Tuesday, July 31, 2012

BALOZI WA PAPA NCHINI TANZANIA ATOA SAKRAMENT YA KIPAIMARA KWA MARA YA KWANZA KATIKA KANISA LA MT. PETRO OYSTERBAY

 Balozi wa baba Mtakatifu hapa nchini, Askofu Mkuu Fransisko Montecillo Padilla, akimpaka mafuta ya kipaimala Theodory Helon,  wakati wa ibada ya Sakaramenti ya kipaimara iliyofanyika katika kanisa la Mtakatifu Petro Osyterbay jijini Dar es Salaam jana. Jumla ya watoto 72 walipata sakramenti hiyo, kushoto ni mzazi wa kiroho  wa mtoto huyo, Daniel Mwisongo.
 Balozi wa baba Mtakatifu hapa nchini,  Askofu Mkuu Fransisko Montecillo Padilla, akimkabidhi Aivan Catrece, zawadi ya msalaba  wakati wa ibada ya Kipaimara iliyofanyika katika kanisa la mtakatifu Petro Osyterbay jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya watoto kati ya 72 waliopata sakaramenti ya kipaimara wakionyesha vyeti vyao baada ya kukabidhiwa na Balozi wa baba Mtakatifu hapa nchini Askofu Mkuu Fransisko  Padilla, wakati wa ibada hiyo iliyofanyika katika kanisa la Mtakatifu Petro Osytarabay jijini Dar es Salaam.
 Balozi wa baba Mtakatifu hapa nchini Askofu Mkuu Fransisko Montecillo Padilla, akikabidhiwa zawadi ya mbuzi na Catrece Theodory ambaye ni mmoja wa wajumbe wa kamati wakati wa Ibada ya kipaimara iliyofanyika jana katika kanisa la mtakatifu Petro oysterbay jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Paroko wa parokia hiyo Joseph Mosha.
 Balozi wa baba Mtakatifu hapa nchini Askofu Mkuu Fransisko Montecillo Padilla, akiwahutubia watoto wa kipaimala  wakati wa ibada ya sakaramenti iliyofanyika katika kanisa la mtakatifu Petro Osyterbay jijini Dar es Salaam, Jumla ya watoto 72 walipata ekaristi hiyo.
 Balozi wa baba Mtakatifu hapa nchini Askofu Mkuu Fransisko Montecillo Padilla, akitoa baraka kwa waumini wa kanisa la Mtakatifu petro Oysterbay wakati wa Ibada ya Kipaimara,Askofu huyo ilikuwa mara yake ya kwanza kuongoza ibada katika kanisa hilo ambapo alisalimiana na waumini wote kwa kuwapa mikono na baraka.
Balozi wa baba Mtakatifu hapa nchini Askofu Mkuu Fransisko Montecillo Padilla, akitoa baraka kwa waumini wa kanisa la Mtakatifu petro Oysterbay wakati wa Ibada ya Kipaimara,Askofu huyo ilikuwa mara yake ya kwanza kuongoza ibada katika kanisa hilo ambapo alisalimiana na waumini wote kwa kuwapa mikono na baraka.
Mmoja wa watoto waliopta sakaramenti ya kipaimara katika kanisa la Mtakatifu Petro, Aivan Catrece, akionyesha kipaji chake cha kupiga ngoma wakati wa Ibada hiyo.

Kizaazaa Cha Mgomo Wa Walimu Manispaa Ya Singida...!

Wanafunzi wa shule ya msingi Ipembe, Nyerere, Unyankindi na Singidani ktk Manispaa Singida

Na: Elisante John Singida.
Julai 30,2012.

MGOMO Uliondaliwa na CWT nchini, umeleta madhara katika Manispaa Singida, baada ya wanafunzi wa shule za msingi kuandamana hadi ofisi ya RC leo.

Kwenye maandamano hayo, watoto wa shule ya msingi Nyerere, Singidani, Ipembe na Unyankindi, walitembea kilomita tatu hadi ofisi ya Mkuu Mkoa, huku barabarani wakiimba ‘tunataka haki zetu, walimu wamegoma, tunataka haki zetu’.

Baada ya askari polisi kubaini usalama wa watoto hao upo hatarini, waliingilia kati na kuongoza maandamano hayo hadi ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Wanafunzi hao zaidi ya 600 walijazana katika uwanja wa mbele, jengo la Mkuu wa Mkoa kuanzia saa tatu hadi saa 4:30 asubuhi.

Hatimaye Serikali ya Mkoa kupitia katibu wa tume idara ya Utumishi wa walimu Samweli Ole Saitabau, aliwataka kurudi nyumbani hadi kesho, wakaendelee na masomo katika shule zao.

Zitto Ahojiwa Kwa Rushwa

SAKATA la wabunge kuhusishwa na rushwa limeingia sura mpya, baada ya Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe kuhojiwa na chama chake cha Chadema kwa saa tatu jana.
Wakati Zitto akihojiwa, kambi rasmi ya upinzani bungeni, iliwataja wabunge saba wa CCM na kueleza kuwa ndiyo wanaolichafua Bunge kwa kujihusisha na mambo yenye maslahi binafsi wakiwa watumishi wa umma.

Kadhalika, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) ilikuwa ikiendelea kuwahoji baadhi ya wabunge kuhusu tuhuma za rushwa na kwamba uchunguzi ukikamilika taarifa zitawekwa wazi.

Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, jana aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Tweeter kwamba alihojiwa na Sekretarieti ya chama chake kutokana na tuhuma za rushwa zinazowagusa badhi ya wabunge.
Katika maelezo yake, Zitto alisema aliiambia sekretarieti ya chama hicho kwamba Chadema kifanye uchunguzi ili kubaini ukweli wa suala hilo na kwamba yuko tayari kuwajibika ikiwa itathibitika kwamba alihusika kula rushwa.

“Kwa saa tatu nimejieleza mbele ya sekretariati ya chama kuhusu tuhuma za rushwa dhidi yangu. Niliomba kutaka kutoa maelezo kwa Katibu Mkuu, nimekiomba chama kufanya uchunguzi na ikibainika hatua zichukuliwe,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo kwenye Tweeter.

Lissu ataja wengine
Kwa upande wake, Mnadhimu Mkuu wa kambi hiyo, Tundu Lissu aliwataja wabunge wa CCM ambao wanatuhumiwa kuwa ni Nasir Abdallah (Korogwe Mjini), Mariam Kisangi (Viti Maalumu), Vicky Kamata (Viti Maalumu) na Charles Mwijage (Muleba Kaskazini) ambao hata hivyo, wote wamekanusha madai hayo.

Habari zaidi:  http://www.mwananchi.co.tz/habari

Gazeti La Mwanahalisi Lafungiwa

                                          JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
                              WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO


                                                           TAMKO LA SERIKALI
                                         GAZETI LA MWANAHALISI LAFUNGIWA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelifungia kutochapishwa gazeti la MwanaHalisi kuanzia 30 Julai, 2012 kwa muda usiojulikana kutokana na mwenendo wake wa kuandika habari na makala za uchochezi, uhasama na uzushi likiwa na nia ya kusababisha wananchi kukosa imani na vyombo vya dola hali inayoweza kuhatarisha amani na mshikamano uliopo nchini.

Katika matoleo yake hivi karibuni, gazeti la MwanaHalisi toleo Na. 302 la Jumatano Julai, 11 – 18, 2012 na toleo Na. 303 la Jumatano Julai 18 – 24, 2012 na toleo Na. 304 la Jumatano Julai 25 hadi 01 Agosti, 2012 na mengine yaliyotangulia yamekuwa yakichapisha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii.

Mhariri wa gazeti la MwanaHalisi, ameitwa na kuonywa mara nyingi, lakini hataki kukiri kuwa maudhui ya makala zake hazina tija kwa jamii, pia hazifuati weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.
   
Mhariri, mara zote katika utetezi wake amekuwa akinukuu kifungu cha 18 cha Katiba ya nchi yetu ambacho kinatoa uhuru wa kutoa maoni na kwa makusudi kutonukuu kifungu cha 30 cha Katiba hiyo kinachoweka ukomo wa uhuru.

Uamuzi wa Serikali

Serikali imeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi, kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu Na. (25) (i), adhabu hiyo itaanza tarehe 30 Julai, 2012 kwa mujibu wa Tangazo la Serikali (Government Notice) Na. 258 lililochapishwa katika Gazeti la Serikali na kutolewa jijini Dar Es Salaam tarehe 27 Julai, 2012

Serikali inawataka wamiliki, wahariri na wanahabari kuzingatia sheria, uzalendo, weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari katika kutekeleza wajibu wa kuhabarisha, kuelimisha na kutoa burudani kwa wananchi.

Kama ilivyoelezwa Bungeni wakati wa kuwasilisha Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo hivi karibuni waandishi na watangazaji wa habari wanatakiwa kuhakikisha kuwa habari wanazoziandika na vipindi wanavyoandaa vinazingatia  taaluma na kuweka mbele maslahi ya Taifa letu na uzalendo. Uhuru na haki ya vyombo vya habari uendane na wajibu.

Kuanzia sasa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya vyombo vya habari ambavyo kwa maksudi vitatoa taarifa za uchochezi ambazo zitahatarisha hali ya amani na utulivu uliopo nchini mwetu.
Imetolewa na

OFISI YA MSAJILI WA MAGAZETI
WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
30 Julai, 2012

TAARIFA ZA MIKOA TOFAUTI KUHUSU MGOMO WA WALIMU PAMOJA NA KAULI YA WAZIRI.

