Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na waandishi wa habari kwenye makazi yake mkoani Dodoma jana kuhusu hatua zilizochukuliwa kudhibiti vurugu za gesi mkoa wa Mtwara.Kulia ni waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel
Madai kwamba gesi hiyo inapelekwa Bagamoyo yalikuwa moja ya ujumbe mkuu uliokuwa umeandikwa kwenye baadhi ya mabango wakati wa maandamano ya Desemba 27 mwaka jana yaliyofanyika Mtwara Mjini, yakiratibiwa na baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani.
MOJA ya mambo yaliyoamsha hisia za wakazi wa Mkoa wa Mtwara hadi kushinikiza kwa vurugu wakitaka gesi isitoke mkoani humo, ni taarifa kuwa nishati hiyo ingepelekwa wilayani Bagamoyo, nyumbani kwa
Rais Jakaya Kikwete.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema jana nyumbani kwake mjini Dodoma kuwa, mbali na imani hiyo, amebaini pia kuwa mpasuko ndani ya CCM mkoani Mtwara na harakati za kisiasa ni sababu nyingine iliyochochea mgogoro huo.
Pinda alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mgogoro huo ambao ulisababisha vifo vya watu wanne huku wengine wakijeruhiwa vibaya na uharibifu mkubwa wa mali zikiwamo nyumba za wabunge kuchomwa moto na namna alivyofanikiwa kuuzima.
Waziri Mkuu alifanya ziara ya siku mbili mkoani Mtwara, Januari 25 na 26 mwaka huu na kufanikiwa kuzima mgogoro huo baada ya kufanya mazungumzo na makundi mbalimbali ya wadau wa gesi mkoani humo.
“Sasa hili nililitolea ufafanuzi kwa kukanusha kuwa siyo kweli kwamba gesi inakwenda Bagamoyo. Lakini pia baada ya kukaa nao nilibaini kuwa hata viongozi wenyewe wa CCM hawako pamoja,” alisema Pinda na kuongeza:
“Pamoja na hayo nikachukua maelezo kuhusu matatizo yao mengine na nikawaahidi kwamba nitayafikisha katika mamlaka husika ili waweze kuona namna ya kufanya.”
Madai kwamba gesi hiyo inapelekwa Bagamoyo yalikuwa moja ya ujumbe mkuu uliokuwa umeandikwa kwenye baadhi ya mabango wakati wa maandamano ya Desemba 27 mwaka jana yaliyofanyika Mtwara Mjini, yakiratibiwa na baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani.
Pinda alisema viongozi wa kisiasa mkoani Mtwara wakiwamo wabunge, wameonekana kuwa na mpasuko unaosababisha uchochezi kwa makundi ya watu.
Alipotakiwa kuzungumzia madai hayo ya Waziri Mkuu, Katibu wa CCM Mkoa wa Mtwara, Alhaji Masoud Mbengula alikiri chama hicho kumeguka na akataja sababu kuwa ni makundi yaliyotokana na uchaguzi wa ndani uliofanyika mwaka jana.
“Tusiwe wanafiki, ni kweli kuna makundi ndani ya chama… wabunge hawako pamoja na ndiyo hali iliyotufikisha hapa… suala hili lipo wazi kabisa,” alisema Alhaji Mbengula.
Kamati ya Spika hatihati
Akizungumzia Kamati ya Bunge iliyotarajiwa kuundwa na Spika kwenda Mtwara kwa ajili ya kuwasikiliza wananchi wa huko, Pinda alisema hawezi kuingilia mhimili huo wa Dola isipokuwa atatoa taarifa bungeni na kama Spika ataona wabunge wameelewa, basi ataamua lolote.
“Nitakuwa na nafasi ya kuzungumzia jambo hili ndani ya Bunge na Spika akiona wabunge wamenielewa bila shaka atasitisha lakini akiona bado inafaa ataamua yeye,” alisema.
Kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari jana, kiongozi huyo alifanya mazungumzo na Mawaziri wanaotoka Mkoa wa Mtwara ambao ni George Mkuchika (Utawala Bora) na Hawa Ghasia (Tamisemi) pamoja na wawekezaji wa kutoka China ambayo alisema yalilenga kuwapa halihalisi ya huko.
Kauli ya Nchimbi
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alisema vurugu hizo zimefikia mwisho na Serikali haitavumilia tena machafuko ya aina hiyo.
Dk Nchimbi alisema timu ya wataalamu ipo Mtwara kuweka mambo sawa na kusema Serikali itatimiza majukumu yake pasi na shaka yoyote na kusisitiza kuwa haiwezi kukubali Tanzania ikawa vipande.
Alisema Serikali inafanya tathmini kujua hali ilivyo Mtwara na ikibidi itasitisha shughuli zote za kisiasa mkoani humo.
No comments:
Post a Comment