Thursday, January 31, 2013
MTUHUMIWA WA MAUAJI YA MWANGOSI NA ASKARI WENZAKE WAMDHARAU HAKIMU, WAOMBA MSAMAHA
Askari polisi wakimrejesha mahakamani mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa Channel Ten na mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Iringa Daudi Mwangosi, askari wa FFU mwenye namba G2573 Pasificus Cleophace Simoni (aliyevaa kofia nyekundu) baaada ya kutoroshwa kizimbani kabla ya mahakama kumaliza shughuli zake jana.
Pasificus Cleophace Simoni akirudishwa ndani ya mahakama.
SAKATA la mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten mkoani Iringa marehemu Daudi Mwangosi limezidi kuchukua sura mpya baada ya askari waliomfikisha mtuhumiwa huyo wa mauaji askari wa FFU mwenye namba G2573 Pasificus Cleophace Simoni (23) kumtibua hakimu na kuagiza mtuhumiwa huyo kurudishwa tena kizimbani kwa kudharau mahakama hiyo.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 5.35 asubuhi kwa askari hao watatu ambao majina yao hayakuweza kufahamika mara moja kumshusha kizimbani mtuhumiwa huyo wa mauaji na kumkimbizia mahabusu kama njia ya kukwepa kupigwa picha na wanahabari waliokuwepo hapo lilitokea mara baada ya mahakama hiyo kuombwa kutaja tarehe nyingine ya kutajwa kesi hiyo.
Huku bado mahakama ikiwa inaendelea kwa hakimu kutaja tarehe ya kesi hiyo ya mauaji namba 1 ya mwaka 2012 mtuhumiwa huyo alishuka kizimbani akiwa kavaa kofia ya sweta (mzula) na miwani ya nyeusi na kuanza kuondoka.
Wakati hakimu akijiandaa kusimama ili kuhitimisha shughuli za kimahakama kwa siku hiyo ghafla alijikuta anabaki na mwanasheria wa mahakama, kalani wake, wanahabari, askari mmoja na ndugu wawili wa mtuhumiwa huyo huku askari watatu wenye silaha na mtuhumiwa huyo wakiwa tayari wameondoka ndani ya chumba cha mahakama.
“Mbona hao askari wanamtoa mtuhumiwa bila utaratibu wa mahakama? hebu mwanasheria waambie wamrudishe ndani mtuhumiwa ....huu si utaratibu mbona wanafanya fujo mahakamani hao?” alisikika akisema hakimu mkazi wilaya ya Iringa, Dyness Lyimo.
Hata hivyo pamoja na jitihada za mwanasheria wa serikali, Adolf Maganda kuwaita kwa sauti askari hao kuwataka kumrudisha ndani ya mahakama mtuhumiwa huyo, bado askari walizidi kukimbia na mtuhumiwa kwenda nae mahabusu na baada ya dakika kama 5 hivi ndipo mwanasheria huyo aliporejea na askari hao na mtuhumiwa ambaye hata hivyo hakwenda kusimama kizimbani na badala yake alikwenda upande wa kushoto wa mahakama hiyo ambako alikuwa amekaa mwanzoni kabla ya mahakama kuanza na kuketi katika kiti huku akiwa amevaa miwani na kofia yake.
Kutokana na tukio hilo hakimu alilazimika kuwahoji askari hao watatu kwa vurugu hizo walizozifanya kwa kuwauliza swali moja pekee kuwa wanaona walichofanya ni sahihi na askari hao kuomba msahama.
Mwendesha mashtaka wa jamhuri, Adolf Maganda aliiomba mahakama hiyo kutaja tarehe nyingine ya kutajwa tena kesi hiyo ambayo ilitajwa Januari 27 na mtuhumiwa huyo kushindwa kufika kutokana na tatizo la ugonjwa lililokuwa likimsumbua.
Hata hivyo mahakama hiyo iliahirisha kesi hiyo hadi Februari 14 mwaka huu kesi hiyo itakapofikishwa mahakamani hapo kwa kutajwa tena.
Mtuhumiwa huyo anatuhumiwa kumuua kwa makusudi kwa bomu aliyekuwa mwandishi wa habari wa Channel Tena mkoa wa Iringa marehemu Mwangosi Septemba 2 mwaka jana katika kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa wakati wa vurugu kati ya polisi na wafuasi wa Chadema kinyume na kifungu cha sheria namba 148 kifungu kidogo 5A.i cha makosa ya jinai. Kwa mujibu wa kesi za jinai, sheria kifungu 196 kanuni ya adhabu Cap. 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
(Picha na Francis Godwin)
Na Francis Godwin, Iringa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment