Thursday, December 13, 2012

Ikulu Ilivyowakera Wahariri

•  Wasota kwa saa nne kusubiri mkutano wao na Kikwete

WAHARIRI wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, wamelazimika kusota kwa zaidi ya saa nne Ikulu, kusubiri mkutano wao na Rais Jakaya Kikwete.
Hali hiyo ilitokea jana wakati wahariri wakisubiri mkutano wao na Rais Jakaya Kikwete na mgeni wake, Rais Marc Ravalomanana, aliyeondolewa madarakani kwa nguvu nchini Madagascar.

Katika mkutano huo wa dharula ulioitishwa na Rais Kikwete mwenyewe, ulikuwa na lengo la kuzungumzia msimamo wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC ) kuhusu mgogoro wa Madagascar na kutoa fursa kwa Rais Ravalomanana anayeishi uhamishoni nchini Afrika Kusini, kueleza msimamo wake.
Wakati Rais Kikwete akiwa ziarani jijini Dar es Salaam, Ikulu iliwasiliana na wahariri wa vyombo vya habari na kuwataka wafike Ikulu saa sita kwani Rais Kikwete alitaka kufanya mkutano wa dharula na wakuu hao wa vyombo vya habari saa saba.

Wahariri hao walianza kuitikia wito wa kufika Ikulu kuanzia saa sita tayari kwa mkutano huo ambao kwa mujibu wa mawasiliano na Ikulu, ulipangwa kufanyika saa saba baada ya Rais Kikwete kukatisha ziara yake na kisha kuendelea nayo baadaye jioni.

Ilipofika saa saba, hakukuwa na dalili zozote za Rais Kikwete na mgeni wake kufika ukumbini na hakuna taarifa zozote zilizotolewa na watendaji wa Ikulu.
Wanahabari hao waliendelea kusubiri na ilipofika majira ya saa nane mchana, bado hakukuwa na taarifa za muda halisi wa kuanza kwa mkutano huo.

Ilipofika saa tisa, mmoja wa maafisa wa Ikulu, aliwaambia waandishi wa habari hao kwamba mkutano huo ungelianza saa 9.30 na kwamba tayari Rais Kikwete alikuwa amesharejea Ikulu na kujiandaa kukutana nao.

Hata ilipofika saa 9.30, hakukuwa na dalili za kuanza mkutano huo, hali iliyowafanya baadhi ya wahariri kukaa vikundi kuzungumzia adha hiyo, huku wengine wakichapa usingizi.

Rais Ravalomanana aliwasili viwanja vya Ikulu majira ya saa 9.45 na kwenda kukutana na Rais Kikwete kabla ya kuingia ukumbini kuanza mkutano huo.
Majira ya saa 10 jioni, maafisa wa Ikulu na watu wa usalama, walijipanga kujiandaa kuwakaribisha viongozi hao ukumbini, lakini baadaye walirejea kwenye nafasi zao za awali baada ya kuambiwa kwamba ungeaanza saa 10.30 jioni.
Hatimaye ilipofika saa 10.28, Rais Kikwete na mgeni wake waliingia ukumbini na kuanza mkutano huo uliodumu kwa takriban dakika 30.

Wakati mkutano huo unamalizika majira ya saa 11 jioni, Mkurgenzi wa Mawasilino Ikulu, Salva Rweyemamu, aliwashukuru wahariri kwa uvumilivu wao, lakini hakueleza sababu za mkutano huo kuchelewa kuanza saa saba kama ilivyopangwa na badala yake ulianza saa 10.30 jioni.

Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa hakukuwa na mawasiliano sahihi kati ya watendaji wa Ikulu na vyombo vya habari na kusababisha kero hiyo.
Hata hivyo akizungumza katika mkutano huo, Rais Kikwete alisema katika mkutano wa wakuu wa nchi za SADC uliomalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, umeazimia kuwa Rais Ravalomanana arejee Madagascar bila masharti na kuhakikisha ulinzi na usalama wake.

Alisisitiza kuwa SADC imesisitiza Ravalomanana arejee nchini mwake na kupuuza tishio la wapinzani wake la kumtaka arejee nchini humo baada ya uchaguzi.
Pia alisema wamekubaliana kwamba Rais Ravalomanana na hasimu wake anayeongoza Madagascar kwa sasa, Rais Andry Rajoelina wasigombee urais katika uchaguzi mkuu ujao, unaotarajiwa kufanyika Mei mwakani.

“Ili kudumisha amani nchini Madagascar, viongozi wa SADC wamekubaliana kuwa Rais Rajoelina na Rais Ravalomanana wasigombee urais,” alisema Rais Kikwete.
Kwa upande wake, Ravalomanana alikubali kurejea nchini humo na kuwa raia wa kawaida na kuahidi kutoa ushirikiano katika kuijenga upya Madagascar iliyoathirika kwa kiasi kikubwa kiuchumi.

Alisema pia amekubali kutogombea urais Mei mwakani, lakini anaweza kugombea miaka mitano baadaye kama hali itaruhusu.

Rais Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa SADC, alimshukuru Ravalomanana kukubaliana na viongozi wa SADC na kuahidi kuzungumza na Rais Rajoelina.

http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=43437

No comments: