Tuesday, April 30, 2013

LEMA ASEMA HAYA BAADA YA KUACHIWA MAHAKAMANI KWA DHAMANA

 Mbunge wa jimbo la Arusha mjini Godbless lema ameachiwa huru kwa dhamana na mahakama ya hakimu mkazi baada ya kusota rumande kwenye kituo kikuu cha polisi kwa siku tatu  kwa kosa la kuchochea vurugu chuoni uhasibu huku baada ya kutoka akiwataka wanachama na wapenzi wa chama hicho kumzomea mkuu wa mkoa.

Lema alifikishwa mahakamani hapo majira ya saa Tatu na robo asubuhi akiwa chini ya ulinzi wa polisi na kufikishwa mbele ya hakimu Devotha Msele  na ndipo mwendesha mashtaka Eliang’enyi Njiro alisimama kuanza kumsomewa mashtaka ya uchochezi na kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani aliyoyafanya kwenye eneo la chuo cha uhasibu njiro jijini Arusha.

Baada ya kutoka mahakamani hapo alielekea kwenye ofisi za chama hicho na kuzungumza na waandishi wa habari huku akitoa malalamiko na kuwataka wanachama na wapenzi wa chadema kumzomea mkuu wa mkoa iwe kanisani,mskitini,au kwenye sherehe mbali mbali,

“Nawatakeni kumzomea huyo mkuu wa mkoa Magessa Mulongo na kuwa nia ya kumshtaki ipo pale pale ndugu zangu Makamanda wenzangu huyu jamaa awe msikitini kanisani kote tumzome hiyo itakuwa ndiyo salamu yetu kwake”alisema Lema

Katika hali nyingine jeshi la polisi liliimarisha ulinzi tangu nje ya mahakama hadi ndani ya mahakama hiyo kiasi utulivu katika mahakama hiyo ulionekana na shughuli kuendelea bila bughaa.

Hali kwenye mitaa mbali mbali ya viunga vya jiji la Arusha ilionekana kuendelea na mishughuliko ya kila siku kama kawaida kuliko ilivyokuwa ikionekana huko mwanzo kwenye kesi zilizokuwa zikimkabili mbunge huyo kwa wakazi wa jiji hili kuacha shughuli zao na kuelekea mahakamani kufuatilia kesi ya mbunge huyo.

No comments: