Thursday, March 7, 2013

MATOKEO YA UCHAGUZI KENYA: MFUMO WA ELEKRONIKI UMEKWAMA....ZOEZI LINAANZA UPYA

 Huku Wakenya wakiendela kusubiri kwa hamu kubwa kumjua mshindi wa kura ya urais kufuatia uchaguzi wa Jumatatu, wasiwasi unaongezeka baada ya kukwama kwa mfumo wa uwasilishaji matokeo kwa njia ya elekroniki.

Kufuatia hitilafu hiyo, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) imesema kwamba inategemea sasa matokeo yatakayowasilishwa na wasimamizi wa uchaguzi kutoka majimbo yote 290 kote nchini ili kuanza upya shughuli ya kujumlisha kura za urais.

“Maafisa wetu wa usimamizi wa uchaguzi wanatarajiwa kuleta matokeo rasmi wakati wowote kuanzia sasa. Tutaanza kutangaza matokeo rasmi kutoka maeneo bunge yote 290 kuanzia hapo kesho”. Alisema Mwenyekiti wa IEBC, Isaack Hassan, hapo jana jioni baada ya kukwama kwa mfumo wa kuwasilisha matokeo kwa njia ya elektroniki.

Hassan amedokeza kwamba idadi ya kura za urais zilizoharibika au kukataliwa zitajumuishwa na kura zote zilizopigwa ili kupata hesabu ya asilimia ya kura kwa kila mgombea.


                                                             Wafuasi wa muungano wa Jubilee.

“Kwa mujibu wa katiba jaduali la matokeo litarekebishwa kuonyesha asilimia ya kura kwa kila mgombea kuzingatia kura zilizopigwa.”

Ikiwa hilo litafanyika, inamaanisha kwamba hakuna mgombea atakayepata asilimia 50 ya kura zote na hivyo kupelekea kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi.

Hatua hiyo imezua wasiwasi mkubwa kwenye muungano wa Jubilee ambao mgombea wake, Uhuru Kenyatta, amekuwa akiongoza kwa asilimia 54 huku mpinzani wake Raila Odinga wa muungano wa CORD akiwa na asilimia 42 kufikia jana jioni.


“Sisi muungano wa Jubilee tuna wasiwasi. Kwani hatujui ni nini kimesababisha mabadiliko haya ya ghafla ya kukusanya matokeo na tunataka kuamini kwamba hii sio njama ya kuunyima ushindi wa muungano wa Jubilee kama inavyoonekana. Tunamtaka mwenyekiti wa tume uchaguzi atueleze." Alisema mgombea mwenza wa muungano huo, William Rutto.

Baadhi ya wagombea wamemiminika katika ukumbi wa Bomas kulalamikia kuchelewa kuwasilishwa kwa matokeoya kura ya urais. Pia kumekuwa na visa kadhaa vya udanganyifu vilivyoripotiwa kutoka vituo mbali mbali nchini.

Kinachosubiriwa sasa ni maafisa wasimamizi wa uchaguzi kuja na fomu za matokeo ya kura hiyo ili yajumuishwe kwa mkono na Tume iweze kutangaza rasmi matokeo ya kura ya urais.

No comments: