Thursday, June 20, 2013

"NASSARI NI MUONGO NA NI MNAFIKI, TUMEMRUHUSU KWA AMANI NA BADALA YAKE KADAI ETI KATOROKA ILI TUSIMUUE"...KAULI YA DAKTARI

 UONGOZI wa hospitali ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ya Selian jijini Arusha umekanusha vikali taarifa zilizotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema John Mnyika kuwa serikali ilipeleka maafisa wa usalama hospitalini hapo kwa lengo la kumdhuru mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki Joshua Nassari pamoja na majeruhi wa mabomu waliolazwa katika hospitali hiyo na kusema ni uzushi mtupu.

Mnyika alisema kufuatia kitendo hicho mbunge Nassari alipiga kelele (yowe) akiwa katika korido ya wodi namba 14 aliyokua amelazwa ili kuomba msaada baada ya maafisa hao wa usalama waliokua wamevalia mavazi ya kitabibu na kubeba vifaa vya kitabibu kumtundikia drip aliyohisi ilikua na lengo la kumdhuru ambayo aliitoa na kuitupa.

Mnyika alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya mahakama kuu kanda ya Arusha wakati akisubiri wabunge wanne wa chama chake pamoja na wafuasi wao waliohusika na mkusanyiko usio halali katika viwanja vya Soweto jijini Arusha juziKwa mujibu wa Mnyika, kufuatia hali hiyo Nassari aliamua kutoroka usiku wa kuamkia jana  na kutokomea pasipojulikana ili kujinusuru maisha yake na kwamba Chadema baada ya kupata taarifa hiyo imeamua kumtafutia mbunge huyo hospitali nyingine itakayomtibu kwa gharama za chama hicho.

Pia Mnyika alisema mbali na tukio hilo pia polisi kwa kushirikiana na madaktari wa hospitali hiyo wamekuwa wakiwaruhusu majeruhi wa tukio la mlipuko wa bomu kwenda majumbani kwao kabla ya kupata naafuu ikiwa ni hatua ya kupoteza ushahidi wa tukio hilo.

“Nassari amelazimika kutoroka hospitalini pale jana usiku baada ya kutundikiwa drip na watu tunaowajua ni maafisa usalama waliokuwa na lengo la kummaliza ambapo  aliitoa na kisha kuanza kupiga yowe katika korido ili kuomba msaada na alifanikiwa kutoroka sasa tutmtibu sisi wenyewe”alisema Mnyika.

Mnyika aliwataja maofisa usalama hao kuwa John Ngowi na Flugence Mark ambao wamekuwepo hospitalini hapo kwa siku kadhaa wakitoa huduma kwa majeruhi wa ajali ya mlipuko wa bomu lililosababisha vifo vya watu nne na kujeruhi zaidi ya 70.

Akijibu tuhuma hizo Kaimu mganga Mkuu wa hospitali hiyo Paul Kisanga alisema si kweli kwamba mbunge huyo alitoroka hospitalini hapo bali alipewa ruhusa katika hali ya kawaida baada ya kuonekana hana tatizo lolote linalomsumbua tangu kufika hospitalini hapo.

Dk.Kisanga alisema mbunge huyo alipewa ruhusa hiyo siku ya Jumanne majira ya saa 9.30 alasiri bila kuwa na malalamiko yoyote kuhusu kutaka kudhuriwa na madaktari anaowadai kuwa ni maafisa usalama waliotumwa na serikali.

Aidha alisema mbunge huyo katika kuondoka kwake hakuwa na masharti yoyote kuwa anahitaji kupata uhamisho wa kwenda katika hospitali nyingine yoyote kwa matibabu zaidi kwakua hata alipotembelewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda alimweleza wazi kuwa afya yake imeimarika.

“Mimi namshangaa Nassari kama kweli ametoa tuhuma hizo .Sisi tumemruhusu baada ya kusema kuwa anaona afya yake imeimarika na hata mbele ya waziri mkuu aliyasema hayo na kwanini hakuyasema hayo kwa uongozi wa hospitali kabla huu ni uzushi”..alisema Dk.Kisanga.

Wakati huo huo, Kaimu mganga huyo alisema mtoto Fahali Jamali(7)aliyekua melazwa katika chumba cha ungalizi maalumu(ICU)tangu siku ya tukio amefariki dunia jana saa saba mchana kufutia hali yake kuwa mbaya zaidi.

Dk.Kisanga alisema marehemu Fahali alifariki dunia kufuatia majeraha makubwa kichwani yaliyosababisha matundu matatu aliyoyapata kutokana na kulipukiwa na bomu siku ya tukio hilo.
Aliongeza kuwa mara baada ya marehemu huyo kufariki mwili wake ulichukuliwa na jeshi la polisi pamoja na mzazi wake hadi katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru kwaajili ya uchunguzi zaidi kabla ya taratibu za maziko kufanyika.

No comments: