WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka wakazi wa wilaya mpya ya Mlele mkoani Katavi walime mazao mbadala ya biashara kama alizeti, karanga na ufuta kwa sababu yanachukua muda mfupi na hivyo kuleta kipato cha haraka.
Ametoa wito huo juzi jioni (Ijumaa, Desemba 14, 2012), wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Nsenkwa mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye zahanati ya kijiji hicho akiwa katika siku ya pili ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.
Waziri Mkuu aliwataka wakazi hao kuachana na mazoea ya kulima tumbaku kwa vile inachukua muda mrefu hadi kukomaa na inachangia uharibifu mkubwa wa mazingira kwani inahitaji kuni nyingi wakati wa kukausha.
“Tumbaku hivi sasa haina bei kwa sababu wanaopanga bei ni wakubwa huko nje… tuangalie mazao ya alizeti, ufuta na karanga kwa sababu yanatoa pesa kwa haraka zaidi. Mfano mzuri ni Singida ambao wamekuja juu kiuchumi kwa sababu ya zao la alizeti,” alisisitiza.
Aliwataka wakazi hao waangalie ufugaji nyuki kama fursa ya kipekee kwa sababu mkoa huo umejaliwa kuwa na misitu mingi na unaweza kuongeza kipato cha mkoa wao. “Asali ni dawa, asali ni chakula, asali ni biashara na ina soko hapa nchini hadi nje ya nchi.
Changamkieni fursa hii, ongezeni uzalishaji wa asali na nta,” aliongeza.Aliwashauri pia waangalie uwezekano wa kulima miembe ya kisasa kwasababu inazaa kwa wingi na katika kipindi kifupi mno. “Hii miembe yenu inazaa maembe 10-20 kwa mwaka lakini ya kisasa inazaa hadi maembe 10,000, ikiwa chinichini tu,” alisema.
No comments:
Post a Comment