KOCHA mpya Yanga, Tom Saintfiet aliyeingia mkataba wa kufundisha klabu hiyo ya Jangwani, atavuna Sh288 milioni iwapo mkataba wake hautaishia njiani.
Katika kipindi cha miaka mitano, Yanga imekuwa na makocha tofauti, baadhi wakishindwa kudumu klabuni kama mikataba yao ilivyokuwa ikielekeza.
Makocha waliofundisha Jangwani tangu 2007 na kuondoka kwa sababu mbalimbali, nyingi kutokana na kushindwa kutekelezwa kwa makubaliano ni Milutin Sredojovic, Dusan Kondic, Kostadin Papic na Sam Timbe.
Hata hivyo, Papic aliyekuja nchini mara ya kwanza mwaka 2009, alirejea mwaka jana baada ya Timbe aliyeipa jangwani taji la Ligi Kuu na Kombe la Kagame kutimuliwa.
Katikati ya wiki iliyopita Kocha, Saintfiet raia wa Ubelgiji
aliingia mkataba wa miaka miwili kuifundisha Yanga kwa mshahara wa Sh12 milioni.
Ina maana, katika kipindi cha mwaka mmoja, Saintfiet aliyetamba kuleta mafanikio Jangwani, tavuva Sh144 milioni.
Mshahara huo unamzidi kwa Sh730,000 kocha aliyeondoa muda mfupi baada ya kumalizika kwa msimu, Kostadin Papic kutoka nchini Serbia.
Habari za uhakika toka ndani ya klabu hiyo zimedaiwa kupanda kwa mishahara ya wachezaji, ambapo wa chini utakuwa Sh800,000 na wa juu Sh1.5milioni.
Micho ambaye sasa ni Kocha wa timu ya taifa ya Rwanda (Amavubi), aliondoka nchini baada ya timu hiyo kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Ndogo mwaka 2007.
Mtihani wa kwanza wa Saintfiet katika utekelezaji wa ahadi yake ya kuleta mafanikio, Jangwani unaanza leo kwa mechi ya kirafiki dhidi ya JKT Ruvu
Yanga inashuka Uwanja wa Taifa kupambana na maafande hao katika mchezo wenye sura ya maandalizi kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame inayoanza Jumamosi wiki hii.
Lakini pia Bosi, Saintfiet ataitumia mechi hiyo kuwachambua wachezaji wake walioonyesha uwezo ili aweze kujenga mhimili wa kikosi cha kwanza.
Kwenye kikosi hicho kuna wachezaji wengi wameonyesha uwezo jambo ambalo ni wazi litampa wakati mgumu kuchagua kikosi cha kwanza.
Kumekuwa na ushindani mkubwa kwenye kikosi hicho chenye mchanganyiko wa wachezaji na chipukizi kadhaa wapya kama Frank Domayo, Simon Msuva na David Luhende.
Domayo na Msuva wametishia nafasi za wakongwe kama Nurdin Bakari, Juma Seif na Hamis Kiiza baada ya kuonyesha kiwango kikubwa katika pambano la kirafiki dhidi ya Express ya Uganda hivi karibuni.
Naye Luhende anayecheza nafasi beki ya kushoto ameonekana kumkuna Saintfiet baada ya kutisha katika mazoezi ya timu hiyo hivu karibuni, hivyo kuwafanya wapinzani wake wa nafasi hiyo Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua na Godfrey Taifa kuwa mtegoni.
Nayo JKT ambayo msimu uliopita ilishindwa kutamba itautumia mtanange huo kama sehemu ya kuona makali yake kabla ya kuingia katika hekaheka za Ligi Kuu msimu ujao.
No comments:
Post a Comment