Saturday, January 5, 2013

walionunua ving'amuzi star times waambiwa wavirejeshe

KAMPUNI ya Star Media Tanzania Ltd (Startime) imewataka watu ambao wamenunua ving’amuzi na kubaini kuwa havifanyi kazi kuvirejesha kwenye ofisi zao ili wapatiwe vingine.
Vilevile wamewataka wale waliouziwa kwa bei ya kulangua wafike kwenye ofisi zao pamoja na risiti walizonunulia ili hatua zinazofaa ziweze kuchukuliwa.

Hatua hiyo inatokanana malalamiko ya wananchi siku chache tangu kuanza kutumika kwa mfumo wa dijitali wa kurusha matangazo ya runiga.

Malalamiko hayo yanayolalamikiwa na kampuni hiyo ni kuhusiana na kushindwa kuonekana kwa baadhi ya chaneli licha kufunga king’amuzi kwenye Televisheni

Baadhi ya wakazi jijini Dar es Salaam wamelalamikia huduma za ving’amuzi zitolewazo na kampuni ya Star Media (Tanzainia) Limited kuwa wameshindwa kutoa huduma iliyokusudiwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na jijini jana, wakazi hao walisema kuwa kumekuwa na matatizo ya picha na sauti katika matangazo yao na hivyo wameitaka kampuni hiyo kutoa elimu zaidi juu ya ving’amuzi hivyo ili watumiaji waweze kufaidika na huduma hiyo.

Walisema tangu mfumo huu mpya uanze wamekuwa hawatumii king’amuzi hicho kutokana na matangazo mengi kuonekana kukwama na vingine kutopata sauti vizuri.
Mmoja wa wananchi hao, Tatu Omary mkazi wa mbezi alisema kuwa amashangazwa na baadhi ya vituo kupotea bila kupata taarifa zozote huku akitolea mfano wa kituo cha Clouds ambacho tangu kuanza kwa mfumo mpya matangazo yake hayaonekani katika king’amuzi hicho.

Naye Ramadhani Abdalla ambaye ni fundi umeme alisema kuwa bei za ving’amuzi bado ziko juu ukilinganisha na kipato cha wananchi ingawa Serikali imesema wamepunguza kodi ili ving’amuzi vishuke bei.

Akijibu malalamiko hayo jana mbele ya waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Star Media, William Lan alisema kuwa matatizo mengi wanayoyapata wananchi ni kutokana na kushindwa uunganishaji wa antena kama inavyotakiwa.
Alisema kuwa wakati wa kuunganisha antena zinapaswa kuelekezwa kwenye mitambo yao ambayo kwa sasa iko Kisarawe mkoa wa Pwani.

Alisema kuwa katika kutatua tatizo hilo wanatarajia kujenga kituo cha kurushia matangazo cha kisasa katika maeneo ya Makongo Kilimani.

Awali, Meneja Mauzo wa Kampuni hiyo, David Kisaka alilaumu vikali baadhi ya mawakala wao wanaopandisha bei za ving’amuzi kwa faida zao.
Alisema kuwa kitendo hicho hakiharibu jina la kampuni yao kwenye soko tu bali pia kina waumiza wateja wao kwa kiasi kikubwa.

Alisema Star Times imefanya punguzo la bei ya ving’amuzi vyake kwa bei ya Sh39,000 badala ya Sh70,000.“Kama kuna mtu ameuziwa king’amuzi kwa bei ambazo zipo juu ya bei zetu atoe taarifa kwenye ofisi zetu,” alisema Kisaka.

Alifafanua kuwa kwa sasa dekoda moja yenye kifurushi cha mambo kitauzwa kwa bei ya Sh48,000, dekoda yenye kifurushi cha Uhuru kitauzwa kwa Sh53,000 wakati kile chenye kifurushi cha Kili kitauzwa kwa Sh62,000.


No comments: