Wafanyakazi wa shirika la ndege, Fast Jet
Meneja wa wahudumu wa ndege za kampuni ya ndege ya Fastjet, Emma Donavan, amekamatwa na polisi, kuwekwa mahabusu na kuhojiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kumtolea lugha ya matusi mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Polisi walimshikilia na kumhoji Donavan kwa takribani saa tisa kuhusiana na tuhuma za kumtolea lugha ya matusi mfanyakazi huyo raia wa Tanzania.
Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Deusdedit Kato, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba meneja huyo alikamatwa jana saa 2:00 asubuhi kwa tuhuma za kumtukana mfanyakazi mwenzake, Samson Isembe, ambaye ni Ofisa Mwendeshaji wa kampuni hiyo.
Kamanda Kato alisema baada ya Donavan kukamatwa, alikataa kuhojiwa na polisi kwa sharti ya kuwako kwa mwanasheria wake ambaye aliwasili kituo cha polisi cha uwanja wa ndege saa sita baada ya mteja wake kukamatwa.
Mwanasheria wake aliwasili katika kituo hicho saa 8:30 mchana na taratibu za kuanza kumhoji zilianza saa 8:50 mchana na hadi saa 10:15 jioni alikuwa akiendelea kuhojiwa.
Kamanda Kato akisimulia mkasa huo, alidai kuwa juzi saa 10:00 jioni, Isembe alikwenda katika ofisi ya Donavan kuchukua nyaraka baada ya kutumwa na afisa mwenzake.
Alidai kuwa baada ya mtuhumiwa kumkuta Isembe akifungua mlango wa ofisi yake, ndipo alianza kumtolea matusi ya nguoni.
Isembe alidai kuwa kwa kuwa ilikuwa majira ya jioni hakuweza kuchukua hatua zozote hadi jana alipokwenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi.
“Taarifa zilizopofikishwa polisi, askari wa zamu walikwenda kumkamata meneja huyo na walipoanza kumhoji kutokana na tukio hilo alikataa kutoa maelezo akidai kuwa mpaka awepo mwanasheria wake,” alisema Kamanda Kato.
Kamanda Kato alisema polisi wameanza uchunguzi wa tukio hilo na baada ya kukamilisha watachukua hatua za kumpeleka mahakamani meneja huyo ambaye aliachiwa saa 11:00 jioni kwa dhamana.
Awali Ofisa mmoja wa polisi katika kituo hicho (jina limehifadhiwa) aliiambia NIPASHE kuwa meneja huyo alimtolea mlalamikaji matusi ya nguoni ambayo hayafai kuandikwa gazetini.
Alisema baada ya kupewa taarifa hizo, askari walikwenda kumkamata meneja huyo saa 2:00 asubuhi na kumuweka rumande hadi saa 8:50 mchana alipoanza kuhojiwa mbele ya mwanasheria wake.
Mwanasheria mmoja alisema kumtukana mtu linaweza kuhesabika kosa kama kuna ushahidi wa watu wengine waliosikia wakati mlalamikaji anatukanwa.
Alisema kwa upande mwingine kama mlalamikaji alitukanwa akiwa peke yake, ushahidi utakosekana na hivyo siyo rahisi kwa mlalamikiwa kupatikana na hatia.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment