Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka wa pili Kitivo cha Sheria, Joseph Bernadina (25), amejinyonga kwa kutumia kamba na kukutwa ameifunga juu ya mti, katika eneo la Yombo chuoni hapo.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Utawala, Profesa Yunus Mgaya, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba alipata taarifa hizo jana asubuhi.
Aliongeza kuwa Jumamosi iliyopita alipokea simu kutoka kituo cha polisi cha chuo hicho akielezwa kuwa kuna mwanafunzi alitishia kujiua, lakini aliwahishwa hospitali na kupatiwa ushauri kutoka kitengo maalum cha washauri wa chuoni hapo na kuruhusiwa Jumapili.
“Nilikuja tena kushituka leo asubuhi napokea simu kutoka kwa mshauri wa wanafunzi kuwa kuna wanausalama wamemkuta mwanafunzi akiwa amejinyonga juu ya mti huku akiwa na karatasi kwenye mfuko wa sharti ikimtambulisha pamoja na ujumbe uliosema, kifo chake kisihusishwe na mtu yeyote kwani amejiua kwa ridhaa yake --asisumbuliwe mtu yeyote kwani nimefanya hivi kwa maamuzi yangu mwenyewe pia nizikwe kwetu--” alisema.
Profesa Mgaya alisema taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa na Uongozi wa chuo kwa kushirikiana na ndugu wa marehemu na kwamba Chuo kitagharamia kuusafirisha mwili kama alivyoomba katika ujumbe aliouacha wa kupelekwa wilayani Ludewa Mkoa wa Iringa.
Naye rafiki wa marehemu, Daniel Mwamlima, alisema marehemu hakuwahi kuzungumza chochote kilichoashiria kuwa ana matatizo wala mgogoro na mtu yeyote. Alisema walimuacha hospitalini Jumamosi na kesho yake kumchukua, lakini baadaye aliwatoroka.
“Sasa leo (jana) asubuhi tulipata taarifa za mwanafunzi kujinyonga mbaya zaidi tukakuta ni yeye,” alisema Mwamlima.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho (DARUSO), Yasini Athumani, alisema wamezipokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa tukio na alisema uchunguzi wa awali umebaini kwamba marehemu aliwahi kuwa na historia ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kupata matibabu ya ugonjwa wa msongo wa mawazo.
No comments:
Post a Comment