Chama cha walimu Tanzania kimeanza mgomo wa walimu nchi nzima july 30 2012 ambao unatokana na walimu laki moja na elfu 53 kuukubali.

Ishu imekua nzito baada ya kushindwa kupata kile walichotaka kwa serikali ndani ya siku 30.

Wanachotaka ni kulipwa malimbikizo, ongezeko la mishahara kwa asilimia 100, posho za kufundishia kwa walimu wa sayansi asilimia 55 na walimu wa sanaa asilimia 50 na posho za mazingira magumu kwa asilimia 30.

Shinyanga walimu waliendelea na kufundisha kama kawaida, ambapo walimu wengi wakuu wamesema hawana taarifa zozote za kuanza kwa mgomo, yani hawakuambiwa chochote na bado wanaendelea na kazi.

Dar es salaam shule nyingi kumekua na mgomo mfano Mbezi Luis ambako wanafunzi walikwenda hadi kituo cha polisi Mbezi Luis kwa maandamano.

Kwenye mkoa wa Tanga shule kadhaa zimeonekana kuwa kimya huku wanafunzi wakiwa wenyewe shuleni, walimu wamegoma na wanafunzi kubaki kucheza tu na wengine wakarudi nyumbani.

Kwenye mkoa wa Pwani mgomo ulikuepo ambapo kwenye shule ya Mkoani wanafunzi walikua nje baada ya walimu kuondoka ambapo mwandishi wa habari Victor kasema kwenye shule ya Mtongani Mlandizi wilayani Kibaha ilikua kimya na imefahamika walimu waliwachapa wanafunzi walioingia darasani.

Amesema kwenye shule ya msingi Maili Moja mgomo ulikuepo ambapo baadhi ya wanafunzi walikua wakipiga mawe kwenye ofisi za walimu ambazo milango yake ilikua imefungwa, walimu hawajafanya chochote toka asubuhi.

Singida na Mbeya pia kumekuwepo na mgomo, kwa upande wa Mbeya kwa mujibu wa mbeyayetu Blog kuna vurugu kubwa ambayo mpaka Polisi waliingilia na kupiga mabomu ya machozi kutawanya wanafunzi walioandamana kushinikiza walimu wawape mitihani kabla ya kufunga shule.

Pamoja na hizo taarifa zote za mgomo, Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi Dr Shukuru Kawambwa amesema mgomo huo ni batili lakini Serikali inawahakikishia walimu ambao hawajajihusisha na mgomo kwamba Serikali na vyombo vya usalama vitawalinda na kuwahakikishia usalama wao.

Amesema “tunawatahadharisha Walimu wote ambao wamegoma na wamekua wakiwatishia maisha walimu wengine ambao hawako kwenye mgomo, atakaebainika hatua za kisheria zitachukuliwa”

KAULI ZA BAADHI YA WABUNGE KUHUSU RUSHWA BUNGENI.

Baada ya kuwepo malalamiko ya rushwa kutembea bungeni na kusababisha kuvunjwa kwa kamati ya kudumu ya bunge ya Nishati na Madini mwishoni mwa wiki iliyopita, baadhi ya Wabunge wametaka majina ya wenzao wanaojihusisha na rushwa yawekwe wazi na wafukuzwe bungeni.

Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari (CHADEMA) amesema pamoja na kwamba kamati ya nishati na madini imetajwa moja kwa moja, zipo kamati nyingine ambazo wabunge wake wanatajwa kuhusika na kuomba rushwa.

Amesema “zipo kamati kadhaa zinatuhumiwa kwa rushwa, Mh Spika nilikua naomba muongozo wako kwamba kwa nini ofisi yako isiamue kuzivuruga kamati kadhaa ambazo zinatuhumiwa kwa rushwa ikiwemo kamati ya kudumu ya bunge ya Serikali za mitaa inayoongozwa na Mh. Mrema na Kamati ya kudumu ya bunge ya Mashirika ya Umma inayoongozwa na Mh. Zitto Kabwe, hii ni kwa sababu wabunge wengi wamekua wanazikimbilia zile kamati ambazo zina mikataba lakini kamati kama ya maendeleo ya jamii ya huduma za jamii ambazo zina umuhimu mkubwa kwenye nchi kwa sababu hazina mikataba zinakimbiwa”

Mbunge wa Lindi mjini Salum Khalfan na mbunge wa Nkasi kaskazini Ally keissy Mohamed wamelitaka bunge kuwafukuza bungeni wabunge wote watakaogundulika kula rushwa, wanataka watajwe kwa sababu sasa hivi wabunge wengine kila wakipita barabarani wanakosa raha kutokana na hiyo kashfa ya rushwa iliyolichafua bunge.

Baada ya hayo Naibu Spika wa bunge Job Ndugai aliomba kamati ya uongozi wenyeviti wa kamati za bunge kukutana na Spika kulizungumza ili baadae wampe maelekezo zaidi.