Thursday, August 16, 2012

KAULI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU MAJINA YA WALIOWEKA FEDHA USWIS.

Kambi rasmi ya upinzani bungeni imesema italazimika kuweka wazi taarifa na majina ya watu wenye umiliki wa fedha katika benki nchini Uswis zinazofikia bilioni 315.5 kama serikali haitatoa hizo taarifa.

Waziri kivuli na msemaji mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni Wizara ya fedha na uchumi Zitto Kabwe amesema hizo fedha zililipwa na makampuni ya utafutaji mafuta na gesi kwenye pwani ya mkoa wa Mtwara, kampuni ambazo zilipewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.

Nimemkariri Zitto akiongea bungeni kwamba “kambi rasmi ya upinzani bungeni imepata taarifa kuwa mmoja wa viongozi wa juu kabisa wa Tanzania na baadhi ya mawaziri wa serikali ya awamu zilizopita ni miongoni mwa wamiliki wa fedha hizi, sehemu kubwa ya fedha zililipwa na kampuni za utafutaji wa mafuta na gesi katika pwani ya mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006, kambi rasmi ya upinzani inaitaka serikali kutoa taarifa rasmi ya hatua gani ambayo imechukua mara baada ya kutolewa kwa taarifa kutoka benki ya taifa ya Uswis, tunaitaka serikali kuliambia taifa hatua itakazochukua kurejesha fedha hizi na nyingine zozote zilizofichwa ughaibuni”

Kuhusu ishu ya mjadala kuhusu kampuni ya BAE system ya Uingereza, Mh Zitto amesema “ukilinganisha fedha iliyorejeshwa kama chenchi ya rada na fedha ambayo Tanzania iliilipa benki ya Barclays, je chenchi ya rada ilikua na thamani yoyote kifedha? mjadala wa ununuzi wa rada hauwezi kuisha kwa kufurahia kurejesha chenchi tu, mjadala huu bado mbichi kabisa kwani tunataka ukweli mtupu uelezwe kwa umma na kuona taifa lilipata hasara kiasi gani kwa ufisadi huu wa kimataifa na hatua stahiki za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wote walioliingizia taifa hasara”

Baada ya Zitto Kabwe kumaliza kuwasilisha, Mbunge wa Simanjiro (CCM) Christopher Ole Sendeka aliomba mwongozo kwa spika na kusema “tuhuma hii ni kubwa sana nilitaka kuomba mwongozo wako kwamba nani abebe mzigo huu, ni Zitto ataje majina ya wanaohusika au serikali iwataje hao wanaohusika katika utoroshaji wa fedha hizo ambazo zimeenda ughaibuni ili kila mmoja abebe msalaba wake pale itakapothibitika kwamba fedha za wananchi wa Tanzania zimepelekwa nje ya nchi bila kufata taratibu za kisheria”

No comments: