Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 4, 2013, katika Ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jana Aprili 3, 2013, mmoja wa Viongozi wa ngazi ya juu wa Chadema alitoa tuhuma dhidi ya Chama Cha Mapinduzi kuwa kupitia kampuni ya Chama ya Jitegemee Trading Company, CCM imeingia mkataba na Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) kwenye mradi wa upanuzi wa Bandari kavu kwa kutumia eneo la SUKITA lililopo maeneo ya makutano ya barabara ya Kawawa na Mandela ambalo ni mali ya CCM.
Tuhuma hizi zimechapishwa leo na baadhi ya vyombo vya habari na hasa TanzaniaDaima zikidai “Chadema wameibua unaoitwa ufisadi wa Mwakyembe wa kuipa CCM zabuni ya kupanua bandari”.
Kiongozi huyo wa Chadema alikwenda mbali kwa kuishutumu Wizara ya Uchukuzi na Waziri wake Dokta Harrison Mwakyembe kwa madai ya kukiuka taratibu na kutoa zabuni ya upanuzi wa bandari ya Dar es salaam kwa CCM kinyume na taratibu za manunuzi jambo ambalo ni uongo.
Ukweli ni kwamba Kampuni ya Jitegemee Trading Company ni mali ya CCM, na pia ni kweli kuwa kiwanja kilichotajwa ni mali ya CCM kilichokombolewa kutoka zilizokuwa mali za SUKITA ambayo pia ilikuwa kampuni ya CCM.
Lakini TPA na Jitegemee mpaka sasa hawajaingia mkataba wowote. Eneo hilo limeombwa na wawekezaji wengi wakiwemo TPA na masharti waliyopewa waombaji wote ni kuleta mapendekezo ya mipango yao ya kibiashara kabla ya kufikia uamuzi wa nani anawekeza kwa ubia na Jitegemee kwenye eneo hilo.
Wanachokiita wenzetu wa Chadema kuwa ati ni zabuni iliyotolewa kwa kampuni ya Jitegemee na Mamlaka ya Bandari ni barua ya TPA kwenda Jitegemee wakiomba ridhaa ya kushirikiana kuliendeleza Eneo la kampuni hiyo ya Jitegemee lenye ukubwa wa zaidi ya ekta 100, katika mfumo wa ushirikiano yaani "Joint Venture" kupitia utaratibu wa PPP (Public, Private Partnership) jambo ambalo ni la kawaida sana kwani linafuata utaratibu na sheria zote husika.
Kama nilivyokwisha kusema Chama Cha Mapinduzi kinamiliki Kampuni ya Jitegemee, na kwamba pamoja na umiliki huo, kampuni hiyo imekuwa ikitekeleza shughuli za uwekezaji kwa muda mrefu kwa kufuata taratibu zote na sheria za nchi kwa ujumla.
Tunatambua kuwa Chadema kwasasa wanapitia wakati mgumu sana kisiasa kutokana na kuanza kuvuna walichopanda kwa muda mrefu katika siasa za nchi yetu.
Lakini pia tunatambua tabia ya viongozi wa Chama hicho ya kudandia kila gari linalopita bila kujua linakokwenda kwa kugeuza kila kinachofanyika nchini, ilimradi hakifanywi na wao basi ni haramu.
Hata hivyo mazingira haya wanayopitia hayawapi uhalali wa kuwa wavivu wa kufikiri kiasi cha kushindwa kutofautisha barua ya maombi ya kushirikiana kuendeleza eneo na mkataba!.
Aidha mazingira wanayopitia kwasasa hayawapi uhalali wa kuwa wavivu wa kufikiri kiasi cha kushindwa kujua kuwa kinachofanyika ni mawasiliano ya awali sana ya kusudio la kuendeleza eneo husika na hakuna taratibu zilizokiukwa.
Umbumbumbu wa aina hii unatia mashaka sana juu ya uwezo wao wa kufikiri na kupambanua mambo. Jambo moja wanaloonekana kulimudu ni uwezo wao wa kutunga uongo na kupanga machafuko. Na hii ndio siri ya watanzania kuwakataa kila kukicha na ndio siri ya kufa kwa chama hicho, kwani njia ya muongo ni fupi.
Lakini tunazo taarifa kuwa uongo huu wamelishwa na baadhi ya mafisadi waliotaka kutumia eneo hili la CCM kujaribu kukaa katikati ya mwekezaji yeyote atakayejitokeza na Jitegemee kwa lengo la kujinufaisha wao binafsi. Na huu ni mwendelezo wa Chadema kutumiwa na mafisadi katika kutimiza mambo yao. Kutumika huku kunasukumwa na kiu yao ya kushika dola kwa gharama yoyote. Watanzania tuwapuuze na kuwaepuka.
CCM inachukua nafasi hii kuipongeza Wizara ya Uchukuzi kwa kazi nzuri inayoendelea kuifanya chini ya Dr. Harrison Mwakyembe hasa ya kuongeza ufanisi kwenye bandari yetu ya Dar es salaam. Tunawataka wasikatishwe tamaa na mafisadi wachache, wachape kazi kwa uzalendo huohuo waliouonesha.
Imetolewa na:-
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
ITIKADI NA UENEZI
04/04/2013
No comments:
Post a Comment