ZAIDI ya wanafunzi 300 wa udaktari kutoka nchi mbalimbali duniani wanatarajiwa kufanya mkutano wa kimataifa utakaojadili jinsi ya kutatua migogoro katika sekta ya Afya kwenye ukanda wa Afrika.
Hayo yalisemwa na Rais wa Chama cha Wanafunzi wa Udaktari Tanzania(TAMSA) Francis Tegete wakati akizungumza na waandiishi wa habari jana jijini Dar es salaam.
Alisema kuwa washiriki wa mkutano huo watajadiliana jinsi ya kuboresha rasilimali watu ,sera za afya na miundo mbinu ya kutolea huduma ya afya katika nchi zao ili kutimiza malengo ya Melinia .
Alisema kauli mbiu ya mkutano huo inalenga kujadili migogoro ya afya barani na jinsi ya kuitatua kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wananchi hasa wanaoishi katika mazingira magumu na vijijini.
Tegete aliongeza kuwa mkutano huo utakuwa muhimu kwa wanafunzi wa udaktari nchini kupata fursa ya kubadilishana uzoefu na wenzao wa jinsi gani wanavyoweza kusaidia katika utoaji wa huduma za afya ikiwemo upunguzaji wa vifo vya watoto na mama wajawazito.
Alisema kuwa mkutano huo utafunguliwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt Hussein Mwinyi siku ya Jumanne tarehe 18 na kumalizika 22 Disemba mwaka huu jijini Arusha.
Baadhi ya washiriki wanatoka Marekani , Uingereza, Lebanon, Sierra Leone , Uganda, Kenya , Rwanda, Burundi, Congo, Korea Kusini, Sudan, Zambia , Ethiopia na Sweden .
Na: Heka Wanna na Shakila Galus-MAELEZO_DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment