LICHA ya serikali kuyapiga marufuku maandamano yaliyoratibiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuishinikiza kumwajibisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Naibu wake wajiuzulu kutokana na matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne 2012, chama hicho kimesema yapo pale pale.
Chama hicho kimewaomba wananchi wote waliochoshwa na kufelishwa kwa watoto wao, kunyimwa elimu bora wajitokeze kuandamana kwa nguvu zote, na wanafunzi wote waliofeli pia wajitokeze kudai elimu bora kwani ni haki yao.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana na kutoa msimamo huo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema “wananchi wajitokeze kwa wingi ili kilio chao kisikike duniani kote.”
Alisisitiza kuwa maandamano hayo yatafanyika mbele ya ugeni wa Rais wa China, Xi Jinping ili kufikisha kilio hicho na kamwe haikubaliani na sababu ya serikali kuyazuia kwa sababu ya ugeni huo.
Alisema maandamano hayo yatasaidia kupuuza kunakofanywa na Serikali ya CCM kuonwe na dunia nzima maana vyombo vyote vya habari vitafuatilia tukio hilo.
Mbowe aliongeza kuwa, “Watanzania waliochoshwa na ubabaishaji katika elimu wajitokeze, kulaani kitendo cha Waziri Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo kulindwa na serikali, badala ya kuwajibishwa kwa matokeo mabaya ya watoto wa Kitanzania.”
Alipoulizwa itakuwaje maana kutakuwa na ugeni wa Rais wa China nchini, sababu ambayo hata serikali imeitumia ili kuyazuia maandamano hayo, Mbowe alijibu: “Kilio chetu hakikuja na Rais wa China, kama Serikali ya CCM wanaona aibu kumwajibisha waziri mmoja na naibu wake, basi wasubiri aibu ya dunia kuona jinsi Tanzania inavyoendeshwa kibabe, ikiwa haina elimu bora.
“Tumetangaza maandamano wiki tatu zilizopita, hatukuwa na taarifa na ujio wa Rais wa China, lakini jinsi Mungu alivyo upande wetu amemleta Rais wa China, kweli Mungu ni mwema, hakuna tena nafasi ya kusubiri kuficha ubovu katika sekta ya elimu nchini, ndani ya siku ambayo CHADEMA waliandaa maandamano ili dunia nzima isikie kilio cha Watanzania kuhusu elimu.
“Sababu kuwa CCM nao wameandaa maandamano kupinga maandamano ya CHADEMA hazina msingi ni kutowajibika kwa Jeshi la Polisi. Hatukatazi maandamano, polisi wapange ratiba siku tofauti, sisi tutaandamana kumpinga waziri ili kama CCM wataandamana kumpongeza waziri wao wapangiwe siku yao, ila sisi tulitangaza mapema na barua tulipeleka kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.”
Alipoulizwa kwanini asisubiri Tume ya Waziri Mkuu itoe majibu, Mbowe alisema: “Hatuna shida na Tume ya Waziri Mkuu, matatizo ya elimu katika nchi yetu yapo wazi, tukizungumza bungeni wanatuchakachua, na sasa huku nje wanatukejeli, tunataka ifike mahali wajue kuwa nchi hii ni yetu sote, na Watanzania wanapaswa kusikilizwa kilio chao.”
Kwa mujibu wa Mbowe, maandalizi ya maandamano hayo yanayotarajiwa kufanyika katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Arusha na Dar es Salaam, yamekamilika.
Jana, Idara ya Habari (Maelezo) ilitoa barua iliyosainiwa na mkurugenzi wake, Assah Mwambene kuzuia maandamano yaliyokuwa yafanyike Jumatatu ijayo katika mikoa ya Mbeya na Arusha tu.
Taarifa hiyo haikuzungumzia maandamano yaliyopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam wala Mwanza.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, serikali ilisema kuwa maandamano ya CHADEMA yalipangwa kuhusisha wananchama kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na Ruvuma, na kuongeza kuwa CCM ilipanga kufanya maandamanno yake mkoani Arusha kupinga kusudio la CHADEMA kuandamana, wakieleza kwamba wana imani na tume maalumu ya Waziri Mkuu inayochunguza tatizo la kufanya vibaya wanafunzi wa kidato cha nne.
Awali CHADEMA walitangaza maandamano yatakayofanyika katika kanda nne. Kanda ya Kusini yatafanyika Mbeya; Kanda ya Ziwa yatafanyika Mwanza; Kanda ya Kaskazini yatafanyika Arusha, na Kanda ya Mashariki yatafanyika Dar es Salaam.
Tanzania Daima ilipomuuliza Mkurugenzi wa Maelezo imekuwaje yeye akawa msemaji wa jambo hili, alijibu: “Mimi ni msemaji wa serikali, hata Ikulu naisemea, hivyo usiulize kwanini naisemea polisi.”
Sababu nyingine iliyotolewa na serikali kupitia Maelezo ilisema ni kwa sababu siku hiyo ni muhimu kwa Watanzania kumpokea Rais mpya wa China ambaye atakuwa na ziara ya siku mbili nchini.
Februari 19 mwaka huu akiwa jijini Mwanza, Mbowe alitoa siku 14 kwa Waziri Kawambwa kujiuzulu kutokana na matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne.
Kauli hiyo ilitolewa siku moja baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kutangaza matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012 ambapo asilimia sitini ya wanafunzi wote waliofanya mtihani wamefeli.
Gazeti la- Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment