Ikiwa ni wiki ya kwanza ya ikimalizika tangu kuanza kwa michuano ya 30 ya Olimpiki jijini London, huku Afrika Mashariki ikiwa bado hoi kwa kutonyakua hata medali moja kwa kuanza vibaya, mwanga wa matumaini umeonekana, baada ya Kenya kufungua ukurasa wa mafanikio kwa medali.Wawakilishi kadhaa wa nchi za Kenya, Uganda, Tanzania, Burundi na Rwanda wakiwa wametolewa, na sasa wanariadha wa Kenya wamewafuta machozi.
Uganda nayo imejijengea matumaini, baada ya wanariadha wake kuvuka kwenye hatua za mchujo wa mbio za mita 3,000 na kuingia fainali.Tanzania inaweka tegemeo kwa wanariadha wake wanne, watakaopeperusha bendera yake Jumanne na Jumapili ya wiki ijayo, baada ya wanamichezo wake wengine watatu kutolewa.
Kwa Kenya, wikiendi imeanza vizuri kwa sababu Sally Kipyego amefanikiwa kunyakua medali ya fedha katika fainali ya mbio za mita 10,000 Ijumaa, ambapo dhahabu ilikwenda kwa bingwa mtetezi, Tirunesh Dibaba wa Ethiopia.
Dibaba hakuwa mshindani rahisi, kwani katika mashindano yaliyopita ya Olimpiki mjini Beijing alipata medali mbili za dhahabu
Kenya iling'ara zaidi kwenye mbio hizo za Ijumaa, baada ya mwanariadha wake mwingine, Vivian Cheruiyot kutwaa medali ya shaba, baada ya kupitwa na Kipyego katikati ya mbio jijini London.Kipyego alitumia dakika 30:26:37.
Cheruiyot ni bingwa wa dunia wa mwaka jana kwenye mbio za mita 10,000 na 5,000, ambapo juzi Ijumaa, kasi yake ilimfanya akamaliza mchezo kwa dakika 30:30.44. Kipyego hakuamini kupata medali hiyo muhimu ya fedha, na baada ya mbio aliishia kububujikwa machozi ya furaha."Nimelia kwa sababu ni safari ndefu, watu hawajaelewa bado ilivyo kazi ngumu na jinsi hisia zinavyochanganya kwenye mbio hizi. Unajiandaa kwa miaka mingi lakini hujui utakuja kuvuna nini siku ya mwisho.
"Mara unashitukia umekatiza mstari wa mwisho na kumaliza mbio. Kwa kweli kuna mengi yasiyoonekana tunayojinyima ili kufikia fahari hii. Kocha anaelewa na watu wachache, nashukuru sana kwa fursa nilizopata, nimefurahi sana," akasema msichana huyo mwenye umri wa miaka 26.
Kipyego anafundishwa na kocha Mark Rowland na anasema ndiye nguzo yake muhimu, kwa jinsi anavyompa moyo, ukiachilia mbali mafunzo ya muda mrefu. Kipyego ni mhitimu wa shahada ya uuguzi, na anasema kwa hatua aliyofikia, nguvu zilishamwishia na hangeweza kwa namna yoyote ile kufanya la ziada kumfikia Dibaba.
"Nilikuwa nachunga uhai wangu pia, nilijisema nikiongeza kasi huenda nisiweze hata kumaliza mbio hizi kwa hiyo ngoja niende pole pole."Nilipoangalia nikagundua Vivian (Cheruiyot) naye hakuwa anakuja kasi, nikajua naye kachona, nikaamua kumaliza taratibu," akasema akionesha uchovu wa kazi hiyo ngumu.Cheruiyot naye akizungumzia michezo hii, anasema anashukuru kupata medali ya shaba ambayo si ndogo, maana wengi wanaitafuta na kuikosa.
Anasema sasa analenga kutafuta medali kwenye mbio za mita 5,000 na kwamba amebaki kuwa mwenye furaha kubwa.
"Nilikuwa nimechoka niliposikia sauti ya kengele na sikuweza kuendelea kuwakimbiza. Kwa matokeo haya nafurahi, silalamiki wala kumlaumu yeyote, sasa najipanga kwa ajili ya mbio za mita 5,000.
"Kupata medali ya shaba kwenye Olimpiki si kitu rahisi, hasa mnapokuwa na washindani wenye uzoefu na stamina kama hawa," anasema Cheruiyot anayepewa nafasi kubwa kushinda medali kwenye mbio za mita 5,000.
Kenya ilikuwa na mwanariadha mwingine kwenye mbio hizo, Joyce Chepkurui, lakini hakuweza kufurukuta, kwani aliishia kwenye mzunguko wa 17 na kuondolewa na wahudumu.
Katika mbio za mita 400 kuryka vihunzi kwa, Joyce Zakari wa Kenya aliwashangaza wengi kwa kuvuka na kuingia nusu fainali. Hata hivyo Vincent Kiplagat Kosgei hakufanya vizuri, kwani alimaliza katika nafasi ya saba, huku mwenzake, Boniface Mucheru akishika nafasi ya sita kabla yake Wanariadha wengine wa Kenya waliofuzu ni bingwa mtetezi wa Olimpiki mita 3,000, Brimin Kipruto, bingwa wa dunia, Ezekiel Kemboi na Abel Mutai. Zakari alionesha furaha ya aina yake baada ya kufuzu, akisema; "mwili wangu upo katika hali nzuri, na ninachosubiri ni nusu fainali tu." Kipruto aliyeonekana kujawa furaha, alipohojiwa na waandishi wa habari alisema:
''Najihisi vizuri, zilikuwa mbio nzuri na sasa tunaangaza mbele ambapo suala si kukimbizana na muda bali medali."
Mfaransa Mahiedine Mekhissi, ambaye awali alijulikana kwa jina la Mekhissi-Benabbad, alionekana kuwaogopa Wakenya, kwani alisema atakuwa mpweke kwenye mbio hizo, kwa sababu atakuwa dhidi ya Wakenya watatu.
Mfaransa huyu aliyepata medali ya fedha Beijing, na hukimbia mita 1,500 na 3,000.
"Nitakuwa mwenyewe wakati Wakenya watakuwa watatu. Lakini hii hainiogofyi kwa sababu wote ni rafiki zangu," akasema kijana huyo mwenye umri wa miaka 27.
Benjamin Kiplagat afuzu kwa Uganda. Kwa upande wa Uganda, mwanariadha wake mahiri, Benjamin Kiplagat alifanya vizuri Ijumaa kwenye mbio za mchujo za mita 3,000 kuruka vihunzi, na kupata tiketi ya kuingia fainali Jumapili hii.
Kiplagat amefufua matumaini ya Waganda kwenye michezo hii. Baada ya kuanza mbio kwa kasi, katika hatua za mwisho aliteleza na kujigonga, hivyo kushindwa kufuzu moja kwa moja.Hata hivyo, kwa kuzingatia kasi yake, na kwamba alijigonga kwa bahati mbaya, alipewa nafasi moja kati ya mbili za ziada za kuingia fainali.
Kitaalamu, ikiwa hangejigonga angeweza kushika nafasi za mbele kabisa kwenye mchujo. Alikimbia kwa muda wa dakika 8:18.44, na alipewa nafasi hiyo kwa kuzingatia ni mmoja wa wanariadha wawili walioshindwa, lakini waliokwenda kasi sana.
Kiplagat alipata medali ya fedha kwenye mashindano ya vijana ya dunia yaliyofanyika 2008, lakini pia ana medali ya shaba ya ubingwa wa Afrika.Akizungumzia alivyojizuia kuanguka na kutoka kwenye mbio hizo katika tukio hilo, Kiplagat mwenye umri wa miaka 23 alisema alijipa moyo, akijua anaibeba nchi yake.
"Nilijaribu kwa nguvu zote niweze kufuzu, nashukuru nimefanikiwa kufanya hivyo, sasa najiandaa kwa ajili ya Jumapili," akasema na kuongeza kwamba amedhamiria kupata medali wikiendi hii.Simanzi kwa Uganda ilitokea baada ya mwanariadha wake mwingine, Jacob Araptany kushindwa kufuzu, alipotumia dakika 8:35.85 na kuwa wa saba.
Kama mwenzake Kiplagat, mwanariadha huyu alitawala vyema hatua za mwanzo za mbio, akionekana angemaliza katika nafasi za juu, lakini alishindwa kadiri mbio zilivyokaribia ukingoni.Araptany alifanya vizuri kwenye hatua za aali za mashindano ya riadha ya Afrika nchini Benin Juni mwaka huu, lakini tatizo likawa mwishoni, akashindwa kung'aa.Shujaa mwingine wa Uganda anayetupiwa macho niMoses Kipsiro (26) katika mbio za mita 5,000 anayesema iwe iwavyo, hatakimbia tena mita hizo, bali anahamia kwenye marathon Olimpiki ijayo.
Kipsiro mwenye rekodi ya kupata medali katika kila mashindano makubwa anayoshiriki, anatarajia kufanya vyema wikiendi hii."Sasa nabadilisha mbio, nitaingia barabarani mwishoni mwa mwaka huu nikikimbia marathon," anasema na kuongeza kwamba atasikitishwa sana akistaafu bila kupata medali ya Olimpiki.Kipsiro ana medali mbili za dhahabu za Jumuiya ya Madola na wikiendi hii anashiriki mbio za mita 10,000 kabla ya wiki ijayo kuingia zile za mita 5,000.
"Sipo katika hali nzuri kama ambavyo ningependa kuwa, lakini nitapambana, pengine nikikosa medali itaniumiza kwa maisha yangu yote…nadhani nitafanya vizuri zaidi kwenye mbio za mita 10,000," akasema.Uganda ilileta wanamichezo 16 kwa ajili ya michezo mitatu katika Olimpiki ya London. Hao ni pamoja na Jacob Araptany,Thomas Ayeko, Abraham Kiplimo, Stephen Kiprotich, Moses Kipsiro, Geoffrey Kusuro na Julius Mutekanga.Wengine ni Janet Achola, Dorcus Inzikuru, Annet Negesa, Jane Suuto, Edwin Ekiring, Ganzi Mugula, Jamila Lunkuse na Charles Ssekyaaya.
Rwanda na Burundi hazijaona mwanga
Rwanda na Burundi bado zinasubiri majaliwa yao kwenye mashindano haya, zikiomba dua. Ndoto za Alphonsine Agahozo ambaye alikuwa tegemeo kubwa la Rwanda, ziliyeyuka Ijumaa. Alitarajia kufanya vyema kwenye kuogelea mita 50 'freestyle' kwa wanawake pale Aquatic Centre, lakini alitumia sekunde 30.72, akishika nafasi ya tatu miongoni mwa washindani wanane.Pamoja na kujitahidi huko, ufanisi wake haukutosha kumjalia nafasi kwenye nusu fainali, kwani katika kundi la waliokwenda kasi zaidi, wapo wawili waliomzidi, hivyo kumnyima nafasi. Rwanda waliokuwa wakijiandaa kwa mashindano haya huko Bury St Edmunds prior to the Games.Sasa Rwanda itabidi isubiri kwenye riadha kwa washiriki wake wa mbio ndefu za mita 10,000.Kocha wao, Innocent Rwabuhihi alisema alikuwa na matumaini ya kufanya vizuri.Mmoja wa wanariadha hao ni Claudette Mukasakindi, mwenye rekodi ya kukimbia kwa dakika 33:51.57.
Mwingine ni Robert Kajuga anayeshiriki mbio za mita 10,000 pia kwa wanaume. Hata hivyo, Kocha Rwabuhihi anasema wachezaji wake walikuwa na tatizo la kuzoea hali tofauti ya hewa ya London, ambayo hubadilika karibu kila siku.
Rwanda ilikuwa na washiriki saba, ambao ni Alphonsine Agahozo katika kuogelea, Robert Kajuga, Claudette Mukasakindi na Jean Pierre Mvuyekure kwenye riadha. Wengine ni Jackson Niyomugabo kwenye kuogelea, Adrien Niyonshuti katika mbio za baiskeli za milimani na Fred Yannick Uwase anayepambana kwenye judo.Burundi pia bado haijapata medali, licha ya kuwa na mmoja wa wakongwe wa Olimpiki, Venuste Niyongabo.
Huyu ni Mrundi wa kwanza kuwa bingwa wa Olimpiki, kwani katika Michezo ya Atlanta, Marekani mwaka 1996 alitwaa medali ya dhahabu katika mbio za mita 5,000. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza Burundi kushiriki Olimpiki, ikiwa na wanamichezo saba, na tangu hapo imeshiriki michezo yote ya majira ya joto ya Olimpiki.Mwaka 1996, Aloys Nizigama wa Burundi alikaribia kutwaa medali ya shaba, alipomaliza mbio za mita 10,000 akiwa nafasi ya nne.
Artehemon Hatungimana ana rekodi ya Mrundi wa kwanza kushiriki michezo mitatu ya Olimpiki, ambapo alishindana kwenye mita 800 mwaka 1996, tena akarudia mwaka 2000 na mwaka 2004.Kuanzia mwaka 2004, timu ya Burundi imekuwa ikijumuisha waogeleaji. Katika riadha, Joachim Nshimirimana ameshiriki nusu marathon mara mbili, mojawapo ikiwa mwaka 2008. Mwaka huu, washiriki wa Burundi ni Beni Bertrand Binobagira na Elsie Uwamahoro katika kuogelea; Olivier Irabaruta, Francine Niyonsaba na Diane Nukuri katika riadha; Odette Ntahomvukiye kwenye judo.Tanzania bado yajipa matumaini
Baada ya wachezaji wake watatu kuondolewa kwenye mashindano kwa kushindwa mbele ya washindani wao, Tanzania inawategemea wanne waliobaki. Waogeleaji wake, Magdalena Moshi na Ammaar Ghadiyali walitolewa, Moshi akishika nafasi ya mwisho kwenye mchujo kati ya washiriki saba. Ghadiyali alikuwa wa tatu, ambapo wawili wa mbele yake walivuka.
Bondia pekee, Selemani Kidunda alipoteza mchezo wake Belous wa Moldova kwa pointi 20-7. Kidunda hakuonesha kiwango kizuri, hivyo mpinzani wake hakuwa na kazi ngumu ya kumshinda. Wanariadha waliobaki kwa upande wa Tanzania ni Zakhia Mrisho anayekimbia Jumanne hii mbio za mita 5,000, kujaribu kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Wengine watatu wataingia kwenye marathon barabarani jijini London Jumapili ikayo. Hawa ni Samson Ramadhani, Mohamed Msenduki na Faustine Musa. Mwaka 2006 Ramadhani alitwaa medali ya dhahabu kwenye Michuano ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Melbourne, Australia, alipotumia 2:11:29.
Msenduki naye ameshinda mashindano mbalimbali ya Marathon, na anatarajiwa kutumia uzoefu huo jijini London. Musa anashiriki marathon kwa mara ya pili, baada ya mbio za Warsaw, Poland alikoshika nafasi ya tatu.Tanzania haijawahi kufanya vizuri kwenye Olimpiki tangu mwaka 1980, wanamchezo wake, Filbert Bayi na Suleiman Nyambui walipotwaa medali za fedha katika mashindano yaliyofanyika nchini Urusi.Marekani na China zinachuana vikali kwenye nafasi za mwanzo, huku wenyeji Uingereza nao wakichomoza kwa medali kadiri michezo inavyoendelea.Afrika Kusini ndiyo pekee barani iliyopata medali za dhahabu (tatu), pia ina moja ya fedha. Afrika Mashariki ikisubiri kuona watakacholeta wanamichezo wake baada ya medali za Kenya.
Habari kwa hisai ya Israel Saria, BBC
No comments:
Post a Comment