwenzako naye anakujenga.
Siku zote tambua kwamba jinsi unavyojiweka kistaarabu ndivyo unavyoweza kutoa sura ya namna ambavyo mwenzi wako atachukuliwa na watu wengine. Mapenzi ni sanaa inayohitaji mtu aishi kwa masilahi ya mwenzi wake. Kwa faida yako, nakuomba uanze utekelezaji wa falsafa hii.
Kuna msemo kwamba ukitaka kumjua mtu muangalie rafiki yake. Hivi ndivyo inavyokuwa.
No comments:
Post a Comment