Nyosso.
BEKI wa Simba SC Juma Said Nyosso amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kuichezea klabu hiyo baada ya mkataba wake mwanzo kumalizika hivyo kumaliza tetesi kwamba anaweza kuhamia kwa watani wa jadi, Yanga SC.
Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ameiambia blog ya BIN ZUBEIRY kwamba Nyosso alisaini mkataba huo Julai 1 mwaka huu.
Kaburu alisema kwamba Simba ina imani na beki huyo wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na ndio maana imemuongezea mkataba.
Aidha, Kaburu aligusia suala la beki wao, Kelvin Yondan aliyehamia kwa watani wa jadi Yanga akisema bado ni mchezaji wao halali na wameshapeleka malalamiko yao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wanasubiri majibu.
Kuhusu Tetesi za Emmanuel Okwi kuhamia Yanga kama ilivyoandikwa na magazeti kwamba amesaini mkataba usiku wa manane, Kaburu amekanusha hizo taarifa kwenye kikao na wanahabari ambapo alimpigia simu Okwi na kumuweka loudspeaker na wote kumsikia akikanusha ambapo kwa sasa anajiandaa kwenda kufanya soka la majaribio Italy.
Kaburu pia amesema mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Felix Sunzu tayari amejiunga na wenzake kambini visiwani Zanzibar, ambako timu hiyo inashiriki Kombe la Urafiki.
Kaburu amesema Simba itaendelea kuwa Zanzibar hata baada ya michuano hiyo, wakijiandaa na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, ambalo linatarajiwa kuanza kutimua vumbi Julai 14, Simba wakifungua dimba na URA ya Ugandea Julai 16.
No comments:
Post a Comment