Wednesday, January 16, 2013

Bus la champion lamgonga mtembea kwa miguu na kusababisha kifo

YAH: TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA DODOMA KWA VYOMBO VYA
HABARI TAREHE 15/01/2013

Mtu mmoja amefariki Dunia Mkoani Dodoma katika tukio la ajali ya gari kumgonga mtembea kwa miguu na kusababisha kifo.

Tukio hilo  limetokea tarehe 14/01/2013 majira ya saa 09:30 alasiri katika kijiji cha Kelema  Wilaya ya Chemba barabara ya DODOMA -KONDOA baada ya  gari lenye namba za usajili T. 769 BNP aina ya Scania  Bus mali ya  Kampuni ya Champion  likendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina la  George s/o Maiko Kwayu likitokea Dodoma kuelekea Kondoa kumgonga mtembea kwa miguu na  kumsababishia kifo chake papo hapo.

Marehemu ametambuliwa kuwa ni Mohamed s/o Hassan mwenye umri wa Miaka(110) Mrangi ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kalamba kuu Kelema wilayani Chemba.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa Dereva kwa kutokuwa mwangalifu kwa watumiaji wengine wa barabara kwani  alikuwa katika mwendo wa kasi  katika eneo lenye makazi ya watu kinyume na sheria za usalama barabarani zinavyoelekeza.

Madereva wanatakiwa kujua na kuzingatia ni mwendo gani watumie katika maeneo tofauti wanayopita, kama Kifungu namba 51, kifungu kidogo cha 8 (a) cha  sheria ya Usalama barabarani ya Mwaka 1973 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 sura ya 168 ambayo inatamka bayana kwamba mtu yeyote anayetumia chombo cha moto barabarani haruhusiwi kuendesha chombo hicho zaidi ya spidi 50  kwenye makazi ya watu.

Napenda kutoa wito kwa madereva wote kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za usalama Barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima, ambazo hulipunguzia taifa nguvu kazi.

Mtuhumiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi na atafikishwa mahakamani pindi uchunguzi utakapokamilika.

DAVID MISIME - ACP

KAMANDA WA POLISI MKOA WA DODOMA



No comments: